Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Je uchaguzi huu usioisha utaisha lini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni siku kadhaa tangu kinyang'anyiro cha kuingia Ikulu ya White House kushindwa na Joe Biden wa Democratic, lakini Donald Trump bado hajaridhia matokeo ya uchaguzi huo - au kuonesha dalili ya kukubali kushindwa.
Badala yake, amekuwa akitoa madai ambayo hayajathibitshwa kuhusu wizi wa kura, ambao anasema ulimpendelea Bwana Biden.
Lakini hesabu ya kura ilivyo - yuko nyuma kwa maelfu ya kura katika majimbo kadhaa ambayo yangemsaidia kushinda. Baadhi ya watu wanaona kama ni harakati ambazo hazitafua dafu.
Msimamo wa Trump, kupinga maadili ya kisiasa umezua hofu kote nchini, huku maafisa wa umma na wapiga kura wa Marekani wakiendelea kujadili hatua hiyo.
Haya hapa baadhi ya maoni ya jinsi makundi muhimu yanavyoshughulikia siku hizi za kutokuwa na uhakiki ni nini kitakachotokea.
Viongozi wa Republican
Je Donald Trump amekubali kushindwa?
Hapana.
"Rais ana kila haki kufuatilia madai ya udanganyifu na kuomba kura zihesabiwe tena kwa mujibu wa sheria." - Kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Mitch McConnell
Ukweli wa mambo
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, wanasiasa wa Republican - kuanzia kwa wale wanaoshikilia nyadhifa za juu bungeni na ndani ya chama wanakabiliwa na wakati mgumu kujibu masuali yaliyoibuka kutokana na hatua ya Trump iliyozua utata.
Wanachukua muda wakisubiri kuona jinsi dhoruba hilo litakavyopita.
Mpango wao ni rahisi. Warepublican wachache hawataki kumkosea mtu ambaye anaweza kuwashambulia kupitia mtandao wa Twitter.
Kwa hivyo licha ya rais kushindwa katika uchaguzi, Warepublican wameamua kusimama kando na kumuacha rais aendelea kusisitiza kwamba alishinda kupitia "kura halali", hadi pale mchakato wa kisheria wa kupinga matokeo ya uchchaguzi utakapokamilishwa na kuidhinishwa.
Wanasiasa wa Republican lazima watathmini maisha yao ya baadae, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi na utawala wa Demokratic unaoingia madarakani na kuwaridhisha watu walio na misimamu ya kadri kwa ajili ya chaguzi zijazo. Tofauti na rais, hawana mpango wa kujiingiza moja kwa moja katika mzozo wa kisiasa. Ratiba yao ya kisiasa inapimwa kwa miaka na wala sio siku au wiki kadhaa.
Kwa kuzingatia hilo janga la mchezo ni kuwa na subira. Wakubali kuwa rais ana haki ya kutoa madai hayo, wampe nafasi ya kutoa ghadhabu zake, lakini wajue kwamba hakutakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo kiasi cha kubadilisha matokeo ya uchaguzi.
Kupitia mate yao, kama sio matamshi, wanakubaliana kuwa kufikia Januari, kutakuwa na rais mpya na kwamba Bw. Trump pia, ataondoka tu.
Mwanasheria Mkuu Bill Barr
Je Donald Trump akubali kushindwa?
Haiko wazi.
"Wakati madai yaliyo na uzito yanastahili kushughulikiwa kwa uangalifu mkubwa, uvumi na madai yasiyokuwa na ushahidi haustahili kuwa msingi wa kuanzisha uchunguzi." - alisema Barr katika barua aliyoandikia kitengo cha haki
Ukweli wa mambo
Siku ya Jumatatu, katika hatua ambayo ilionekana kwenda kinyume na hali ya kawaida ya muda mrefu, Mwanasheria Mkuu Bill Barr alitoa waraka kwa maafisa wake wa ngazi ya juu kuidhinisha kuanzishwa mara moja kwa uchunguzi wa madai ya udanganyifu katika uchaguzi badala ya idara ya haki kufanya hivyo kabla ya matokeo ya uchaguzi kuidhinishwa na majimbo.
Hatua hiyo inampatia Donald Trump uthibitisho kwamba serikali inachunguza madai ambayo hayathibitishwa ya ukiukwaji mkubwa wa maadili ya uchaguzi katika majimbo mengi aliyopoteza kwa maelfu ya kura.
Mwanasheria Mkuu haha hivyo ameandika waraka huo kwa uangalifu mkubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Licha ya uangalifu wa maneno yaliyotumiwa waraka huo wa Barr, utatoa nafasi kwa Trump na wafuasi wake, ambao wanasisitiza kura ziliibwa kuendelea na madai hayo ya udanganyifu (bila kujali wagombea wengine wa Republican walishinda kupitia mchakato huo wanaoukosoa).
Kuna ulinzi wa kisheria uliopo kuhakikisha uchunguzi wa jinai hauingiliwi kisiasa, hasa katika masuala yanayozunguka uchaguzi .
Barr sasa ameondoa ulinzi huo. Swali sasa ni je hatua hiyo inatosha kumasaidia rais ambaye anatafuta ushahidi wa kuthibitisha madai yake ya udanganyifu au wizi wa kura?
Wandani wa karibu wa Trump
Je Trump akubali kushindwa?
Hapana! (Pengine?)
"Nimetoka kuzungumza na Rais Trump na nimemwambia kwamba namuunga mkono kwa kusimama imara kupigania utawala wa sheria, katiba na mfumo wetu wa Marekani." - Mshauri wa kisheria wa Trump, Jenna Ellis, kupitia Twitter
Ukweli wa mambo
Hadharani, washauri wa karibu wa rais na wandani wake wa karibu - hasa wale ambao wamekuwa naye kwa muda mrefu, kama Rudy Giuliani - wamesimama naye anapoendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Moja ya sababu ni kwamba. Endapo Rais ataondoka madarakani watapoteza kazi zao (au pengine, kuwa karibu na mtawala wa nchi).
Kwa wengine kama, msemaji wa rais Kayleigh McEnany, hii ni ishara kwamba wanasisitiza upande wao utashinda ("Huu uchaguzi haujamalizika. Tuko Mbali sana na hilo.").
Wengine kama, Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo, ni hatua ya kejeli ("Itakuwa ni kutoa nafasi ya muhula wa pili kwa utawala wa Trump.").

