Uchaguzi Tanzania 2020: Bernard Membe na mawindo ya urais kupitia upinzani

- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Ndani kabisa ya moyo wake, Bernard Membe - Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania ni mwindaji.
Marehemu baba yake alikuwa mwindaji na alipoteza maisha yake akiwa mawindoni. Kwa watu wengine, hilo lingeweza kumuweka mbali na pengine kuchukia shughuli hiyo.
Lakini Membe anajivunia urithi huo wa familia yake. Katika wakati wake wa mapumziko, huwa anapenda kuwinda wanyama akiwa kijijini kwake Rondo.
Na baada ya wiki hii kutangaza kujiunga na Chama cha ACT Wazalendo, ni wazi kwamba sasa anawinda kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Endapo hatimaye atapitishwa na chama chake -au muungano wa upinzani kuwa mgombea wake wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ataleta changamoto tofauti kabisa na ilivyokuwa kwa wagombea wengine wa upinzani tangu mwaka 1995.
Kutoka Mwanadiplomasia hadi Mtetea Haki
Miaka kumi tu iliyopita, jina la Membe halikuwahi kutajwa kama mmoja wa watetea haki mashuhuri hapa nchini. Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete aliyekuwa na majukumu mengi nje ya nchi.
Alionekana tu kama mwanadiplomasia aliyekuwa akitekeleza majukumu ya serikali ambayo msingi wake ulikuwa ni kufanya diplomasia ya uchumi.
Membe hakuwa mmoja wa wanasiasa pendwa ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na nguvu yake pekee kisiasa ilielezwa kuwa ukaribu wake na Kikwete.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kulikuwa na fununu kwamba yeye ndiye aliyekuwa kipenzi cha Kikwete na si Edward Lowassa aliyekuwa akitajwa kama kipenzi cha wengi ndani ya CCM.
Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, Membe hakufanikiwa kupitishwa na CCM kuwa mgombea wake -nafasi hiyo ikienda kwa John Magufuli; Rais wa sasa wa Tanzania.
Tofauti na Lowassa, Membe hakuhama CCM baada ya kukosa nafasi hiyo. Hata hivyo, kwenye utawala wa Rais Magufuli, Membe amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa uendeshaji wa serikali na dola kwa ujumla jambo hilo limempa umaarufu na kumpaisha kisiasa kuliko wakati mwingine wowote kwenye maisha yake.
'Jini' lililotengenezwa na utawala wa Magufuli

Chanzo cha picha, Membe/Twitter
Mfumo wa aina yoyote - uwe wa gari, mwili au wa utawala, huhitaji kuwa na mahali pa kupumulia. Kwenye mfumo wa kawaida wa demokrasia, watu hueleza, na hivyo kupumua, kupitia vyombo vya habari, asasi za kiraia, vyama vya siasa na taasisi nyingine.
Tangu kuingia madarakani kwa utawala wa Rais Magufuli, kumekuwapo na kupungua kwa uhuru wa kujieleza kupitia njia zilizokuwa zimezoeleka kwa takribani miaka kumi hadi 20 iliyopita.
Tanzania haijawahi kuwa nchi uhuru kamili kwa vyombo vya habari , kwani huko nyuma yalikuwepo pia magazeti na asasi za kiraia zilizofungiwa kwa kutoifurahisha serikali katika kutimiza majukumu yake.
Tofauti iliyopo sasa kulinganisha na miaka kumi iliyopita iko kwenye wastani na wingi wa matukio yanayoonesha kubanwa kwa asasi hizo.
Matokeo yake ni kuibuka kwa watu binafsi; wanaojulikana na wasiojulikana, ambao wamekuwa wakitoa maoni yao bila kuhofia kinachoweza kuwapata.
Umaarufu wa Membe, kuliko sababu nyingine yeyote, umesababishwa na ukweli kwamba yeye ndiye mwanasiasa maarufu na mkubwa aliyekuwa na uthubutu wa kukemea hadharani kuhusu mambo ambayo yangeweza kukemewa na asasi zilizokuwa zikifanya hivyo lakini sasa hazitimizi majukumu yake.
Kwa hiyo, umaarufu wa Membe wa sasa ni zao na vitendo vya serikali ya CCM katika miaka ya karibuni. Yeye amekuwa sehemu ya 'kupumua' na Sauti ya Wasiosikika katika nyakati.
Kwa maneno mengine, Membe ni kama jini lililotengenezwa na serikali ya Rais John Magufuli .
Membe anapeleka nini kwenye upinzani?
Tofauti na Augustine Mrema wa mwaka 1995 au Lowassa wa mwaka 2015, Membe si aina ya wanasiasa waliokuwa na mvuto wa kuhama na maelfu ya wanachama au wafuasi.
Kwa maana nyingine, Membe si sawa na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye kitendo chake cha kuhama kutoka chama cha CUF na kuhamia ACT kimebadili kabisa ramani ya kisiasa ya Zanzibar.
Hata hivyo, Membe ana sifa za kipekee zilizofanya viongozi wa ACT wamtongoze ajiunge na chama hicho. Hizo ni sifa zitakazokifanya chama hicho kiimarike zaidi kuliko kilivyo sasa.
Kwanza, Membe ni mwanachama mpya ambaye amewahi kuwa waziri na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Tofauti ya ACT Bara na ACT Zanzibar ni kwamba huku Bara viongozi wake kitaifa ni watu ambao hawana uzoefu wa kiuongozi serikalini na oganaizesheni kama wenzao wa visiwani.

