Raia wa Malawi wanashiriki duru ya pili ya uchaguzi wa urais

Chanzo cha picha, AFP
Raia wa Malawi wanapiga kura leo katika awamu ya pili ya uchaguzi wa urais, miezi mitano baada ya mahakama ya katiba kufuta matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana.
Rais Peter Mutharika awali alikua ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi Mei 2019 kwa ushindi mdogo wa 38.5%. Lakini upinzani ulipinga matokeo hayo mahakamani, ukilalalmikia wizi wa kura.
Mutharika anakabiliana na Mchungaji aliyegeuka kuwa mwanasiasa Lazarus Chakwera - ambaye anashikilia bendera ya muungao wa upinzani. Mgombea wa tatu ni, Peter Kuwani,ambaye anaonekana kama mtu wa nje katika kinyang'anyiro hicho cha kuingia ikulu ya Malawi.
Uchaguzi unafanyika chini ya sheria mpya, ambapo mshindi sasa atahitaji kupata wingi wa kura wa 51% . Baada ya miezi ya hali ya suitafahamu ya kisiasa na wakati mwingine maandamano ya ghasia, Malawi imegawanyika pakubwa.
Nchi hiyo inahangaika kiuchumi,na viwango vya umaskini na ukosefu wa ajira ni vya hali ya juu, huku serikali inakabiliwa na ukosoaji mkubwa kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri.
Wamalawi wanatumai kuwa matatizo haya yatatatuliwa na uchaguzi wa leo wa kihistoria.

Chanzo cha picha, AFP
Vyama vikuu vya upinzani sasa vimeungana na kumuunga mkono mgombea mmoja anayekabiliana na rais Mutharika, ambaye anagombea kuwania muhula wa pili mamlakani.
Rais aliye madarakani Peter Mutharika alitangazwa mshindi mwezi Mei 2019 baada ya kupata ushindi mdogo wa asilimia 38.5 ya kura zote zilizokuwa zimepigwa.
Lakini viongozi wa upinzani walipinga matokeo hayo mahakamani wakidai kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.
Majaji walikubaliana nao na kutupilia mbali matokeo hayo Februari na kuagiza marudio ya uchaguzi huo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa miezi kadhaa sasa, raia wa Malawi wamekuwa katika mgogoro wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo. Ni zaidi ya mwaka sasa tangu mamilioni ya raia walipojitokeza katika uchaguzi wa bunge na urais.
Kumekuwa na maandamano ya kupinga serikali pamoja na kutokea kwa ghasia ambako kumetishia nchi hiyo kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi.
Masuala ibuka
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Malawi pia amejiuzulu huku wanachama wapya wa tume hiyo wakichaguliwa ili kusimamia uchaguzi huo.
Uchaguzi huu unafanyika chini ya sheria tofauti baada ya mahakama kutoa uamuzi kwamba mfumo wa chaguzi zilizopita (anayepata kura nyingi hata kama hajafikisha asilimia hamsini ya kura zilizopigwa anatangazwa mshindi) ulikuwa kinyume na katiba.
Atakayeibuka na ushindi kati ya wagombea hao wawili, atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na mgawanyiko uliojitokeza na kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika kipindi cha mwaka moja uliopita.
Kukabiliana na ufisadi, kupunguza umaskini na ukosefu wa ajira ni miongoni mwa masuala ya msingi katika uchaguzi huo.
Raia wa Malawi wana imani kwamba sauti zao zitasikika na kuwa Jumanne pengine huenda ikawa ndio mwanzo mpya kwa nchi hiyo.












