Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sheria ya Uraia India: Watu sita wauawa wakipinga mabadiliko ya sheria inayolalamikiwa na Waislamu
Maandamano makali yanaendelea nchini India kupinga sheria mpya juu ya wahamiaji na kusababisha mapambano makali na polisi.
Mpaka sasa, takribani watu sita wamepoteza maisha kufuatia siku tano za makabiliano makali na vyombo vya usalama.
Kati yao, wawili wameuawa katika jimbo la kaskazini mashariki la Assam, ambapo kwa mujibu wa maafisa usalama waliuawa baada ya mamia kukiuka marufuku ya kutotoka nje.
Maelfu ya polisi na wanajeshi wamepelekwa katika maeneo ambayo watu wanaandama ili kutuliza ghasia.
Huduma za mawasiliano ya intaneti pia zimezimwa ili kufanya ugumu kwa watu kuwasiliana.
Mtafaruku huo unakuja siku chache tu baada ya bunge la India kupitisha mabadiliko ya sheria ya Uraia ambayo wakosoaji wanasema ni sehemu ya ajenda ya serikali kuwakandamiza Waislamu.
Sheria hiyo inawapatia msamaha wahamiaji haramu ambao si Waislamu kutoka nchi tatu za jirani ambazo wasio waislamu ni wachache, nchi hizo ni Pakistani, Bangladeshi and Afghanistani.
Wahamiaji hao pia wanapatiwa uraia wa India baada ya sheria kupita.
Serikali ya India inaongozwa na chama cha kitaifa cha Kihindu Bharatiya Janata Party (BJP), ambacho kinadai kuwa hatua hiyo itawapatia hifadhi watu ambao wanakimbia unyanyasaji wa mateso kutokana na imani zao za dini.
Maandamano hayo yamesambaa mpaka katika mji mkuu wa New Delhi, na miji ya Mumbai, Hyderabad na Kolkata.
Sheria mpya inasemaje?
Mabadiliko haya yanakuja kurekebisha sheria ya Uraia iliyopitishwa miaka 64 iliyopita ambayo ilikuwa hairuhusu wahamiaji haramu kupatiwa uraia wa India.
Wahamiaji haramu wanatafsiriwa kwa sheria hiyo kama wageni wanaoingia India bila kuwa na kibali sahihi cha kusafiria au wanaopitiliza muda wao wa kukaa ulioruhusiwa.
Wahamiaji haramu wanaweza kufungwa gerezani au kurudishwa katika nchi zao za asili.
Sheria mpya pia inarekebisha kipengele kinachosema mtu yoyote anatakiwa kuishi India au kufanya kazi katika serikali ya shirikisho kwa takriban miaka 11 kabla ya kuomba uraia.
Sasa, kutakuwa na utofauti kwa utekelezwaji wa sheria hiyo kwa waumini wa dini sita, ambazo ni Hindu, Singasinga, Mabudha, Jain, Parsi na Wakristo kama wanaweza kuthibitisha kuwa ni raia wa Pakistani, Adghanistani au Bangladeshi.
Wao watatakiwa kuishi au kufanya kazi ndani ya India kwa muda wa miaka sita ili kuweza kuomba uraia wa India.
Sheria hiyo pia inasema watu ambao wana kadi ya uraia wa India kutoka nje ya nchi (OCI) - hadhi ya uhamiaji inayomruhusu raia wan je ya India kuishi na kufanya kazi ndani ya India bila vikwazo vyovyote, wanaweza kupoteza hadhi hiyo kama wakiuka sheria za ndani kwa makosa makubwa au madogo.
Kwa nini sheria hii inaleta utata?
Wapinzani wa sheria hiyo wanasema inawatenga na kwenda kinyume na kanuni za katiba. Wanasema imani haiwezi kutumika kama kipimo cha kupata uraia.
Katiba inakataza ubaguzi wa dini kwa raia na inawahakikisha watu wote haki sawa kabla ya sheria na ulinzi wa sheria.
Mwanasheria kutoka mjini Delhi, Gautam Bhatia amesema: ''kwa kuwagawanyisha watu wanaodhaniwa kuwa wahamiaji katika makundi ya waislamu na wale ambao sio waislamu, sheria hii kwa dhahiri inatafuta kuingiza ubaguzi wa dini katika sheria, jambo ambalo ni la kinyume na misingi yetu ya kikatiba.''
