Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Pompeo aishutumu Democrats kwa unyanyasaji wa wafanyakazi wake

Waziri wa mambo ya kigeni nchini Marekani, Mike Pompeo amekishutumu chama cha Democrats kwa kuwanyanyasa wafanyakazi wake, na kuwakingia kifua dhidi ya uchunguzi unaomlenga rais Donald Trump.

Bwana Pompeo ameilaumu kamati ya bunge inayoongozwa na Democrats kwamba inajaribu kutumia nguvu yake kuwanyanyasa wafanyakazi wake.

Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa mombi ya maofisa wake watano kufika kwenye kamati maalum ya bunge ya uchunguzi huo "hayatawezekana".

Wajumbe wa kamati maalumu ya bunge la Congress wanafuatilia shutuma dhidi ya rais Trump kumshinikiza rais wa Ukraine kufanya uchunguzi wa kashfa za rushwa dhidi ya Joe Biden ambaye ni mpinzani wake kisiasa

Lakini kwa upande wake Steve Cohen ambaye ni mmoja wa kamati ya wanasheria ya bunge amesisitiza kuwa madai hayo bwana Pompeo si ya kweli.

"Wao ndio timu inayonyanyasa na kufanya ukatili, Hatutaki kuona watu wakishuhudia matumizi mabaya ya madaraka ambayo rais anakuwa mmoja wao na kuhatarisha usalama wa taifa".

Uchunguzi huo umefikia wapi?

Siku ya Jumatatu ilibainika kuwa bwana Pompeo alikuwepo wakati Trump akifanya mawasiliano hayo ya simu na rais wa Ukraine.

Mambo mengine ambayo yamejiri kutokea hapo ni:

  • Rais Trump aliwataka maofisa wa Australia kumsaidia katika uchunguzi unaoendelea ili kupata chanzo cha uchunguzi huo na tayari, Australia imethibitisha.
  • Mwanasheria mkuu wa Marekani, William Barr ameripotiwa kufanya mazungumzo ya faragha na maafisa wa ujasusi wa Italia na Uingereza kuomba usaidizi wa katika uchunguzi wa ripoti ya mchunguzi maalum Robert Mueller.
  • Maafisa wawili pamoja na balozi wa zamani wa Marekani nchini Ukraine Marie Yovanovitch, amethiitisha kutoa ushaidi kwa Congress.
  • Wakili binafsi wa rais Trump, Rudy Giuliani, ameitwa kuwasilisha nakala muhimu kuhusu Ukraine na kamati tatu za bunge.
  • Seneta wa Republican Chuck Grassley - ambaye yuko nafasi ya tatu kuchukua wadhifa wa rais kama Trump ataondolewa madarakani amewatetea watu waliotoa taarifa hizo na kutaka walindwe.
  • Kufuatia mazungumzo ya simu kati ya rais Trump na kiongozi wa Ukraini bwana Zelensky ameiambia Reuters: "Siwezi kushawishika."

Bwana Pompeo alisema kuwa maombi ya mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje, Eliot Engel itaeleweka tu kama jaribio la unyanyasaji katika maeneo ya kazi katika ofisi yake.

"Siwezi kuvumilia mambo ya namna hiyo na nitafanya kila mbinu kuzuia unyanyasaji katika eneo la kazi na kuweka wazi jaribio lolote lililolenga kuharibu sifa ya wataalamu ambao ninajivunia kuwaongoza".

Democrats imewataka maofisa watano wa idara hiyo pamoja na balozi wa zamani wa Marekani nchini Ukraine na rais Trump kuja na majibu sahihi juu ya jambo hilo ndani ya mwezi huu.

Bwana Pompeo alisema kuwa maombi ya bwana Engel yaliibua maswali mengi kuhusu ushahidi wa mamlaka na kamati yake na kumshutumu pia kwa kutoleta mashaidi kwa wakati .

Athari za uchunguzi dhidi ya Trump

Uhalifu anaoshutumiwa nao Trump unaweza kumuondoa rais madarakani, na unapitia hatua mbili za mchakato wa kisiasa.

Kama kura za wawakilishi hazitatosha, basi bunge la seneti litalazimika kusimamia kesi hiyo.

Kura ya seneti inahitaji walau wingi wa theluthi mbili ya wingi - na inaweza kushindwa kwa sababuchama cha Trump kina maseneta wengi zaidi.

Ni marais wawili tu katika historia ya Marekani ambao ni Bill Clinton and Andrew Johnson ambao walikabiliana na kesi ya namna hiyo na hakuna kati yao ambaye alishtakiwa au kuondolewa madarakani.

Rais Nixon alijiondoa madarakani kabla ya kung'olewa na bunge.

Mazungumzo baina ya Trump na Zelensky yalikuwaje?

Kwa mujibu wa mukhtasari uliotolewa jana na Ikulu ya White House, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mwana wa Joe Biden, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Bw Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

"Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo," Trump ananukuliwa akisem kwenye mazungumzo hayo na kuongeza: "Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

"Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo...ni jambo baya sana kwangu."

Zelensky anaripotiwa kujibu: "Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

"Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana."

Akimshukuru Trump, bw Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.