Chanzo cha picha, Alamy
Membe anapunguza nakisi hiyo na kukifanya chama hicho kizidi kuonekana kuwa na watu walio tayari kuongoza nchi kama watapewa madaraka baada ya uchaguzi.
Mwanadiplomasia huyu pia anafahamika kwa kuwa na marafiki wengi ndani na nje ya nchi. Katika mazingira ya sasa ambapo matajiri wa Kitanzania wana hofu ya kuhusishwa na vyama mbadala, kuwa na mwanasiasa mwenye ushawishi nje ya nchi ni faida.
Jambo jingine ambalo Membe analileta kwenye upinzani ni kuhusu eneo analotoka. Waziri huyu wa zamani anatokea mikoa ya Kusini mwaTanzania ambayo taratibu inaonekana kuanza kuwa ngome ya vyama vya upinzani.
ACT Wazalendo, na upinzani kwa maana nyingine, unatarajia kuwa kumpata Membe kutasababisha ipate kura nyingi katika mikoa hiyo ambayo inaelezwa kuwa tayari ina "rutuba" ya kisiasa.
Propaganda ya Udini
Barani Afrika, ni vigumu kuepuka kuhusisha siasa na vitu kama udini, ukabila na upendeleo. Zipo nchi zimewahi kuingia vitani kwa sababu za kikabila na kidini.
Tanzania, ingawa imejitahidi sana kujiepusha na siasa za namna hiyo, zimekuwa zikiibuliwa wakati wa kampeni. Wakati CUF kikiwa chama kikuu cha upinzani, kilikuwa kikihusishwa na Uislamu na Chadema bado kimekuwa kikihusishwa na Ukristo. CCM kwa sababu ya kuwa chama tawala chenye mizizi nchi nzima, kimekuwa kikiepuka tuhuma hizi.
Sehemu kubwa ya viongozi wa juu wa ACT Wazalendo ni Waislamu na ni rahisi kwao kuanza kuhusishwa na propaganda ya udini.
Ujio wa Membe unafuta dhana hiyo. Mbunge huyu wa zamani wa Jimbo la Mtama si Mkristo wa kawaida kwani ni Mkatoliki ambaye alifikia hatua ya kutaka kusomea Utawa katika Seminari ya Peramiho kabla ya kukatisha baada ya kupata nafasi ya kusoma sekondari ya Itaga.
Kwa tukio hili la kumpata Membe, ACT Wazalendo inaamini itakuwa rahisi kupambana na propaganda za udini dhidi yake.
Mshindani wa Magufuli?
Hakuna kiongozi mmoja au chama kimoja cha upinzani hapa nchini kinachoweza kuishinda CCM chenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Namna pekee ya upinzani kupata matokeo mazuri kwenye uchaguzi huu ni kwa kumsimamisha mgombea mmoja atakayeungwa mkono na vyama vya upinzani.
Vyama viwili; ACT na Chadema, ndivyo vinavyotakiwa kutafuta namna ya kushirikiana na kupata mgombea mmoja kuanzia ngazi za chini hadi ile ya Urais.
Katika mahojiano yake na BBC hivi karibuni, Membe alisisitiza pia umuhimu wa jambo hilo la kusimamisha mgombea mmoja.
Hadi sasa, inaonekana mmoja kati ya wanasiasa wafuatao; Membe, Lazaro Nyalandu, Tundu Lissu na Freeman Mbowe; ndiye atapewa nafasi hiyo- au wawili kati ya hao ndiyo hatimaye watasimama.
Kama ACT Wazalendo na Chadema watasimamisha wagombea kila mmoja; CCM itapata ushindi mkubwa kuliko iliyoupata mwaka 2015. Kama hatimaye watakubaliana; iwe Membe au mwingine yeyote, hali inaweza kuwa tofauti.
Ni suala la kusubiri. Katika mafunzo ya uwindaji, somo la kwanza, hata kabla hujafunzwa shabaha, linahusu subira. Inaweza kuchukua saa kadhaa kabla kitoweo hakijaonekana.
Bernard Membe ni mwindaji. Atasubiri.
Membe ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Bernard Kamillius Membe alizaliwa katika kijiji cha Rondo, mkoani Lindi mnamo Novemba 9 mwaka 1953. Alipata elimu yake ya awali katika Shule ya Msingi Rondo-Chiponda na kusoma katika sekondari za Namupa na Seminari ya Itaga kwa masomo ya juu ya sekondari.
Ni mhitimu wa masomo ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani.
Membe na mkewe, Dorcas, walifunga ndoa Agosti mwaka 1985 na katika uhusiano wao huo wamejaliwa kupata watoto watatu.












