Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Je, huu ni mwisho wa upinzani Tanzania?

Wanachama wa chama cha mapinduzi wakishangilia
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Baada ya kuanguka kwa Dola ya Urusi na kubomolewa kwa Ukuta wa Berlin, mwanasayansi ya siasa mashuhuri duniani, Yoshihiro Francis Fukuyama, aliandika kitabu kilichoitwa 'The End of History'.

Hoja yake kubwa ilikuwa kwamba baada ya kuanguka kwa Ukomunisti, dunia sasa itabaki na mifumo miwili tu ya kudumu; Soko Huria na Demokrasia.

Hakutakuwa na mfumo mwingine.

Fukuyama alikuwa sahihi wakati huo lakini leo, takribani miongo mitatu baada ya kitabu chake kile, dunia imejikuta ikiongozwa na aina ya viongozi; Donald Trump, Narendra Modi, Vladmir Putin na Recep Erdogan ambao wana dhana tofauti ya demokrasia na soko huria. Hawa wana misimamo ya kihafidhina yenye mrengo wa utaifa.

Ni eneo ambalo Fukuyama hakuwa amelitambua.

Baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka huu ambayo yanaendelea kutolewa, ni rahisi kuandika taazia ya mfumo wa vyama vingi nchini. Pengine Fukuyama -kama angekuwa Dar es Salaam au Mwanza, angeweza kuandika kitabu na kukiita 'The End of Multipartism in Tanzania', lakini, kwa mara nyingine, asingekuwa sahihi sana.

Hii ni kwa sababu, jambo pekee lisilobadilika kuhusu maisha ya wanadamu na mataifa duniani kote ni moja; mabadiliko. Jambo la kudumu kuliko yote ni mabadiliko.

Mdee

Chanzo cha picha, The Citizen

Katika wakati huu, siasa za Tanzania zinapitia mabadiliko na changamoto za wakati huu lakini jambo hili pia halitakuwa la kudumu kwa sababu - kwa asili, mwanadamu ni mtu anayeishi kwa kutaka mabadiliko.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama vya upinzani vilipata takribani asilimia 40 ya kura zote zilizopigwa. Katika uchaguzi huu, kwa namna matokeo yanavyoelekea kutoka, itakuwa vigumu kwa vyama hivyo kupata walau asilimia 20 ya kura zote.

Watu wale asilimia 40 waliovipigia kura miaka mitano iliyopita hawajafa wote au kupotelea angani.

Maswali pekee ambayo vyama vya upinzani na wachambuzi wa siasa wanatakiwa kulitafutia jibu kwenye tafakuri ya uchaguzi ni kwamba kwanini mamilioni haya ya watu hawakupiga kura kwenye uchaguzi huu na kama walipiga, ni kwa nini sauti yao haikusikika kwenye matokeo yanayoendelea kutangazwa.

Maneno ya Alexis du Tocquiville

Katika uchambuzi wake kuhusu mapinduzi ya Ufaransa yaliyotokea zaidi ya miaka 200 iliyopita, mwanazuoni maarufu, Alexis du Tocquiville, aliandika kwamba wakati mbaya zaidi utawala mkongwe uko katika nyakati mbili.

Mosi ni wakati ambapo utawala husika unajiona uko salama zaidi kuliko wakati mwingine wowote na pili ni pale utawala uliokuwa ukijulikana kwa mabavu yake unapoanza kufanya mambo ya kuonesha kwamba unabadilika na kuwa wa kiungwana.

Joseph Mbilinyi ni mbunge aliyepoteza kiti chake jimbo la Mbey mjini

Chanzo cha picha, JOSEPH MBILINYI

Uchambuzi huo ni wa kweli hadi leo. Mengistu Haile Mariam wa Ethiopia aliondolewa na akina Meles Zenawi, wakati akianza kufanya marekebisho ya sheria kali za utawala wake wa kidikteta.

