Je, maridhiano ya BBI yamegeuka kuwa mpasuko wa kisiasa Kenya?

Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bwana Odinga na Bwana Kenyatta walishikana mikono kama ishara ya kumaliza uhasama wa kisiasa kufuatia uchaguzi wenye utata wa mwaka jana 2017.
    • Author, Na Hezron Mogambi
    • Nafasi, Chuo Kikuu Cha Nairobi

Huku siasa kuhusu uhamasishaji juu ya mchakato wa ripoti ya Jopo la maridhiano nchini Kenya (BBI) zikichacha, kumezuka tofauti kati ya wanasiasa wakuu nchini Kenya kuhusiana na mbinu na njia za kufuata katika kufanikisha suala hili.

Siasa zenyewe zinatokana na shauku kuhusu taratibu za kufuata, mipango na mipangilio ya mikutano ya uhamasishaji na siasa zinazohusiana na uchaguzi mkuu nchini Kenya wa mwaka wa 2022.

Vuta nikuvute kuhusiana na ripoti hii imefanya serikali ya Kenya kuonekana yenye kuvuta pande mbili kuhusiana mpangilio na hatima ya ripoti hii.

Kuna makundi mawili ambayo yameibuka kutokana na shughuli nzima ya BBI na hatima yake.

Kwa upande mmoja kuna wale wanaomuunga mkono makamu wa rais ambaye wamekuwa wakipinga utaratibu mzima wa jopo la maridhiano pamoja na jinsi ya kutekeleza mapendekezo yake na kwa upande mwingine kuna wale wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga ambao ndio waanzilishi wa Jopo hili la Maridhiano la Kenya.

Itakumbukwa kuwa Jopo la Maridhiano nchini Kenya (BBI) liliundwa kutokana na tofauti zilizozuka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka wa 2017 ambazo zilitishia kuleta utata nchini Kenya.

Baadaye, Rais Uhuru alipoapishwa na kuingia ofisini, waliamua kuzika tofauti zao na kukutana mnamo Machi 9, 2018 na kuorodhesha ajenda tisa ambazo walisema ndizo zilizowafanya kuanza kufanya kazi pamoja kwa minajili ya kuboresha Kenya na siasa zake.

Baadhi ya wanasiasa wa Kenya wanahofu kuwa mchakato wa BBI na ripoti yenyewe ni mpango wa kisiri wa kumnyima Naibu Rais Dkt. William Ruto fursa ya kuongoza nchi.
Maelezo ya picha, Baadhi ya wanasiasa wa Kenya wanahofu kuwa mchakato wa BBI na ripoti yenyewe ni mpango wa kisiri wa kumnyima Naibu Rais Dkt. William Ruto fursa ya kuongoza nchi.

Ajenda za kuundwa kwa Jopo la Maridhiano ni pamoja na jinsi ya kumaliza migawanyiko ya kikabila, kuwashirikisha watu wote kuhusu masuala ya utawala na siasa za Kenya.

Jinsi ya kushughulikia suala la kumaliza uhasama wa kisiasa unaotokea wakati wa uchaguzi mkuu, jinsi ya kuimarisha amani na usalama, kukabiliana na janga la ufisadi, jinsi ya kukabiliana na ukosefu wa maadili ya kitaifa, masuala ya majukumu na haki za raia, masuala ya kuwajibika kwa pamoja na jinsi ya kuendeleza serikali za ugatuzi.

Kitakachofuatia baada ya Wakenya kukubaliana juu ya ripoti ya BBI

Viongozi hawa wawili wa Kenya wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Kenya baadaye waliunda kamati ya watu kumi na nne ambao waliandaa mikutano ya umma kwenye majimbo 47 kote nchini Kenya, ili kupokea maoni kuhusu mabadiliko wayatakayo wakenya.

Kamati hiyo ilikusanya maoni kutoka kwa wakenya wapatao elfu saba na kuandaa ripoti ambayo sasa inaendelea kujadiliwa zaidi na Wakenya ili kuiboresha.

Ikiwa Wakenya watakubaliana na yaliyomo kwenye ripoti hiyo, huenda kura ya maoni ikaitishwa na kuerekebisha katiba ya mwaka wa 2010 ambayo itasababisha mabadiliko katika muundo wa serikali.

