Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Amber Guyger: Polisi aliyemuua jirani yake akutwa na hatia
Afisa wa polisi nchini Marekani ambaye alimpiga risasi na kumuua jirani yake ndani ya nyumba yake amekutwa na hatia ya mauaji.
Bi Amber Guyger, 31, amejitetea kuwa alimuua Botham Jean, 26, baada ya kudhani, kimakosa, alivamia nyumba yake.
Hukumu imetolewa baada ya kesi kunguruma kwa siku saba ambapo Bi Guyger alikiri kuwa: "Nilimpiga risasi mtu asiye na hatia."
Kutokana na hukumu hiyo, sasa anakabiliwa na uwezekano wa kutupwa maisha jela.
Ndugu wa marehemu walilipuka kwa furaha baada ya hukumu kutolewa, lakini alijibwaga kwenye meza na kuangua kilio.
Marehemu alikuwa akila aiskrimu wakati akishambuliwa
Mawakili wa Bi Guyger walimtetea mteja wao kuwa alikuwa amepumbazwa na ujumbe wa simu wa mapenzi kutoka kwa polisi mwenzake na alikuwa ametoka kazini ambapo alihudumu kwa zaidi ya saa 14 wakati alipofanya kile walichokiita "mlolongo wa makosa" usikuwa Septemba 8, 2018.
Waendesha mashtaka wanamtuhumu kwa kuingia katika nyumba ya Jean kwa "staili ya kikomando" na kumshambulia kwa risasi wakati akiwa kwenye sofa lake akila aiskrimu.
Waendesha mashtaka pia wamedai utetezi wake ni "takataka" na kudai matendo yake "hayakuwa ya makosa".
Moja ya askari waliochunguza tukio hilo amedai kuwa ni jambo la kawaida kwa wakazi wa jengo lilotokea shambulio hilo kuingia kwenye nyumba ya jirani wakidhani ni zao kutokana na kufanana kwa roshani.
Guyger alijitetea kuwa alikuta mlango ukiwa upo wazi kidogo wakati alipofungua kitasa cha mlango ambao alidhani ni wake.
Waendesha mashtaka wamedai kuwa afisa huyo alishindwa kujua tofauti za wazi ikiwemo pazia jekundu mlangoni kwa Jean.
'Upepo unabadilika'
"Huu ni ushindi mkubwa kwa watu weusi nchini Marekani," amesema mwanasheria wa kutetea haki za watu weusi Lee Merritt baada ya kusomwa hukumu hiyo.
"Hii ni dalili kuwa upepo unabadilika hapa. Polisi sasa watachukuliwa hatua kwa matendo yao, na tunaamini hilo litaanza kufanya polisi wabadilike tabia duniani kote."
Shambulio hilo lilisababisha maandamano ya vurugu kutokana na wakaazi wa eneo hilo kuamini kuwa Bi Guyger hatachukuliwa hatua yoyote.
Awali alikamatwa siku kadhaa baada ya mauaji, na kushtakiwa kwa kuua bila kukusudia kabla ya kuachiliwa siku hiyo hiyo.
Baada ya wiki za machafuko, alikamatwa tena na kushtakiwa kwa mauaji.
Botham Jean, alikuwa akifanya kazi kama mhasibu katika kampuni maarufu ya Pricewaterhouse Cooper wakati akiuawa.
Meya wa zamani wa Dallas Mike Rawlings alikuwa ni moja kati ya wale ambao walimsifu baada kuuawa kwa kumuita "mtu mwema wa mfano."