Familia ya mwandishi wa habari wa Kenya anayezuiliwa Ethiopia haina taarifa kumuhusu

Chanzo cha picha, Yassin Juma/ Facebook
Zaidi ya wiki moja baada ya mwandishi wa habari wa Kenya kukamatwa nchini Ethiopia, familia yake inasema hakuna taarifa kuhusu ni wapi alipo wala hali yake ya kiafya.
Yassin Juma alikamatwa na vikosi vya usalama vya Ethiopia tarehe 2 Julai , kufuatia maandamano makubwa yaliyoibuka baada ya mauaji ya mwanamuziki maarufu Hachalu Hundessa.
Familia yake inasema kuwa bado hawajapokea mawasiliano yoyote kuhusu ni wapi bwana Yassin Juma anashikiliwa.
'' Sijui ni kwanini alikamatwa nchini Ethiopia kwasababu alikua anafanya tu kazi yake ya kuripoti habari. Alitutumia picha za ghasia na maandamano na wanajeshi wakiwakamata watu. Alituomba tumpigia simu kwani alikua anahofia maisha yake…''
''Alituma picha nyingine zikionesha alikua amezingirwa na kile kilichokua kikiendelea karibu na mji, alikua amejaribu kujificha na akatuomba tumuombee '', anasema mke wake Yassin Juma'', Asha Mohamed.

Chanzo cha picha, Yassin Juma/Facebook
Taarifa kuhusu mwandishi huyu wa habari maarufu nchini Kenya hazijulikani tangu alipochukuliwa na vikosi vya usalama tarehe 2 Julai.
"Tunaomba kwamba serikali itatusaidia ili walau Yassin Juma awezi kurudi nyumbani, kwasababu watoto na mimi mwenyewe tunamuhitaji kwasababu yeye ndiye anayetegemewa na familia hata awapo safarini. Kwa hiyo tunaomba kwa unyenyekevu. Kama alifanya makosa nchini Ethiopia msamehe. Ninaomba kwa niaba yake tafadhali mleteni kwetu . " Amesema mke wa Juma, Asha Mohammed.
Juma ni miongoni mwa watu zaidi ya 4,000 waliokamatwa na polisi kufuatia maandamano ya ghasia wakiwemo wanaume wawili wanaoshukiwa kumpiga risasi msanii Hachalu Hundessa.

Chanzo cha picha, Yassin Juma / Facebook
Familia yake sasa inataka majibu ya ni wapi aliko, ikizitaka serikali za Kenya na Ethiopia kumrejesha Kenya akiwa salama.
''Kwa serikali ya Kenya, ningependa imsaidie baba yetu arudi nyumbani. Na kwa serikali ya Ethiopia pia, ningependa sana imuachilie huru baba yangu kwasababu sidhani amefanya uhalifu wowote, kwasababu anafanya kazi ya uandishi wa habari, na sidhani kama uandishi wa habari unahusiana na uhalifu. Ningependa sana serikali ya Ethiopia kumrudisha nyumbani baba yangu'', Hafis Yassin mtoto wa kiume wa Yassin alisema.
Unaweza pia kusoma:
Duru mbali mbali zimeiambia BBC kuwa Juma alikamatwa alipokua katika makazi ya mtaalamu maarufu wa mawasiliano mwenye utata ambaye aligeuka na kuwa kiongozi wa upinzani Jawar Mohammed - ambaye pia anashikiliwa mahabusu na vyombo vya usalama nchini Ethiopia.

Chanzo cha picha, Reuters
Juma anaaminiwa kuwa amekua akifanya kazi nchini Ethiopia kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Wakati Jawar na wanasiasa wengine waliokamatwa walishitakiwa mahakamani kwa kuchochea ghasia, serikali ya Ethiopia imebaki kimya kuhusu hatma ya Bwana Juma.
Wakati huo huo ubalozi wa Kenya nchini Ethiopia unasema kuwa umeiandikia barua wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia kutaka kujua hali ya mwandishi huyo wa habari.
''Ningependa kupongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya Ethiopia, na tunafurahia wanashughulikia suala hili na tunaamini na tuna Imani kwamba watatupa matokeo mazuri , hususan ni wakati huu ambapo tunajua kwamba yuko hai, na labda kama hawatafuatilia hali na tupate taarifa juu ya kile kinachoendelea, tutashukuru sana'', amesema Nick Muyoti msemji wa familia.
Waandishi kadhaa wa habari nchini Ethiopia pia wamekua wakikamatwa wakati wa ghasia, lakini kwasababu mawasiliano ya inteneti bado yamezimwa kote nchini humo, taarifa zimekuwa chache kuwahusu Anasema Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza ambaye amekua akifuatilia taarifa za Ethiopia.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema yanahofia kamata kamata inayoendelea na familia ya Yasin ina sababu ya kuwa na wasiawasi












