Changamoto za safari ndefu kutoka Tanzania kuelekea Zambia kwa utumizi wa reli ya Tazara

Mtu akitazama treni ya tazara iliokuwa ikisafiri kutoka Tanzania kuelekea Zambia
Maelezo ya picha, Mtu akitazama treni ya tazara iliokuwa ikisafiri kutoka Tanzania kuelekea Zambia

Katika msururu wa barua kutoka kwa waandishi wa Kiafrika, Ismail Elinashe anapanda treni ya Tazara express, akitimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kusafiri kwa kutumia kile kinachojulikana kuwa Uhuru Railway, kwa lugha ya swahili.

Nilianza safari ya kilomita 1,860 iliochukua saa 52 kwa kutumia reli ya Tazara kutoka mji mkuu wa kibiashara nchini Tanzania Dar es salaam kuelekea katika eneo la kapiri Mposhi katikati mwa ukanda wa shaba nchini Zambia.

Ikiwa imejengwa na China miaka ya 70 , umuhimu wa reli hiyo iliokuwa na umaarufu mkubwa baada ya ukoloni umepungua huku Zambia ikiwa na njia nyengine za kuuza madini yake.

Hatahivyo mradi huo ulisaidia pakubwa katika kunoa uhusiano kati ya China na Afrika, huku bara hilo likiwa linaongoza katika ushirikiano wa kibiashara kati yake na China na kwamba taifa hilo ni muwekezaji mkuu huku reli hiyo ikisalia kuwa maarufu miongoni mwa abiria.

Usafiri wa kale

Tangu niliposikia kuhusu reli ya Tazara nikiwa kijana mdogo nilikuwa na ndoto ya siku moja kuitumia katika usafiri wangu.

Kituo cha Tazara Dar es Salaam
Maelezo ya picha, Reli ya Tazara ilijengwa na Wachina miaka ya 70

Ni mojawapo ya safari muhimu sana za reli barani Afrika ikipitia eneo kubwa la mashariki na kusini mwa Afrika.

Kituo chaTazara kilichopo Dar es Salaam kina muundo mzuri wa sanaa ya jamii za miaka ya sabuini ikiwa na ngazi kama zile zinazoingia katika kanisa la Cathedral, madirisha makubwa, eneo la kuketi lililopangwa vizuri, kuta zenye rangi ya kijani inayofifia, mazingira yake yanakurudisha katika usafiri wa treni za kale.

Ndani ya kituo cha reli cha tazara mjini Dar es Salaam
Maelezo ya picha, Kituo cha treni cha Dar es Salaam katika muundo wa kikomyunisti

Nauli ya usafiri itakugharimu dola 45.

Kila behewa limepangwa kulingana na jinsia, huku behewa la daraja la kwanza likiwa na nafasi za watu wanne, behewa la daraja la pili nalo likiwa na nafasi ya watu sita huku lile la daraja la tatu likiwa na viti pekee bila vitanda.

Nilitumia behewa langu na watu wengine wawili katika safari yetu ya siku tatu: Mkulima mmoja kutoka katika ukanda wa shaba ambaye alikuwa ameelekea Tanzania kununua mbegu, mimea na magunia ya mchele kuinunulia familia yake mbali na kijana wa Korea kusini ambaye alikuwa amekamilisha huduma yake ya kijeshi na alikuwa akielekea kutalii kuona maji ya Victoria Falls

Treni hiyo ilijaa abiria na mizigo wakati ilipoondoka mjini Dar es Salaam
Maelezo ya picha, Treni hiyo ilijaa abiria na mizigo wakati ilipoondoka mjini Dar es Salaam

Treni tuliokuwa tukisafiria , niliambiwa, ilikuwa ikiendeshwa na Wazambia na kwamba ilikuwa katika hali nzuri zaidi ya zile zilizokuwa zikisimamiwa na watanzania.

Muundo wake ulikuwa wa mwaka 1976 na kwamba imekuwa katika operesheni tangu wakati huo.

Ilikuwa na maji yaliokuwa yakitoka na kulikuwa na mfereji wa kuoga msalani - likiwa ni shimo lililokuwa katika paa la behewa.

'Ilikuwa ikienda polepole kama baiskeli'

Treni hiyo iliokuwa ikiyumbayumba mara nyengine ilikuwa ikifanya kama itakwama na nilikuwa nikiona mabahewa ya siku za zamani zaidi kandokando ya barabara hiyo ya reli.

Wachuuzi walifanyabiashara wakati treni iliposimama nchini Tanzania
Maelezo ya picha, Wachuuzi walifanyabiashara wakati treni iliposimama nchini Tanzania

Tulipokuwa tukielekea kusini mwa Tanzania , kasi ilishuka hadi kilomita 30 kwa saa- wakati mwengine nikihisi kwamba treni hiyo ilikuwa ikienda mwendo wa baiskeli.

Kila tuliposimama kijiji kizima kilijitokeza kutusalamu. Wanawake huikimbilia treni kuuza ndizi, ovakado , mchele na peremende.

Presentational white space

Na watoto wangeruka juu kwa furaha , wakipunga mikono na kusema karibu.

Walikuwa na matumaini mengi

Katika usiku wangu wa kwanza , nilisikia sauti za fisi kwa mbali na kuona jinsi mbingu ilivyokuwa

Mkahawa wa treni ya Tazara
Maelezo ya picha, Mkahawa huo ulikuwa ukiuza vyakula vya aina moja kuku na wali ama nyama na wali

Kuna kitu kinachovutia kuhusu safari ndefu za treni. Kuchelewa kwake na kasi kunaipa fursa muda wa kujifikiria. Unagundua jinsi umbali wa kitu unavyoweza kuwa.