Wakati hayati Kingunge Ngombale Mwiru aliporejea nchini kutoka Romania siku chache kabla ya kupinduliwa kwa Rais Nicolae Ceaucescu, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba "Ceaucescu hajawahi kuwa imara katika utawala wake kama wakati huo".

Nikiwa Japan, mapema mwaka huu, nilipomsimulia rafiki yangu mwandishi wa habari raia wa Romania, Valentin Mihu, aliniambia alichosema Kingunge kilifanana na kilichosemwa na viongozi wengine waliotembelea taifa hilo katika siku za mwisho za Ceausescu mwishoni mwa miaka ya 1980.

Hakuna aliyeona kwamba anguko la Ceaucescu lilikuwa karibu. Katika wakati ambao kila mmoja alimuona akibaki madarakani kwa miaka mingi, ndiyo wakati ambao aliondolewa madarakani.

Ndivyo alivyowahi kuandika Tocquiville; mwanazuoni aliyefanya kazi kubwa zaidi kwenye kuelezea mapinduzi hayo ya Ufaransa kupitia andiko lake la Ancien Regime.

Rais Magufuli akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia. Mbatia amebwagwa katika jimbo la Vunjo

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaelekea kupata ushindi mkubwa kuliko mwingine wowote dhidi ya upinzani katika uchaguzi mkuu tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mnamo mwaka 1992.

Kwenye vitabu vya historia, ushindi huo utakuwa ukisemwa na kunukuliwa na wana CCM wote; kuanzia ngazi ya chini hadi juu kabisa wana haki ya kuona kwamba sasa chama chao kiko salama na imara kuliko wakati mwingine wowote.

Tatizo ni moja tu; kwamba Tocquiville na wanazuoni wengine walioandika kuhusu uimara na udhaifu wa tawala za dunia katika kipindi cha miaka 200 hadi 300 wanatuambia vinginevyo.

Kwanini Upinzani utafufuka?

Sababu ya kwanza, na kubwa kuliko yote, ni kwamba mabadiliko ni jambo la lazima. Kuna wakati utafika ambapo Watanzania watatawaliwa na chama kingine au namna nyingine yoyote ya mfumo wa utawala.

Tanzania ni taifa lenye watu wengi wenye umri mdogo. Takribani nusu ya Watanzania, walau watu milioni 25, hawakupiga kura mwaka huu kwa sababu wana umri chini ya miaka 18; na hivyo ni wadogo kushiriki kupiga kura.

Hili ni kundi kubwa la watu ambao kama watashawishiwa kushiriki katika kupiga kura, wanaweza kuwa chemchem kubwa ya mabadiliko huko miaka ya mbele.

Tafiti mbalimbali zilizowahi kufanyika duniani zinaonesha kwamba tofauti moja kati ya vijana na watu wazima (wazee) ni kwamba kundi moja hupenda mabadiliko na lingine huombea kubaki na kilichozoeleka.

Kama wapinzani wataweza kubuni sera na mipango ambayo itafanya kundi hili kubwa la wapiga kura kuvutiwa nao, bado kutakuwa na uwezekano wa kuibuka na kufanya vizuri kwenye miaka ijayo.

Zitto Kabwe ameangushwa katika nafasi aliyokuwa akiitetea ya ubunge aliyokuwa akiwakilisha Kigoma mjini

Upinzani pia unaweza kuibuka kupitia CCM yenyewe. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kubashiri miaka mingi huko nyuma kwamba upinzani mkubwa ndani ya chama hicho kikongwe utatoka ndani ya chama hicho.

Baada ya matokeo ya uchaguzi huu, dhana hii inaweza kuwa na nguvu zaidi kuliko katika wakati mwingine wowote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Kuna mitihani miwili inaikabili CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo; uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliopangwa kufanyika mwaka 2022 na kinyang'anyiro cha kumpata mgombea atakayebeba kijiti cha chama hicho kwenye uchaguzi wa Rais miaka mitano ijayo.

