Tanzania 'inatumia sera ya hatimiliki ya Twitter kuwanyamazisha wanaharakati'

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Na Dickens Olewe
- Nafasi, Mwanahabari wa BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Sera ya Twitter inayokabiliana na ukiukaji wa hatimiliki inazidi kutumika vibaya ili kuzilenga akaunti za mitandao ya kujihami zinazomilikiwa na wanaharakati wa haki za kibinadamu nchini Tanzania kwa lengo la kuwanyamazisha , wamesema wanaharakati wa haki za intaneti.
Kila siku katika mtandao wa Twitter , Kigogo, jina la Kiswahili lenye maana ya mtu maarufu ama mtu tajiri huandika tetesi mpya zinazoendelea katika serikali ya Tanzania.
Maelezo yanachukiza na kushangaza wakati mwingine lakini wafuasi wa Kigogo wanaokaribia kuwa 400,000 hupenda ufichuzi huo ambao hupamba matukio huku mara kadhaa ukikosea kuhusu maudhui yake.
Alipigwa marufuku katika Twitter
''Mimi ni mfichuzi na hufichua masuala ya ufisadi na unyanyasaji wa haki za kibinadamu nchini humo'', Kigogo ambaye utambuzi wake ni siri kubwa aliambia BBC.
Lakini muda mfupi kabla ya uchaguzi wa tarehe 28 mwezi Disemba , Twitter ilifutilia mbali akaunti ya Kigogo@2014 kutokana na zaidi ya malalamishi 300 kwa mtandao huo wa kijamii kwamba akaunti hiyo ilikuwa inakiuka hatimiliki - madai ambayo Kigogo ameyakana.
Wanaharakati wa haki za Intaneti Acces Now wanadai kwamba sera hiyo inazidi kutumiwa na serikali ya Tanzania kuwanyamazisha wakosoaji wake.
Twitter haijajibu moja kwa moja madai hayo lakini ilitoa taarifa mwezi Oktoba ikipinga kuzuia mitandao ya kijamii wakati ambapo uchaguzi unakaribia.
Katika tukio moja ambalo Kigogo alilielezea, zaidi ya machapisho yake 1,000 yalitumika kuanzisha tovuti tatu, mlalamishi baadaye alizitumia tovuti hizo kusema kwamba hatimiliki zake zimekiukwa.
''Baada ya akaunti yangu kufungwa kwa muda niliandikia Twitter lakini nilikuwa nikizungumza na roboti na sio binadamu . Nilikuwa nikipata majibu ambayo yalikuwa yamerekodiwa . hakuna akili ya binadamu ilitumika'' , Kigogo alisema .
Shambulio hilo lilijiri baada ya Kigogo kuchapisha ujumbe katika mtandao wa Twitter kuhusu njama ya serikali kufanya udanganyifu kwa kutumia makaratasi ya kupigia kura kabla ya uchauzi ambapo rais Magufuli alikuwa akiwania muhula wa pili.
Tume ya uchaguzi ya Tanzania ilikana madai ya udanganyifu kabla na hata baada ya uchaguzi.

Chanzo cha picha, AFP
Walalamishi waliiomba Twitter kumsaka Kigogo kwa ukiukaji wa haki za sheria ya hatimiliki za Marekani ama DMCA ambapo Twitter na kampuni nyengine maarufu za teknolojia nchini Marekani ni sharti wafuate sheria zake duniani.
Inatoa mwelekezo kuhusu jinsi ya kusimamia malalamishi ya hatimiliki ikiwemo jinsi ya kukabiliana na ukiukaji.
Lakini wanaharakati wa haki za intaneti sasa wanasema kwamba kumekuwa na idadi kubwa ya malalamishi ya DMCA kwa lengo la kuwanyamazisha wanahabari, wanaharakati, na mashirika ya kijamii ambayo huripoti matukio ya unyanyasaji wa haki za kibinadamu.
'Walitaka kunitambua'
Shirika hilo linasema kwamba limekabiliana na kesi tisa ambapo malalamishi ya hatimiliki yametumika kulenga akaunti za watu binafsi nchini Tanzania.
''Baada ya Twitter kuifuta akaunti yangu kwa muda, nilitakiwa kutoa habari zangu binafsi kama vile anwani yangu na nambari ya simu ambayo walisema watampatia mlalamishi'', Kigogo alisema.
''Mpango uliokuwepo ulikuwa majasusi wa Tanzania kupata maelezo zaidi kunihusu ambayo yangewasaidia kunitambua, lakini nilikataa''.
Sera ya Twitter inashauri jinsi mtu yeyote anavyoweza kukabili malalamishi ya hatimiliki. Akaunti ya Kigogo ilifutwa mara mbili kwa jumla ya siku 12, kabla ya shambulio la mwezi Oktoba. ''Akaunti hiyo ilikua imedukuliwa …mara tatu, na watu ninaoshuku kuwa majasusi wa Tanzania'', alisema Kigogo.
BBC iliitaka Twitter kutoa tamko lake lakini msemaji wake alitupeleka katika chapisho ambalo kampuni hiyo ilichapisha mkesha wa uchaguzi wa Tanzania ikiitaka serikali ya taifa hilo kutofunga intaneti nchini humo.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe

