Shirika la Afya Duniani lathibitisha Urusi imepunguza unywaji wa pombe kwa 43%

Matumizi ya pombe nchini Urusi yamepungua kwa 43% kutoka mwaka 2003 mpaka 2016, kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO).

Matokeo haya yanakuja baada ya taifa hilo kuchukua hatua kadhaa za kuwasukuma watu kubadili mifumo yao ya maisha na kuishi kwa kuzingatia afya zao.

Shirika la WHO limehusisha matumizi ya pombe na ongezeko la umri wa kuishi .

Awali Urusi ilifahamika kama nchi inayoongoza katika matumizi ya unywaji wa pombe duniani.

"Ni kwa muda mrefu matumizi ya pombe kwa kiwango kikubwa yamekuwa yakitajwa kuwa sababu ya vifo vingi vijana ambao ndio nguvu kazi wa taifa hilo la Urusi,"ripoti zinasema.

Lakini kuanzia mwaka 2003 mpaka 2018, matumizi ya pombe imepungua halikadhalika idadi ya vifo pia imepungua, kutokana na matokeo hayo chanya kutokea ndio sababu ya kuhusisha sababu ya vifo na pombe.

Mwaka 2018, umri wa kuishi nchini Urusi ulivunja rekodi kihistoria na kuwa miaka 68 wanaume na wanawake 78.

Hatua za kukabiliana na matumizi ya pombe zilianzishwa na rais wa zamani Dmitry Medvedev, ambaye alipiga marufuku matangazo ya pombe, aliongeza kodi katika pombe na kupiga marufuku mauzo ya pombe kutofanyika katika muda fulani .

Makatazo ya pombe nchini Urusi ni miongoni mwa mambo ambayo yameleta mabadiliko makubwa nchini humo katika miaka ya hivi karibuni .

Mjini Moscow, maduka madogo (vioski) ambayo yalikuwa yanajaa pombe kali za Vodka na bia yamefungwa muda mrefu au yanauza samaki sasa.

Sasa mtu unaweza kununua pombe dukani mpaka saa tano usiku tu tofauti na zamani.

Ni marufuku kunywa bia barabarani na endapo ukikamatwa na chupa ya bia mtaani, polisi wanakupiga faini .

Pamoja na marufuku hizo, elimu ya kuishi kwa kuzingatia afya imekuwa kwa kiwango kikubwa.

Warusi wengi wameanza kuzingatia kanuni bora za mfumo wa maisha kiafya kama ilivyo katika mataifa mengine ya ulaya na Marekani.

Lakini vilevile utajiri umehusishwa na afya.

Kwa sababu katikae jumuiya nyingi za watu maskini, bado wanakunywa kwa wingi pombe za asili ambazo ni bei nafuu.