Waziri mkuu wa jimbo India atangaza mpango wa kuwa na wizara ya ng’ombe

Mwumini wa dini ya Kihindu akimwabudu ng'ombe wakati wa sherehe ya Krishna Janmashtami jijini Hyderabad, mnamo Septemba 3, 2018.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waumini wa dini ya Kihindu huamini ng'ombe ni mnyama mtakatifu

Serikali ya jimbo moja katikati mwa India imetangaza mpango wa kuanzisha wizara ya masuala ya ng'ombe.

Waziri mkuu wa jimbo la Madhya Pradesh Shivraj Singh Chouhan amesema hatua hiyo itachangia kuongezwa kwa fedha za kusaidia uhifadhi wa ng'ombe.

Taarifa zinasema Bw Chouhan, ambaye ni wa chama cha BJP, amechukua hatua hiyo kama moja ya njia za kujaribu kumzidi mgombea wa chama cha upinzani cha Congress kila mmoja akijaribu kuwavutia wapiga kura wanaowathamini sana ng'ombe.

Alitoa tangazo hilo siku chache baada ya kiongozi wa chama cha Congress katika jimbo hilo Kamal Nath kuahidi kuanzisha makao ya kutoa hifadhi kwa ng'ombe iwapo chama chake kitashinda uchaguzi.

Amesema amesikitishwa sana na vifo vya ng'ombe ambao mara kwa mara hugongwa na magari wakivuka barabara katika jimbo hilo.

Ramu na mmiliki wake Selvarani Kanagarasu aliyekataa kuolewa ili kumfuga ngombe huyo
Maelezo ya picha, Selvarani Kanagarasu alikataa kuolewa ili kumfuga ngombe huyu

Chama cha BJP kimemshutumu mgombea huyo na kusema imekuwa ni sera ya chama cha Congress kutoa ardhi ya malisho kwa maskwota na hivyo kupunguza malisho ya ng'ombe.

Jimbo hilo limekuwa na bodi ya kuangazia maslahi ya ng'ombe inayofahamika kama Gau Samvardhan lakini Chouhan anaamini kwamba wizara ndiyo itakayofaa zaidi kutetea maslahi ya ng'ombe.

Rais wa chama cha BJP Amit Shah Kapashera Dwarka link road on June 4, 2018 in New Delhi, India.

Chanzo cha picha, Hindustan Times/Getty Images

"Bodi hii inakumbwa na matatizo ya kifedha lakini kukiwa na wizara tatizo hilo halitakuwepo tena," amenukuliwa na gazeti la Hindustan Times.

Ngombe hutambulika kuwa mnyama mtakatifu na waumini wa dini ya Kihindu walio wengi nchini India na kwamba mauaji ya ngombe ni haramu katika majimbo mengi ya India.

Kula nyama yake ni mwiko.