Kwanini familia zimekuwa 'zikiwauwa kwa heshima' watoto wao wa kike Pakistani?

Wanaharakati wakipinga utamaduni wa mauaji ya heshima Pakistan

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanaharakati wakipinga utamaduni wa mauaji ya heshima Pakistan

Mauaji ya wasichana wawili walioonekana katika kanda moja ya video yamezua upya suala la 'mauaji yanayodaiwa kuwa ya heshima' nchini Pakistan.

Mauaji ya wasichana hao yanaonekana kuhusishwa na kanda hiyo ya video ambayo ilisambazwa katika mitandao ya jamii,

Kanda hiyo ilioonekana na BBC inamuonesha kijana mmoja akijirekodi video na wasichana watatu katika eneo lililojificha.

Inaonekana kwamba kanda hiyo ya video ilirekodiwa mwaka mmoja uliopita lakini ikasambaa sana wiki chache zilizopita.

Tayari mtu aliyerekodi video hiyo akiwapiga busu wasichana wawili kati yao amekamatwa na kushtakiwa, kulingana na maafisa wa polisi nchini Pakistan.

Lakini je 'mauaji ya heshima' ni ya aina gani?

Ni mauaji ya ndugu wa familia ambaye anadaiwa kuleta aibu miongoni mwa watu wa familia.

Wanaharakati wanasema kwamba sababu za kufanyika kwa mauaji hayo ni kwamba mwathiriwa:

  • Alikataa kuolewa
  • Alikuwa mwathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia au ubakaji
  • Alishiriki ngono nje ya ndoa hata iwapo ni madai tu.

Lakini mauaji yanaweza kufanyika kwa sababu ndogo , kama vile kuvalia nguo kwa njia ambayo inaonekana kukosa heshima.

"Wanaotekeleza mauaji hayo huyatumia kama sababu ya kulinda heshima na maadili ya familia zao kulingana na Mustafa Qadri , Mtafiti nchini Pakistan.

Mwaka 2011 wanawake watatu waliuawa nchini Pakistan baada ya kurekodiwa katika kanda ya video wakicheka na kunyeshewa na mvua nje ya nyumba yao ya familia.

Wanaume pia hulengwa , na ndugu za wanawake ambao wanadaiwa kushiriki nao katika uhusiano wa kimapenzi.

Mwaka uliopita nchini India, wanandoa wachanga waliuawa katika jimbo la Haryan kwasababu walipanga kuoana licha ya kutoka sehemu moja.

Nidhi Baraka, mwenye umri wa miaka 20 alipigwa hadi kufa huku Dharmender Barak akikatwakatwa akiwa hai hadi kufa.

Lakini Rothna Bagum , mtafiti kuhusu masuala ya mashariki ya kati na Afrika kaskazini wa shirika moja la haki za kibinadamu , anasema kwamba huathirika sana na adhabu kama hizo kwasababu huonekana kama walezi wa familia ama watu wenye heshima kubwa katika familia.

line break

Je, familia zinahalalisha vipi mauaji?

Wazo la kwamba mauaji yanaweza kuwa ya heshima linaaminika kutoka katika tamaduni za kikabila ambapo madai dhidi ya mwanamke yanaweza kutosha kuharibu heshima ya familia - mbali na imani kwamba maisha bila heshima sio maisha.

Wanaotekeleza maovu hayo mara nyengine wamejaribu kutumia dini ili kuendeleza vitendo vyao - lakini hakuna hata dini moja duniani inayounga mkono uhalifu kama huo.

Katika baadhi ya mataifa , tamaduni hizi za kidini zimeidhinishwa katika sheria - ambayo inaweza kuwa sababu ya kumuua mtu wa familia.

Kwa mfano maeneo yanayosimamiwa kikabila nchini Pakistan kama vile 'rivaj' - imewekwa katika sheria bila kuelezewa.

Hatua hiyo inaweza kuwa sababu za kisheria za kumuua mtu wa familia, kulingana na bwana Qadri.

Nidhi na Dharmender

Chanzo cha picha, Other

Maelezo ya picha, Nidhi na Dharmender waliuawa na fanilia ya Nidhi kwa kupanga njama ya kufunga ndoa

Mauaji haya pia yameenea sana katika jamii zisizo na haki na zile zinazoishi katika maeneo ya mashambani.

Makosa ya serikali kushindwa kukabiliana na uhalifu na uungwaji mkono na viongozi huchangia kwa tabia hizo kukubalika katika jamii, kulingana na bwana Qadri.

Lakini kuna imani zilizojikita ndani ya jamii kwamba vitendo vya mwanamke vinaonesha anaishi na wanaume wa aina gani, anaongezea.

line break

Familia inaamuaje kuua?

"Kwa lengo la kudai kulinda heshima ya familia , wanawake na wasichana hupigwa risasi, hupigwa mawe na kuchomwa , kuzikwa wakiwa hai , hunyongwa na kudungwa kisu hadi kufa, ilisema taarifa kutoka kwa Umoja wa mataifa wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Wakati mwingine mauaji hufanyika mara kwa mara, lakini katika hali zingine yanaweza kuwa rasmi na kupangwa.

Mkutano unaweza kufanywa na wanafamilia wa kiume na wanawake wakubwa ambao wanaamua ikiwa mwanamke anapaswa kuuawa, na kuamua ni njia gani itakauotumika kumuua.

Katika kisa cha kushangaza Farzana Parveen , ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu , alipigwa mawe na ndugu zake kwasababu aliolewa kinyume na matarajio yao.

Wanawake waomboleza mwili wa Farzana Parveen

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanawake waomboleza mwili wa Farzana Parveen
line break

Je wanaotekeleza vitendo hivyo hushtakiwa

Mauaji mengi yanayotekelezwa huwa vigumu kuyathibitisha ama hata kuyafungulia mashtaka .

Huwa hakuna mashahidi na jamii hukata kushirikiana na polisi ili kuwasaka waliotekeleza vitendo hivyo viovu.

Nchini Pakistan , mashtaka yanayofunguliwa dhidi ya washukiwa ni machache mno kutokana na sheria za kuwasamehe waliotekeleza vitendo hivyo.

Hata wanapofunguliwa mashtaka , wanaume walioshiriki katika mauaji hupata adhabu hafifu.

Rukhsana na mumewe Mohammad
Maelezo ya picha, Rukhsana Bibi anasema kwamba alinusurika jaribio la kumshambulia lililomwacha mumewe akiwa amefariki katika eneo la Kohistan

Rukhsana Bibi anasema kwamba alinusurika jaribio la shambulizi lililomwacha mumewe akiwa amefariki katika eneo la Kohistan, eneo la mashambani katika jimbo la kaskazini mwa Pakistan.

Ni mmojawapo wa wanawake wachache ambao wamezungumzia kutafuta haki . Hakuna mtu aliyefunguliwa mashtaka kufuatia shambulio hilo.

Mauaji ya heshima yanapaswa kuchukuliwa kama mauaji ya kawaida, anasema bi Bagum.

Familia za mwathiriwa zinafaa kupata ulinzi na hukumu hazifai kupunguzwa wakati mtu anapopatikana na hatia , anaongezea.