Katika ulimwengu wa sasa tumezoea kuita Uber kwa urahisi ama hata kusafiri kupitia miji tofauti. Treni hiyo ilikuwa na mkahawa ambapo vyakula vya aina moja vilikuwa vikiuzwa kila siku: Kuku na wali ama nyama na wali. Nilikutana na watu wenye tabia tofauti, nilihisi kama kwamba nipo katika kijiji kimoja ndani ya treni.

Presentational grey line

Kumbukumbu za urafiki kati ya Afrika na China.

Treni ya Tazara ikisafiri kutoka tanzania kuelekea Zambia ikitoka katika handaki moja

Tazara ilijengwa ili kupunguza utumiaji zaidi wa Zambia kusafirisha shaba yake kupitia Zimbabwe na Afrika kusini iliokuwa ikikabiliwa na ubaguzi wa rangi.

Shaba ni asilimia 70 ya bidhaa zote za Zambia zinazouzwa katika mataifa ya kigeni na ndio uti wa mgongo wa taifa la Zambia.

Kenneth Kaunda ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa taifa la Zambia alitafuta usaidizi kutoka mataifa ya magharibi lakini hakupokea usaidizi wa haja wa kifedha.

Hivyobasi akiwa pamoja na Mwalimu Julius Nyerere badala yake waliomba usaidizi kutoka kwa China.

Wakati Treni hiyo ilipoanzishwa ulikuwa uwekezaji mkubwa wa kigeni kuwahi kufanywa na China. Uliipatia Zambia na Tanzania mkopo usio na riba wa dola milioni 500 kulipwa katika kipindi cha miaka 30.

Mwaka 1970 kazi ya ujenzi wa reli hiyo ilianza mjini Dar es Salaam huku wafanyakazi wengi wa China wakijiunga na wenzao wa Afrika kufanya kazi pamoja , wakichimba mahandaki, kujenga madaraja, na kuweka reli katika maeneo magumu yalio na milima kusini mwa Tanzania.

Kuna saini ya Tazara katika kituo cha reli cha Dar es Salaam ; ikionyesha urafiki uliopo kati ya China na Afrika.

Walipokamilisha ujenzi huo 1976, China iliwakabidhi vifaa, treni na kuendesha reli hiyo raia wa Tanzania na Zambia - lakini haikupata abiria wengi ama kuongezeka kwa kasi.

China inasalia kuwa mshirika muhimu katika uendeshaji wa reli hiyo kwa kuwa inaona reli hiyo kuwa uhusiano muhimu kati ya China na Afrika.

Kitu muhimu ilikuwa kukutana na mkulima mmoja raia wa Tanzania katika baa ya treni hiyo , ambaye alikuwa akirudi shambani kwake.

Alinionyesha picha za pacha wake , mvulana na msichana , na baada ya kunywa pombe kadhaa alikiri kwamba ilimchukua mkewe miaka minane kushika ujauzito.

Ilikuwa wazi kwamba kilikuwa kitu ambacho alikuwa akikionea aibu kubwa - lakini usiku huo wakati treni hiyo ilipokuwa ikiendelea na safari yake katikati ya milima mirefu alihisi anaweza kuongea nami.

Usafiri wa treni unaonekana unaweza kuuondoa vikwazo kati ya watu na kuwaunganisha.

Ramani ya Tanzania na Zambia

Pia nilikutana na raia mmoja wa Swazi aliyezaliwa na mama raia wa Ethiopia na baba wa Kichina ambaye alikuwa amehudumia ujana wake akikulia katika taifa la kikomyunisti la Bulgaria 1980.

Kwa sasa anaendesha malori ambayo husafirisha sukari kutoka Swaziland kupitia Zambia hadi nchini Tanzania na Kusini mwa Sudan.

Presentational grey line

Baada ya safari ya saa 28 nchini Tanzania hatimaye tuliwasili katika mji wa mpakani wa Tunduma usiku, ambapo afisa wa uhaimiaji wa Tanzania aliingia ndani ya treni na kutupigia chapa pasipoti zetu.

Baadaye upande wa Zambia pia ulifanya vivyo hivyo kabla ya wabadilishanaji sarufi kujitokeza. Unaweza kudhania kwamba tulikua tayari tunataka kubadilisha fedha za Tanzania kuwa kwacha za Zambia .

Lugha yao pia ilibadilika kutoka kiswahili hadi Bemba huku ardhi ikiwa tambarare na kavu.

Barabara ya reli ya Tazara
Maelezo ya picha, Ni vigumu kukubali mwendo mrefu ambao treni hiyo husafiri katika treni hiyo ya Tazara

Kila kituo ambacho tulikuwa tukisimama tulikuwa tukiwaona wauzaji wachache wa matunda: Tanzania ni taifa la kilimo huku Zambia likiwa taifa la uchimbaji madini.

Baadaya ya saa 24 tuliwasili katika eneo la Kapiri Mposhi muda wa usiku.

Nilipata uzoefu wa usafiri wa kutumia barabara barani Afrika baada ya kuendesha gari hadi katika mji mkuu wa Zambia Lusaka.

Gari hilo lenye viti saba lililokuwa na abiria 12 na mizigo yao lilikuwa likiyapita malori makubwa yaliobeba shaba katika barabara hiyo nyembamba tukio lenye hatari kubwa katika maisha ya kisasa.