Kufungwa kwa intaneti nchini Tanzania kulianza siku chache kabla ya uchaguzi.
Watumiaji wa simu walizuiwa kutoweza kutuma ujumbe huku wengine wakidai kwamba ujumbe mfupi ulio na majina ya viongozi wa upinzani ulizuiwa.
Mitandao mikubwa ya kijamii kama vile Facebook , Twitter na Instagram ilifungwa ama hata kuzuiwa. Ilikuwa vigumu kuingia katika mtandao wa Twitter am a hata simu ya rununu, ijapokuwa baadhi ya watu wanatumia mtandao wa kibinfasi wa VPN ili kukiuka ufungaji huo wa mtandao.
Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania hivi majuzi aliuliza ni kwanini mtandao wa kijamii wa Twitter bado unaminywa nchini humo?
"Je kuna mtu amesahau kuwasha Twitter," aliulizia Balozi huyo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Chanzo cha picha, AFP
Kulingana na Peter Micek, mkuu wa sheria katika kundi la wanaharakati wa haki za mtandaoni Acces Now, Shirika la mawasiliano nchini Tanzania liliweka vifaa ambavyo vingeathiri mtandao wote , kufunga tovuti na kuzuia mawasiliano ili picha na video zisiweze kusambazwa .
BBC ilitafuta tamko la halmashauri ya mawasiliano nchini Tanzania lakini haikuzungumza.
Wanaopinga na wasiopinga wote wamehusishwa na uvumi kuhusu mmiliki wa akaunti ya Twitter ya Kigogo@2014 na mahala anapoishi.
Wengine wanasema kwamba inaendeshwa na mtu mwenye uhusiano mzuri na maafisa wa serikali au wakala.
Wengine wamejaribu kutafuta sababu za utumizi wa sura ya msanii wa muziki wa Hip Hop nchini Marekani Jay Z kama picha iliotumiwa sana katika akaunti nyengine zinazofanana na ile ya Kigogo.

Chanzo cha picha, Kigogo/Twitter

Maafisa kadhaa wa Tanzania wamesema wazi walikuwa wanamsaka jamaa anayemiliki akaunti hiyo wakimlaumu kwa kutoa siri za serikali , uchochezi, kusambaza uwongo na kutishia usalama wa kitaifa.
Ujumbe wa Kigogo hunakiliwa na kusambazwa katika mtandao wa WhatsApp na kutoa habari sambamba katika taifa ambalo kumekuwa na msako mkali wa vyombo vya habari na wakosoaji wa serikali tangu rais Magufuli kuchukua madaraka 2015.
Kabla ya kushinda awamu ya pili katika uchaguzi uliokumbwa na utata mwezi Oktoba, serikali ya bwana Magufuli ilipitisha sheria kama ile ya kudhibiti maudhui mitandaoni na ile ya kukabiliana na uhalifu wa mitandao ambayo inaagiza kuwepo kwa sajili ya mabloga wote mbali na mikahawa ya mitandao kuweka kamera za CCTV na kuwapiga faini wale wanaokiuka sheria hiyo.

Mwandishi Maria Sarungi Tsehai , ambaye biashara yake ya vyombo vya habari ilifungwa na serikali , aliambia BBC kwamba Twitter ndio mtandao wa pekee ambao Watanzania walio na ushawishi mkubwa walitumia kutoa maoni yao.
'Ni eneo la maoni ambayo hayajachujwa'', alisema.
Hivyobasi hakuweza kunyamaza baada ya Kigogo na akaunti nyengine tano maarufu kufungwa kufuatia malalamishi ya hatimiliki siku kadhaa kabla ya uchaguzi.
Muda mfupi baada ya bi Tsehai kuandika barua ya wazi , kwa mwanzilishi wa Twitter na afisa mkuu mtendaji Jack Dorsey akimtaka kusitisha ukandamizaji na kunyamazishwa kupitia mfumo wa kusimamia ukiukaji wa hatimiliki, akaunti hizo badala yake zilifunguliwa na nyengine kuthibitishwa kwa kutumia usaidizi wa shirika la kupigania haki za mtandaoni Acces Now.
'Kusitisha madai bandia'
Ijapokuwa Kigogo anahisi hakikisho kuhusu kulindwa kwa akaunti yake na kwamba Twitter sasa ina ufahamu kuhusu utumizi mbaya wa hatimiliki, anasema kwamba kampuni hiyo inapaswa kuchukua hatua kali zaidi.
Mambo yalibadilika baada ya Maria kumuandikia Jack Dorsey, lakini nadhani wanapaswa kuimarisha mfumo wao wa kuchunguza malalamishi ya hatimiliki. Kwa mfano iwapo ni kampuni basi nakala zote ambazo zinahalalisha kampuni hiyo zinahitaji kuchunguzwa na kuthibitishwa, hiyo ndio njia pekee wanaweza kusitisha malalamishi bandia .
Shirika la Acces Now linaamini kwamba utumizi wa sheria ya hatimiliki nchini Tanzania unaweza kuigwa na mataifa mengine barani Afrika.
Hatua ya serikali kutumia mianya ya sheria ya hatimiliki Tanzania inatia wasiwasi na kuwa tisho kubwa kwa uhuru wa kujieleza barani Afrika, Berhan Taye kutoka shirika la Acces Kenya aliambia BBC.
Aliongezea: Mitandao ya kijamii inayoathirika kutokana na mianya ya sheria ya hatimiliki haina chaguo bali kuangazia suala hilo , na kusaidia kuhakikisha kuwa serikali haziwezi kutumia mbinu hiyo dhidi ya wakosoaji.
Kigogo anaendelea kuwafurahisha wafuasi wake na habari tamu lakini pia anafurahia kile ambacho akaunti yake ya siri imesababisha na kutumai kwamba itaendelea kuwa dondoo kuhusu mmiliki wake. BBC imeomba maoni ya Msemaji wa Serikali ya Tanzania juu ya madai yaliyomo kwenye habari hii, lakini mpaka sasa haijapata tamko lolote.












