Virusi vya corona: Waziri wa Afya Dorothy Gwajima asema Tanzania haina haja ya kuagizia chanjo ya corona kwa sasa

Waziri wa Afya nchini Tanzania Dr. Dorothy Gwajima
Maelezo ya picha, Waziri wa Afya nchini Tanzania Dr. Dorothy Gwajima

Waziri wa Afya nchini Tanzania Dkt. Dorothy Gwajima amesema Tanzania haina mpango wa kuagiza chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Akiongea na waandishi wa habari hii leo huko jijini Dodoma, Waziri Gwajima ameongeza kusema kuwa Tanzania haina maambukizi ya Covid19 bali amewataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kutumia dawa za asili.

''Kwa sasa wizara haina mpango wa kupokea chanjo ya corona au Covid 19, inayoripotiwa kuwepo na kutumika katika mataifa mengine'', alisema

Alisema kwamba serikali kupitia wizara ya Afya ina taratibu zake za kufuata pale inapotaka kupokea bidhaa yoyote ya afya ambayo amesema hatua hiyo hufanyika baada ya serikali kujiridhisha.

Akiongozana na naibu wake pamoja na mtaalamu wa tiba asili Kutoka NIMR Bi Gwajima ameonyesha jinsi tiba hiyo asili inavyotengezwa kwa kutumia tangawizi, vitunguu, limau na pilipili.

Kauli hii ya waziri inakuja wakati ambapo makamo wa rais wa kwanza Zanzibar Maalim Seif Hamad Sharif, pamoja na mkewe na baadhi ya wasaidizi wake wamethibitika kupata maambukizi ya corona na kuendelea na matibabu.

Waziri Dorothy Gwajima akielezea jinsi Watanzania watakavyoangamiza corona
Maelezo ya picha, Waziri Dorothy Gwajima akielezea jinsi Watanzania watakavyoangamiza corona

Hatahivyo Maalim Seif amesema kuwa anaendelea kupata afueni baada ya matibabu hayo.

Tahadhari

Bi Gwajima amesema kwamba taifa la Tanzania lipo salama lakini akawataka raia kuchukua tahadhari kutokana na kuenea kwa ugonjwa huo katika mataifa jirani.

''Kwa hivyo ninachotaka kusema hapa ni kwamba nchi yetu ipo salama , tunasikia kwa jirani huko kuna shida, usisubiri vitoke kwa jirani vije kwasababu tunaingiliana maisha, sisi tunajiandaa kwa maisha,''alisema

''Hizi ndio silaha unatengeneza unakunywa, mazoezi maji mengi, kupumzika, bidhaa za tiba asili'', aliongezea bi Gwajima.

Maelezo ya video, Jinsi ya kutengeneza tiba asili Tanzania

Ili kujilinda dhidi ya corona Bi Gwajima amewataka wananchi kujielekeza kwenye:

Elimu ambayo imekuwa ikitolewa na wataalamu wa Afya ikiwemo kuimarisha usafi wa mazingira, usafi wa kibinafsi, kunawa mikono kwa kutumia maji na sabuni, kwa kutumia vipukushi, kujifukiza, kufanya mazoezi mbalimbali , kula lishe bora, kunywa maji ya kutosha bila kisahau matumizi ya tiba asili ambayo taifa la Tanzania limejaliwa nazo.

Maelezo ya video, Tiba asili Tanzania

Hivi majuzi waziri wa ofisi ya rais tawala ya mikoa na serikali za mitaa , Selemani Jafo alitangaza kwamba taifa hilo litaanza kampeni ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona kuanzia Jumatatu tarehe 1 ,Februari 2021.

Akizungumza alipoambatana na rais wa Tanzania John Pombe Magufuli mkoani Tabora alisema kwamba maradhi hayo hayana nafasi na kwamba raia wa taifa hilo wataendelea kumuomba mwenyezi Mungu.

'Hapa corona haina nafasi, tutaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu, kama Mh.Rais ulivyotuelekeza na umesema watu wajifukize sana, Na Rais naomba nikwambie Jumatatu tunaanza kampeni nyingine ya juma zima season three (awamu ya tatu), nyungu kama kawaida, tunajifukiza, tunakula matunda, tunamuomba Mungu, tunaanza tarehe moja mpaka tarehe saba, hatupoi kazi inaendelea, uchumi wetu lazima usimame'' Alisema Waziri Jafo.

Kauli hii imekuja wakati kukiwa na aina mpya ya virusi vya corona aina ya Afrika Kusini, ambavyo vimekuwa vikienea katika nchi za Kiafrika.

Je Msemaji wa serikali alisema nini?

Siku ya Ijumaa wiki iliopita, msemaji Mkuu wa serikali nchini Tanzania Dkt. Hassan Abbas alisema Tanzania inazingatia miongozo yote ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona na hata wakati huu ambao dunia inapambana na wimbi la pili la maambukizi ya virusi hivyo..

Akihojiwa na kitoa cha redio cha EFM kilichopo jijini Dar es salam, Dkt. Abbas alisema "Sisi Tanzania msimamo wetu ni ule ule, tunafahamu tatizo lipo duniani na dunia inahangaika lakini cha kwanza Watanzania waondoe hofu wizara ya afya ilishatoa miongozo.

WHO ilisema nini hapo awali?

Siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kutaka wizara ya afya kutokimbilia chanjo ya corona bila kujiridhisha, Shirika la Afya Duniani WHO liliitaka nchi hiyo kujiandaa na chanjo ya Corona kama mataifa mengine duniani.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao,mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshdiso Moeti alisema kuwa Tanzania inatakiwa kutumia mwanya wa upatikanaji wa chanjo kwa faida ya wananchi na kanda ya Afrika mashariki kwa ujumla.

''Tumeanza kuwasiliana upya na ngazi za juu za uongozi, na tunatoa mchango wetu kama ilivyokua hapo mwanzo, na tunataka kushirikiana na Tanzania, kwa niaba ya watu wa Tanzania, nchi jirani na dunia kwa ujumla. Sehemu ya mawasiliano yetu na Tanzania ni kukumbusha serikali kuwa, hii ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa'' anasema Dkt. Moeti.

WHO inasema kuwa imekua ikitoa mchango na kuwasiliana na serikali ya Tanzania kuanzia mwanzo wa janga hili la Corona.

Shirika hilo pia limesisitiza Tanzania kutoa takwimu za mwenendo wa Corona nchini ili iwe rahisi katika kupambana na kuzuia maambukizi mapya.

''Moja ya makubaliano ya wanachama ni kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa, nimewakumbusha serikali ya Tanzania na ninayo kumbukumbu kwa maandishi kuwa wao ni sehemu ya wanachama hivyo wanatakiwa kuitikia wito huu. Tuna imani kuwa mawasiliano yetu kuhusu chanjo yatazingatiwa ili kukabili maambukizi ya virusi," ameongezea Dkt. Moeti.