Sababu zingine ni za kibinafisi. Wana wawili wa kiume wa Trump, Don Jr na Eric, wamesimama na baba yao kikamilifu na kupaza sauti kuhusu madai ya udanganyifu katika uchaguzi. Ni jina la familia yao na liko matatani .
Nyuma ya pazia, hata hivyo baadhi yao wanashuku - au hata kutokuwa na hakika- kuhusu hali ilivyo. Binti wa rais Ivanka Trump amesalia kimya tangu uchaguzi, na kumekuwa na ripoti kwamba yeye na mume wake Jared Kushner, wanaamini wakati umewadia kwa rais kukubali kushindwa.
Huku hayo yakijiri wafanyakazi zaidi wa utawala wa Trump ambao huenda wakapoteza kazi katika kipindi cha miezi kadhaa - wameachwa katika njia panda, kuna ripoti zinazoashiria kwamba wameambiwa na mkuu wa watumishi wa rais John McEntee, watafutwa kazi wakijulikana kwamba wanatafuta kazi kwingine.
Wafuasi wa Trump
Je Trump akubali kushindwa?
Kwa kisa gani!
"Nimekuja hapa kuonesha upendo wangu na kumuunga mkono rais wetu, Donald Trump. Huu ni utapeli mkubwa. Eti kuna kura nyingi ambazo bado hazijahesabiwa, zote ni feki, ni za watu waliokufa." - Mfuasi wa Trump mjini Houston, Texas, aliambia BBC
Ukweli wa mambo
Kufikia wiki ya mwisho kuelekea uchaguzi, wafuasi wengi wa Trump waliamini licha ya kura ya maoni kuonesha vingine, mgombea wao atashinda.
Ikizingatiwa matokeo ya kushangaza ya uchaguzi wa mwaka 2016, ambapo kura za maoni zilibashiri ushindi wa Hillary Clinton hadi aliposhindwa, wafuasi wa Trump waliendelea kuamini hali kama hiyo huenda ikajitokeza tena kwasababu matokeo ya uchaguzi yalienda kinyume na kura za maoni.
Pia ushindani katika uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa wa karibu sana kiasi kwamba ilikuwa vigumu kubashiri ni nani atakayeshinda kama ilivyobashiriwa.

Japo kura zimehesabiwa na Biden kutangazwa mshindi, kuna baadhi ya wahafidhina ambao bado wamesimama na rais. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Reuters na Ipsos wikendi iliyopita karibu asilimia 40 ya Warepublican hawaamini Biden alishinda uchaguzi wa urais.
Kampeni ya Trump inapanga mkutano wa "Kupinga Wizi"kote nchini ikiwemo moja katika mji wa Washington, DC Jumamosi hii. Pia kumekuwa naripoti kwamba rais anapanga kufanya mkutano kama wa kisiasa siku zijazo, japo hakuna mipango rasmi iliyotangazwa.
Joe Biden
Je Donald Trump akubali kushindwa?
Ndio.
"Nadhani Ni aibu, kusema kweli, Kile ninachoweza kusema kwa heshima, Nadhani hatua hiyo haitasaidia kudumisha hadhi ya rais atakapoondoka madarakani."
"Mwisho wa siku, mbivu na mbichi itajulikana Januari 20," alisema akiashiria siku ya kuapishwa.
Ukweli wa mambo
Tangu alipotangazwa mshindi wa uchaguzi wa Marekani 2020 siku ya Jumamosi Joe Biden na timu yake wamefanya kitu kinachoonekana kuwa maandalizi ya mchakato wa kupokezana madaraka na mtangulizi wake Donald Trump
Amefanya mkutano na jopo kazi lake la corona siku ya Jumatatu na kujibu maswali kutoka kwa wanahabari Jumanne, ambapo aliahidi kutangaza uteuzi wa maafisa wa nagzi ya juu wa utawala wake katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo.
Biden amepuuzilia mbali hofu kwamba hatua ya rais kukataa kukubali kushindwa imeathiri vibaya kazi yake, akisema kucheleweshwa kwa upatikanaji wa fedha na habari za serikali ambazo kwa kawaida hutolewa kwa wawakilishi wa rais mteule sio kikwazo kikubwa.
Alisema Warepublican, watakuja kukubali ushindi wake, hata kama wengine "wanatishiwa kwa upole na rais aliyeko madarakani".
Wanasiasa wa Democratic wanaamini hata kura zikirudiwa kuhesabiwa watashinda, japo mawakili wao wanapinga vikali hatua hiyo mahakamani.
Donald Trump
JeDonald Trump akubali kushindwa ?
Soma ujumbe ufuatao wa Twitter kupata jibu.
"Watu hawatakubali matokeo ya uchaguzi uliyochakachuliwa!"
Ukweli wa mambo
Ni Donald Trump pekee anajua kwa nini hajakubali kushindwa na Biden, licha ya kuwaachwa nyuma kwa maelfu ya kura katika majimbo tofauti.

Chanzo cha picha, Getty Images