Jambo hili ndilo limekuwa likiwatia kiwewe baadhi wa wanasiasa wa Kenya waking'ang'ania kuwa mchakato wa BBI na ripoti yenyewe ni mpango wa kisiri wa kumnyima Makamu wa rais Dkt. William Ruto kuwania na kushinda Urais katika kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa 2022.

Moses Wetangula (kushoto) na Kalonzo Musyoka (kulia) ambao walikuwa katika Muungano wa Upinzani NASA pamoja na Odinga hawakuhusishwa katika mpango wa BBI

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Moses Wetangula (kushoto) na Kalonzo Musyoka (kulia) ambao walikuwa katika Muungano wa Upinzani NASA pamoja na Odinga hawakuhusishwa katika mpango wa BBI

Kwa sasa, imebainika wazi kuwa Serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta imewatwika majukumu magavana wa Kaunti katika kufanikisha na kutayarisha mikutano ya uhamasishaji katika maeneneo mbali mbali nchini Kenya.

Tayari, mikutano mitatu imeshafanyika magharibi mwa Kenya huku wa hivi karibuni ukifanyika mnamo Jumamosi iliyopita katika mji wa Mombasa, pwani ya Kenya.

Makamu wa rais William Ruto na wabunge wanaomuunga mkono wamekuwa wakikosoa mchakato wa Jopo la Maridhiano nchini Kenya (BBI) kwa kudai kuwa ni njia ya kuharibu pesa za umma na kuwatwika Wakenya mzigo zaidi.

Aidha, wamekuwa wakimsuta kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakidai kuwa kuwa mchakato huo ulikuwa mpango wake wa kunyakua madaraka kupitia mlango wa nyuma.

Mikutano kuhusu BBI inaonekana kuleta mgawanyiko

Tangu Jopo la Maridhiano kuundwa na Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, wanasiasa wanamuunga mkono Naibu Rais wa Kenya Dkt William Ruto wamekuwa wakidai njama ya kutengwa kwa Bw. Ruto kutoka uongozini.

Aidha, wanasiasa hawa wamekuwa wakilitupia cheche za maneno jopo hili la BBI kwa kutohusishwa katika uanzilishi wake na kutojua bayana mwanzo na mwisho wake.

Hata hivyo, joto la kisiasa nchini Kenya kuhusiana na suala la BBI limepungua kuanzia Jumamosi wakati kundi linalomuunga mkono Bw. Ruto kubadili msimamo wao na kuhudhuria mikutano ya uhamasishaji kuhusu ripoti ya BBI.

Hatua hii ya kuamua kubadili msimamo na mikakati yao kuhusu ripoti ya BBI imezua cheche za maneno baina ya wanasiasa kwenye mirengo pinzani.

Hali hii imepelekea kutiliwa shaka jinsi mikutano hiyo itakavyoendelezwa kwenye maeneo mbalimbali.

Tayari kundi la wabunge linalomuunga mkono Bwana Ruto limefanya mkutano wa siku mbili mjini Naivasha kupanga mkakati kuhusu ripoti ya BBI na msimamo wao kuhusiana na mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Wabunge hao waliongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Bw Kipchumba Murkomen, Kiranja wa Wengi katika Seneti Bi Susan Kihika, mbunge Moses Kuria kati ya wengine.

Dkt Ruto alisema kuwa kamati inayoongoza mchakato huo inapaswa kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanapewa nafasi kutoa maoni yao na hautekwi na wanasiasa kama jukwaa la kuendeleza chuki na ukabila.

Joto la kisiasa lililokuwepo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi liliwasukuma Bwana Kenyatta na Bwana Raila kuandaa mpango wa maridhiano wa BBI

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Joto la kisiasa lililokuwepo miongoni mwa raia baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi liliwasukuma Bwana Kenyatta na Bwana Raila kuandaa mpango wa maridhiano wa BBI

"Kamati ya BBI inapaswa kuweka utaratibu ambapo kila Mkenya atapata nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu ripoti hiyo bila kuingiliwa na wanasiasa.