Endapo wana CCM hawataridhika na atakayepitishwa kuwania Urais, jambo hilo linaweza kuibua mpasuko na hivyo kutimiza ubashiri wa Mwalimu Nyerere. Ni jambo la kusubiri kuona ni kwa namna chama hicho kitaivuka mitihani hii miwili ya karibuni.

Bunge la chama kimoja litakuwaje?

Katika Bunge lililopita, kulikuwa na wabunge 393; huku wabunge wa chama tawala wakiwa 274 na wengine 119 wakitoka katika vyama vya upinzani.

Kundi hilo la wabunge wa upinzani lilitengeneza Kambi ya Upinzani bungeni iliyokuwa ikiandaa hoja nzito dhidi ya serikali. Katika miaka 15 iliyopita, wabunge kama Zitto Kabwe, Freeman Mbowe, Halima Mdee, Peter Msigwa, walijitambulisha kwa uwezo wao wa kujenga hoja.

Wakati kura zikiendelea kuhesabiwa, kuna uwezekano vyama vya upinzani vikapata idadi ya wabunge ambayo haitaweza hata tu kujaza nafasi za mawaziri kivuli watakaokuwepo kwenye serikali ijayo.

Tanzania ina uzoefu wa kuwa na Bunge la chama kimoja. Tangu mwaka 1965, na hasa kuanzia mwaka 1977 wakati CCM ilipoanzishwa hadi mwaka 1995, Tanzania ilikuwa nchi ya Bunge la chama kimoja -CCM.

Upinzani kufurukuta?

Chanzo cha picha, BUNGE TANZANIA

Hata hivyo, kulikuwa na mijadala mikali, ukiwamo ule wa kujali Serikali ya Tanganyika uliotokea kwenye miaka ya 1990. Kwa hiyo, kuna nyakati Bunge la chama kimoja lilikuwa na hoja nzito.

Tofauti ya mabunge hayo ya nyuma na linalotarajiwa kuwa Bunge la sasa ni historia ya watakaounda kundi hilo. Wabunge wa CCM wa zamani walikuwa ni watu waliojengwa katika utamaduni wa mijadala mizito kwenye chama na ambao tayari walishatengeneza majina yao kwenye maeneo mengine kabla ya kuingia kwenye siasa.

Wengi wa wabunge wa kisasa, karibu vyama vingi, ni wapya na wengine wanakuwa hawajapata hata muda wa kujenga majina yao katika taasisi nyingine kabla ya kuingia bungeni. Kwa uzoefu, wengi wanakuwa watiifu kwa chama na viongozi wao.

Katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar baada ya uchaguzi wa mwaka 2016, mijadala ilipoa tofauti na ilivyokuwa wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Uzoefu katika nchi nyingine kama Rwanda na Ethiopia, uzoefu unaonesha kwamba Bunge linapokuwa limeshikiliwa kwa kiasi kikubwa na chama kimoja, ubora wa mijadala hushuka.

Mchungaji Peter Msigwa aliangushwa katika jimbo la Iringa mjini

Chanzo cha picha, CHADEMA

Jambo pekee ambalo upinzani na wanaharakati wanatakiwa kulitazama kwa karibu katika Bunge lijalo ni namna ambavyo wabunge wa CCM wanavyoweza kutumia wingi wao kubadili sheria na taratibu zitakazokihakikishia chama chao kubaki madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Hata hivyo, Watanzania wanaweza kushangazwa pia na kiwango cha mijadala itakayokuwa ikitoka bungeni. Na hii ni kwa sababu, kwa kiwango kikubwa, mmoja wao atakayemrithi Rais John Magufuli, katika uchaguzi ujao, atakuwa ndani ya Bunge hili.

Ni lazima mtu huyu, na wenzake wenye matamanio kama yake, atajaribu kujitutumua na kuwaonesha Watanzania nini kipo ndani yake.

Hili ni suala la kusubiri na kuona.