Mocimboa da Praia: Msumbiji yapigania kukomboa bandari iliyotekwa na IS

Resident fleeing violence by boat in northern Mozambique

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Maelfu ya watu Msumbiji wamelazimisha kutoroka makazi yao kwasababu ya mapigano

Msumbiji imesema kuwa vikosi vyake vinapigana kuchukua udhibiti wa bandari muhimu ya Mocimboa da Praia, baada ya taarifa kadhaa kudai kwamba imetekwa na wanamgambo wa Islamic State Jumatano.

Mji huo uko karibu na miradi ya gesi asili yenye thamani ya dola bilioni 60.

Jeshi limesema kuwa hatua imechukuliwa kukabiliana na kundi hilo ambalo limekuwa likitumia wenyeji kama ngao yao.

Hatua hiyo inafuatia mapigano ya siku kadhaa ya kutaka kuchukua bandari hiyo yenye utajiri wa gesi eneo la kaskazini.

Mwandishi wa BBC Africa Andrew Harding amesema kuwa kutekwa kwa bandari hiyo ni pigo kubwa kwa jeshi la Msumbiji, ambalo lina wakati mgumu kudhibiti ukuaji wa makundi ya waasi katika eneo hilo la utajiri wa mafuta la Cabo Delgado.

Bandari ya Mocimboa da Praia inatumiwa kwa uwasilishaji wa mizigo kwa miradi ya eneo la pwani takribani umbali wa kilomita 60 (maili 40), ambayo inaendelezwa na kampuni kubwa za mafuta duniani ikiwemo Total.

Map

Wanamgambo - wenye kuhusishwa na kundi la Islamic State -wamekuwa wakitwaa miji kadhaa ya kaskazini katika miezi ya hivi karibuni, na kulazimisha maelfu ya watu kutoroka makazi yao. Hili lilikuwa moja ya mashambulizi kadhaa katika bandari ya Mocimboa da Praia mwaka huu.

Tanzania pia imesema itafanya mashambulio dhidi ya wanamgambo wa jihadi katika misitu karibu na mpaka na Msumbiji.

2px presentational grey line

Udhaifu uliojitokeza

Uchambuzi wa Andrew Harding, Mwanahabari wa BBC Africa

Vikosi vya ulinzi vya Msumbiji vimeendelea kusisitiza kwamba mapigano ya kutaka kukomboa bandari ya Mocimboa da Praia bado yanaendelea.

Lakini matukio ya wiki zilizopita yameonesha udhaifu uliopo ndani ya jeshi na jinsi waasi wa kiislamu wanavyoendelea kujiimarisha ambako sasa kunajitokeza na kuonyesha vile kunavyoweza kuwa tishio kubwa la eneo hilo.

Taarifa mbalimbali zinaashiria kwamba vikosi vya serikali vilikuwa vimelazimika kusalimu amri baada ya kuishiwa na silaha.

Wanajeshi kadhaa inasemekana kwamba wameuawa na boti lililokuwa linashika doria likazamishwa.

Miezi ya karibuni, waasi wameteka miji kadhaa ya eneo, kiasi fulani inaonekana kuwa propaganda.

Baadhi ya kampuni kubwa duniani za nishati sasa zinataka ulinzi zaidi wakati zinajitayarisha kuanza kuzalisha mafuta katika visima vilivyo pwani ya Msumbiji.

Aidha, serikali imetafuta usaidizi kutoka kwa wanakandarasi wa usalama wa kimataifa. Lakini hadi kufikia sasa, inaonekana haiko tayari kugeukia nchi jirani kutafuta usaidizi wa kijeshi.

2px presentational grey line

Mashambulio eneo la kaskazini mwa Cabo Delgado, yalianza 2017, lakini yakaongezeka mwaka huu baada ya kundi la Ahlu Sunnah Wa-Jama, Kukiri kuhusika na mashambulizi, kudai kuwa na ushirikiano na lile la IS.

Mapema wiki hii kundi la IS lilidai kwamba limetwaa kambi mbili za jeshi karibu na bandari ya Mocimboa da Praia, ambapo wanajeshi kadhaa wa Msumbiji waliuawa na silaha zao kuchukuliwa ikiwemo, bunduki za rashasha na guruneti zilizorushwa kwa makombora.