Inapaswa kuhakikisha mchakato huu umelindwa dhidi ya mwingilio wa aina yoyote ile," akasema Dkt Ruto.

Mnamo Jumanne, Bw. Murkomen, ambaye pia ni Seneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, alidhibitisha kushiriki kwa kwenye mikutano ya uhamasisho ili kuondoa dhana kwamba wamekuwa wakipinga mchakato huo.

Dkt William Ruto amekuwa akionekana kutengwa

Kwa upande mwingine, wanasiasa wa upinzani wanaoumuunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga wamewasuta wenzao kwa kubadilisha msimamo kuhusu mikutano ya uhamasisho huku wakionekana kuwaapa masharti ya kuhudhuria mikutano hiyo. Kwa upande wake, Dkt Ruto amesisitiza kuwa hakuna kundi lolote linalopaswa kutoa kanuni kwa Wakenya kuhusu wanavyopaswa kushiriki kwenye mchakato wa ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

Lililo bayana ni kuwa, siku za hivi karibuni Dkt Ruto amekuwa akionekana kutengwa kwenye mipangilio ya maandalizi ya mikutano hiyo, huku washiriki wakuu wakiitumia kumshambulia kisiasa.

Hili limebainika wazi kwani Naibu Rais hajaonekana katika mikutano iliyofanyika; mjini Kisii na Kakamega, licha ya kusema anaunga mkono mchakato huo.

Wadadisi wa kisiasa wanaeleza kuwa lengo kuu la kundi linalomuunga mkono Bw. Ruto kubadili msimamo wake kighafla linalenga kuondoa dhana kuwa Dkt Ruto anapinga ripoti hiyo, licha ya kuwa ajenda ya serikali.

Raila Odinga na Uhuru Kenyatta

Chanzo cha picha, Reuters

La mno na kinachowakera zaidi wendani wa Bw. Ruto ni ukweli kuwa kwa sababu ya kutoshiriki zaidi katika mikutano hii yenye nia ya kuwahamasisha Wakenya kuhusu ripoti ya BBI kwa sababu ya wadhifa wake,Bw. Raila Odinga ameonekana kuchukua nafasi muhimu katika kuongoza mikutano hii.

Jambo hili linaonekana kumjenga zaidi kisiasa hali ambayo imepelekea baadhi ya wanasiasa kudai kuwa wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na Bwana Raila Odinga wanatumia mchakato wa BBI vibaya ili "kufufua hali zao za kisiasa".

Kuna tetesi nchini Kenya sasa kuwa huenda kundi hili likaanda mikutano yake kuwahamasisha Wakenya kuhusu ripoti ya BBI.

"Ile kamati ya BBI ni lazima ifanye kazi kwa mpango na utaratibu na kutowahusisha "wanabiashara na wasiokuwa na kazi ya kufanya ambao wanataka kuuteka mchakato huu wa BBI," alidai Dkt Ruto mapema juma lililopita.

Mwanasiasa wa upinzani ambaye pia ni kiongozi wa chama cha upinzani Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi pia amekuwa akitilia shaka kukosekana kwa uwazi na pande zote za kisiasa kutojumuishwa katika mchakato wa BBI.

"Hapo awali, tatizo lilikuwa kuhusiana na ni nani anayeandaa mikutano na kuilipia baada ya kumalizika kwa muda wa kuhudumu kwa kamati hii.

''Ilikuwaje tena kuwa baadhi yetu tulitengwa kama wapinzani wa ripoti ya BBI ilhali tulikuwa tumeshaeleza kuwa tunaunga mkono ripoti hii?"

Bwana Mudavadi aliuliza juma lililopita. Maoni kama haya yemtolewa na kiongozi wa chama cha Fork-K Bwana Moses Wetangula ambaye pia ni seneta wa Bungoma.

Unaweza pia kutazama:

Maelezo ya video, Waziri wa maswala ya Kigeni Tanzania Paramagamba Kabudi awataka Wakenya kuiga mfano wa Wat

Bila shaka, siasa kuhusu mchakato wa ripoti ya BBI na hatima yake zitatawala siasa za Kenya mwaka huu.

Prof. Hezron Mogambi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi. baruapepe: [email protected]