Mwanahistoria Mukul Kesavan amesema sheria hiyo ''imesukwa katika lugha inayowalenga wahamiaji lakini lengo lake kuu ni kuwazuia waislamu kupata uraia.''
Wakosoaji wanasema imetengenezwa ikilenga kuwalinda wachache, sheria ingeyajumuisha makundi ya kiislamu ambayo yamepata manyanyaso ndani ya nchi zao kwa mfano Ahmadiya nchini Pakistani na Warohingyas ndani ya Myanmar. (Serikali imeenda mahakama kuu kutaka wakimbizi wa Rohingya waondoke nchini India.)
Akiitetea sheria mpya, kiongozi wa BJP Ram Madhav amesema: ''hakuna nchi yoyote duniani inayokubali wahamiaji haramu.''
''Sheria za uraia wa India zipo kwa yoyote yule anayelalamika. Uraia asili ni chaguo la watu walioomba uraia wa India kwa kufuata sheria. Wahamiaji wengine haramu wote watakuwa wameingia kwa njia za kujipenyeza,'' aliongeza.
Pia akiitetea sheria hiyo mapema mwaka huu, mhariri wa gazeti la Swarajva, R Jagannathan aliandika: ''...kutowaweka wasilamu katika muswada huu inaendana na uhalisia kuwa nchi hizi tatu ni za kiislamu kwasabau katiba zao zinasema hivyo au kwasababu ya matendo ya majeshi ya kiislamu ambao huwataka waumini wa watu wengine kubadilisha dini au kuwanyanyasa."
Ipi historia ya sheria hii?
Muswada wa marekebisho ya sheria ya uraia uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza Julai 2016.
Uliweza kupita katika bunge la chini ambapo BJP ina wawakilishi wengi zaidi, lakini ilishindwa kupitishwa katika bunge la juu, baada ya maandamano na vurugu kutokea kaskazini mashariki mwa India.
Maandamano hayo yalikuwa makubwa zaidi katika jimbo la Assam, ambalo mwezi Agosti wakaazi wake milioni mbili hawakuandikishwa kwenye daftari la raia. Uhamiaji haramu kutoka Bangladeshi umekuwa ni jambo la kuhofiwa ndani ya jimbo hilo.
Sheria ya uraia imekuwa ikihusianishwa na na daftari la uraia, ingawaje ni vitu viwili tofauti.
Mfumo wa kuandikisha uraia (NRC) ni orodha ya watu ambao wanaweza kuthibitisha walikuja katika jimbo hilo kufikia tarehe 24 Machi 1971, siku moja kabla ya nchi jirani ya Bangladeshi kupata uhuru.
Kwa nini usajili wa raia unahusishwa na sheria hii?
Mambo hayo mawili yana uhusiano wa karibu, kwa sababu sheria ya Uraia itasaidia kuwalinda watua ambao sio Waislamu ambao hawamo kwenye daftari la usajili la raia na wanakumbana na hatari ya kurejeshwa kwenye nchi walizotoka ama kufungwa.
Hii ina maaana ya kuwa maelfu ya Wahindu wa Bengali wenye asili ya Bangladeshi ambao hawakuandikishwa kwenye daftari wanaweza kupata uraia na kuendelea kuishi kwenye jimbo la Assam.
Tayari Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Amit Shah amependekeza kusajiliwa kwa raia nchi nzima ili kuhakikisha kuwa "kila aliyejipenyeza (mhamiaji haramu) atambuliwe na afurushwe kutoka India" kufikia mwaka 2024.
"Kama serikali itaendelea na mipango yake ya kusajili raia nchi nzima, basi kuna watu wa makundi mawili watakaoathirika. Kundi la kwanza ni Waislamu ambao sasa wataambiwa kuwa ni wahamiaji haramu, na wengine wote waliobaki pia wataambiwa kuwa ni wahamiaji haramu. Lakini kwa hao wengine tayari kuna sheria inayowalinda kama wataweza kuonesha kuwa nchi yao ya asili ni Afghanistani, Bangladeshi na Pakistani," amesema bw Bhatia.