Hussein Mwinyi: Mfahamu zaidi rais mteule wa Zanzibar

Dkt Hussein Mwinyi ni rais mteule wa Zanzibar

Chanzo cha picha, Getty Images

Tume ya uchaguzi Zanzibar imemtangaza Dkt Hussein Mwinyi kuwa mshindi wa urais Zanzibar.

Mgombea wa chama tawala cha CCM Hussein Mwinyi atangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Urais Zanzibar kwa asilimia 76. 27% huku mpinzani wake Maalim Seif akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87%.

Baada ya kutangazwa mshindi Dkt.Mwinyi amesema "Nimepokea ushindi kwa mikono miwili, Nashukuru kuwa wananchi walio wengi wamenichagua mimi na chama changu cha Mapinduzi kwa miaka 5 ijayo.

''Ninawashukuru kwa uvumilivu na ustahamilivu mkubwa. Niwashukuru zaidi kwa kunipigia kura za kutosheleza kuwa rasi wa Zanzibar. Nitalipa Imani hii kwa utumishi uliotukuka," Dkt Mwinyi amesema.

Je Mwinyi ni nani?

Japo ni mpya katika mbio za urais, Mwinyi ni kiongozi mwandamizi katika siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Safari yake kisiasa ilianzia mwaka 2000, alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Mkuranga kwa upande wa Tanzania bara, na kisha mwaka 2005 kuhamia upande wa Zanzibar katika jimbo la Kwahani ambalo ameliongoza kwa miaka 15.

Katika kipindi chake cha miaka 20 ya ubunge amefanya kazi na marais watatu wa Tanzania, hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na rais wa sasa John Magufuli.

Dkt Hussein Mwinyi alianza safari yake ya kisiasa mwaka 2000

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwaka 2000 alichaguliwa kuwa naibu waziri wa afya na hayati Mkapa, katika miaka 10 ya Kikwete alipanda na kuwa waziri kamili na kuhudumu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Afya na Ulinzi.

Miaka mitano iliyopita amehudumu kama Waziri wa Ulinzi kwenye serikali ya Magufuli.

Ushawishi wa Mwinyi uliojengeka katika utumishi wake katika miongo miwili iloyopita ulijidhihirisha katika namna ambavyo alinyakua tiketi ya kuwania urais ya CCM.

Safari hiyo ilianza kwa zaidi ya wananchama 30 kuchukua fomu za kuwania, kisha majina matano yakapelekwa mbele ya vikao vya juu vya chama hicho kwa maamuzi. Katika kura za mwisho za uteuzi ndani ya chama, Mwinyi akipata kura 129 sawa na asilimia 78 ya kura zote, mshindani aliyemkaribia zaidi alikuwa na kura 19.

Pamoja na uzoefu wake na ushawishi wake binafsi wa kisiasa, Mwinyi anatokea katika moja ya familia maarufu na kubwa kisisasa nchini Tanzania. Baba yake Mzee Ali Hassan Mwinyi ni rais mstaafu wa serikali za Tanzania na Zanzibar.

Kitaaluma, Mwinyi ni tabibu na amepata elimu yake nchini Tanzania, Misri, Uturuki na Uingereza.

Hussein Mwinyi alikabiliana mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Maalim Seif mgombea wa chama cha ACT-Wazalendo

Chanzo cha picha, Getty Images

Safari yake ya kuwania urais

Ushindi wake ndani ya chama ulikuwa wa kishindo, lakini hata wakati wakipongezana kwa kumpata mgombea ambaye chama kilimnadi kuwa ni sahihi, fikra za viongozi wa juu na wanachama wa kawaida zilishahamia katika ushindani dhidi yake.

Rais Magufuli akimnadi Mwinyi baada ya kupitishwa na CCM kuwa mgombea wao wa urais, alituma salamu ama dongo la kisiasa kwa mshindani wao mkuu Zanzibar, Maalim Seif, kwa kuwataka Wazanzibari "...msinichagulie shikamoo."

Suala la umri, limekuwa moja ya hoja za kampeni kwa upande wa CCM, kuwa Mwinyi mwenye miaka 53 ni 'kijana' mwenye nguvu bado ya kuifanya kazi ya urais, huku Maalim Seif mwenye miaka 76 wakidai amechoka na anastahili kupumzika.

Hata hivyo kwa Maalim Seif na wafuasi wake wa chama cha ACT-Wazalendo, umri si kigezo. Maalim amemjibu Magufuli kuwa "...shikamoo utaitoa utake usitake" huku wafuasi wake wakitumia salamu hiyo kama kionjo chao: "Shikamoo Maalim."

'Yajayo ni neema tupu'

Maelezo ya sauti, CCM yamchagua Dr Hussein Ali Mwinyi, kuwa mgombea wa urais visiwani Zanzibar

Katika kujinadi kwa sera na azma ya kuleta mabadiliko visiwani Zanzibar, Mwinyi anatumia kauli mbiu: "Yajayo ni neema tupu."

Baadhi ya vipaumbele vyake ni kupambana na rushwa na ubadhilifu wa mali ya Umma ambapo ameahidi kushughulikia tatizo hilo kwa mtindo wa Rais Magufuli. Kuboresha mazingira ya sekta ya utalii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar pamoja na kuwanyanyua wajasiriamali na wanawake visiwani humo.

Chaguzi zote za Zanzibar kasoro mwaka 2010, zimeshuhudia malalamiko ya wizi wa kura na udanganyifu, uvunjifu wa haki za binadamu na ghasia.

Mwaka 2010 hali ilikuwa tulivu kutokana na kura ya mabadiliko ya katiba ya kuwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baada ya uchaguzi wa 2010, Maalim Seif alichukua nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na chama chake enzi hizo cha CUF kuunda sehemu ya mawaziri wa baraza la mapinduzi.

Mwaka 2015 matokeo ya uchaguzi yalifutwa, na uchaguzi kurudiwa 2016 japo chama kikuu cha upinzani CUF kilisusia kushiriki.

Kutokana na historia ya uchaguzi Zanzibar, ni wazi kuwa Mwinyi alikabiliwa na upinzani mkali wa kupambana nao kutoka kwa Maalim Seif katika uchaguzi wa sita toka mfumo wa vyama vingi kurejea Tanzania.