Coronavirus: Wafahamu watu mashuhuri waliofariki kwa ugonjwa wa corona Afrika

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Nguli wa muziki wa Jazz nchini Cameroon, Manu Dibango amefariki kutokana na coronavirus (Covid-19) nchini Ufaransa
Mchapishaji wake amethibitisha kuwa alifariki katika hospitali moja nje kidogo ya mji wa Paris.
Kifo chake kimeongeza idadi ya watu mashuhuri barani Afrika waliofariki kutokana na ugonjwa wa corona au hali ya afya ya awali ambayo ilizoroteshwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Dibango mwenye umri wa miaka 86, alikuwa muimbaji na mtunzi mkubwa muziki na kazi yake ilitambulika karibu kila pembe barani Afrika, Ulaya na kwengineko haswa kutokana na umahiri wake wa kupuliza midomo ya bata.
Mtindo wake wa muziki uliojumuisha jazz, funk na muziki wa Cameroon ulichangia kubuniwa kwa bendi kama vile Kool and the Gang miaka ya 70 hadi Hip hop miaka ya 90.

Chanzo cha picha, Getty Images
Manu Dibangu ni nani?
Alizaliwa mwaka 1933 katika mji wa Douala, alipenda sana kuenda kanisani, ambako talanta yake ya muziki ilianzia.
Baadae alisomea somo la muziki hatua ambayo iliimarisha uimbaji wake.
Manu Dibangu alipata umaarufu wake kutokana na kibao chake Soul Makossa, ambacho aliutoa kwa ushirikiano na wasani wengine kama vile Herbie Hancock na Fela Kuti.
Mwaka 2009, aliwashitaki waimbaji mashuhuri, Michael Jackson na Rihanna, kwa madai ya kwa kutumia baadhi ya maneno ya utunzi wake katika nyimbo zao, kesi ambayo ilisuluhishwa nje ya mahakama.


Watu wengine mashuhuri waliofariki kutokana na sababu zinazohusiana na maambukizi ya coronavirus ni:
Aurlus Mabele (Mwamuziki wa DRC )
Alhamisi iliyopita mfalme wa miondoko ya soukouss, Aurlus Mabelé, kutoka Congo Brazaville alifariki duniani mjini Paris Ufaransa baada ya kuambukizwa virusi vya Corona.
Taarifa za kifo chake zilitangazwa na binti yake Liza Monet ambaye pia ni mwanamuziki.
Muziki wa Aurlus Mabelé aliyefariki akiwa na umri wa miaka 67 ulipata umaarufu mkubwa miaka ya 1990.

Chanzo cha picha, YOUTUBE
Wakati wa kifo chake masnii huyo alikuwa tayari anauguza uvimbe wa koo hali ambayo ilimtatiza kwa takribani miaka kumi.
Hali hiyo ya udhaifu ya tangu zamani haikumruhusu kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Mabélé, ambaye jina lake asili ni Aurélien Miatsonama alianzisha bendi ijulikanayo kama Loketo mnamo mwaka 1986, ambayo ilijipatia umaarufu Afrika mzima kutokana na muziki wake wakuchangamsha maarufu kama soukous.
Hadi kifo chake alikuwa na zaidi ya albamu zmilioni 10 zilizouzwa ulimwenguni kwa zaidi zaidi ya miaka 30 ya tasnia yake ya muziki.
Mwanamuziki huyo alihamia Ufaransa mwaka 1980.
Mazungumzo na serikali ya Congo bado yanaendelea ili mwanamuziki huyo arudishe kuzikwa nyumbani.
Lakini kwa sasa mwili wake hauwezi kusafirishwa kurejea Congo mpaka katazo la kusafiri liondolewe.
Zororo Makamba (Mwanahabari Zimbabwe)

Chanzo cha picha, Zororo Makamba
Jumatatu wiki iliyopita Zimbabwe ilirekodi kifo cha kwanza kilichotokana na ugonjwa corona.
Hii ni baada ya mwanahabari Zororo Makamba,30, kufariki kutoka na coronavirus siku kadhaa baada ya kupatikana na maambukizi ya virusi hivyo hatari.
Zimbabwe ilitangaza mpango wa kufunga mipaka ya nchi hiyo lakini kama hatua ya kukabiliana na kusambaa kwa maambukizi ya corona lakini nchi hiyo inakabiliwa na uhaba wa chakula.
Hatua hiyo imezua hofu ya usalama wa chakula utekelezaji wake ukidumishwa.
Rose Marie Compaore (Makamu wa kwanza wa spika wa bunge la Burkina Faso)

Chanzo cha picha, Reuters
Mwishoni mwa wiki iliyopita mamlaka nchini Burkina Faso ilitoa maelezo ya mgonjwa wa kwanza aliyefariki kutokana na ugonjwa wa corona (Covid-19).
Maafisa walisema muathiriwa ni mwanamke wa miaka 62 ambaye alikuwa anaugua maradhi ya kisukari kabla ya kupata maabukizi ya virusi vya corona.
Chama cha Union for Progress and Change (UPC) kilisema marehemu alikuwa mbunge Rose-Marie Compaore, ambaye ni makamu wa kwanza wa spika wa bunge.
Burkina Faso ilesema idadi ya walioambukizwa kufikia wakati huo ilikuwa 27.
Wengine waliojitenga kwa kuhofia maambukizibaada ya kutangamana na waathiriwa ni :
- Cavaye Yeguie Djibril - Rais wa bunge la Cameroon
- Amason Kingi - Gavana wa jimbo la Kilifi Pwani ya Kenya
- Khamis Mwinjuma - Rappa wa Tanzania
- Nathaniel Balma- Mkuu wa shirika la kulinda misitu Liberia
- Idris Elba Muigizaji wa filamu za Marekani ambaye mia ni raia wa Sierra Leonean pamoja na mke wake.












