Uchaguzi wa Algeria: Jinsi wanafunzi wa elimu ya juu wanavyoongoza vuguvugu la mabadiliko

Chanzo cha picha, AFP
Amina Boumaraf, mwenye umri wa miaka 19, na Yanis Cherrou, mwenye umri wa miaka 23, ni wanafunzi lakini wameamua kuchukua mkondo mwengine kwa muda hadi ndoto yao itakapotimia.
Kila wiki tangu Februari wamekuwa wakishiriki maandamano yanayoendelea Algeria.
Maandamano hayo yamesababisha kiongozi wa muda mrefu wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu Aprili mwaka huu, lakini bado wanapinga mchakato wa kumchagua mrithi wake katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Alhamisi hii.
Maandamano hayo yalianza kama kuitikia wito uliotolewa na kundi lisilojulikana katika mtandao wa kijamii wa Facebook.
Februari 22, vuguvugu hilo liliwataka watu kujitokeza mitaani na kushiriki maandamano baada ya kusemekana kwamba Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 atawania uraisi kwa awamu ya tano.

"Hatukujua kitakachofuata na kusema kweli nilikuwa na wasiwasi na vurugu zitakazotokea. Lakini nikaamua kushiriki maandamano hayo licha ya kutojua kile kitakachotokea, Cherrou ameiambia BBC.
Miaka ya 1990, Algeria alikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya makundi ya wanamgambo wa Kiislamu na mara nyingi kumbukumbu za siku hizo zimefanya watu kuwa na uzito wa kushiriki maandamano hayo.
Lakini kuna kitu ambacho kimebadilika: Watu kama Boumaraf na Cherrou walikuwa wadogo na hawakumbuki yaliyotokea enzi hiyo. Wanafunzi hawa wawili wameamua kushiriki maandamano yanayoendelea Algeria.
"Mtandao ulikatishwa wakati wa maandamano ya kwanza yaliyofanyika Februari na hadi kufikia jioni siku hiyo, ndipo tulipoona picha za maandamano yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mji mkuu wa Algiers, ambapo kufanya maandamano kulipigwa marufuku tangu mwaka 2001," amesema Cherrou.
"Na hapo ndipo tulipofahamu kwamba hili ni jambo linalowezekana."
'Wazazi wangu walikuwa na hofu'
Boumaraf anasema kwamba awali, wazazi wake hawakutaka ashiriki maandamano .
"Walikuwa na hofu kwelikweli. Lakini baada ya maandamano ya mwezi Machi, niliwaambia kwamba nitashiriki. Kwangu mimi halikuwa jambo la kuchagua bali wajibu wangu. Nchi yangu ilinihitaji."
Awali, maandamano yalijikita katika suala la Bouteflika kushiriki tena uchaguzi.
Alipojiuzulu, siku ya kufanyika kwa uchaguzi mpya iliwekwa, lakini kama maelfu ya wengine, Cherrou na Boumaraf hawakutaka kukomea hapo.

Pia unaweza kusoma:

"Tunaishi katika enzi za ufisadi na ukosefu wa haki. Raia wanateseka kila siku," amesema Boumaraf, kiongozi wa wanafunzi huko Algiers.
"Kabla ya mapinduzi, tulipokuwa tunataka kuboresha ama kufanya mageuzi, haikuwezekana.
"Kuna watu wenye pesa na watu ambao wanaweza kuwasaidia katika kufanikisha chochote wanachotaka, lakini sisi hatuna mtu tunaye mjua, hatuna chochote."

Wanafunzi wote wawili wanakiri kwamba kushiriki maandamano haya yanayofahamika kama "hirak" neno la kirabu linalomaanisha kukusanya watu pamoja - limechukua muda wao mwingi na kulazimika kuweka kando masomo yao na kila kitu pembeni. Maandamano hufanyika kila Ijumaa.
"Kile ninachopenda ni kwamba raia wamekuwa na mshikamano," anaelezea Boumaraf, anayesomea ujenzi.
"Kuna watu wa kila rika na kutoka nyanja mbalimbali wakati wa maandaamano. Kila wiki tunakuwa na malengo yetu. hilo linanipa matumaini.
"Wakati mwingine huacha ninachofanya na kutazama wengine na hilo linanipa nguvu. Ni jambo linalofanyika kila wiki."
'Mapinduzi ya Tabasamu'
Cherrou, ambaye anasomea teknolojia ya mawasiliano, anamtazamo huohuo kuhusu maandamano hayo licha ya kwamba anaishi takriban kilomita 100 mashariki mwa mji mkuu eneo la Tizi Ouzou.

Chanzo cha picha, EPA
"Awali ghadhabu ilikuwa ya juu, walikuwa wamechoshwa na hali hiyo," amesema.
"Lakini baada ya maandamano ya tatu, hali iligeuka na kuwa na kufurahiwa zaidi, maandamamo hayo yakapewa jina la 'Mapinduzi ya Tabasamu'.
"Ninaweza kusema kwamba najivunia kushiriki maandamano haya. Familia yangu ilipigania uhuru kutoka kwa Ufaransa nami pia ninafuraha kwamba nimepata fursa ya kuleta mabadiliko, na siyo tu kwa jamii yangu bali kwa nchi nzima."

Chanzo cha picha, Reuters
Watu wamekuwa wakikamatwa katika maandamano hayo huku maafisa na wafanyabiashara wanaohusishwa na Bouteflika wakifungwa gerezani, baadhi yao wakiwa ni miongoni mwa viongozi waliopo uongozini ambao wamekuwa wakitawala Algeria tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru wake mwaka 1962.
"Mabadiliko yanayopiganiwa siyo tu dhidi ya rais, yanapinga mfumo mzima uliopo. Tunataka mabadiliko makubwa," amesema Boumaraf.
"Siyo kwamba ninapinga uchaguzi kama inavyooneka lakini ninachopinga ni hatua ya kuandaa uchaguzi katika mazingira kama haya," mama mmoja kijana amesema.
"Tunataka kuwa na mfumo huru wa utekelezaji sheria na uhuru wa kujieleza."
Na kwasababu hii, wengi wanapanga kuendelea kushiriki maandamano wiki hii, hadi siku ya uchaguzi.
'Hii ni dhihaka'
Wagombea wa urais ama wanamuunga mkono Bouteflika ama walikuwa katika serikali yake.
"Kuwa na wagombea wa aina hii, hii ni dhihaka wanayotufanyia. Ni sawa na kuanzisha tena mfumo uliokuwepo," amesema Cherrou.

Chanzo cha picha, AFP
"Hatutaweza kubadilisha mfumo wa sasa ikiwa tutakuwa na rais asiyetuwakilisha, rais ambaye hatakuwa halali," amesema Boumaraf.
"Itakuwa vigumu kweli kweli."
Bwana Cherrou anasema ni kana kwamba maandamano yote ambayo wamekuwa wakifanya tangu Februari yamekuwa kazi bure. Na kibaya zaidi ni kana kwamba hakuna anayeona.
"Inasikitisha kuona dunia imenyamaza kuhusiana na kile kinachoendelea," amesema Cherrou.
"Kwa kipindi cha wiki 42 zilizopita tangu maandamano haya yalipoanza taifa zima limepuuzwa."













