Msitu wa Mau: Sababu zinazofanya eneo hilo kuzozaniwa Kenya

Hezron Mogambi

Siasa za msitu wa Mau nchini Kenya zimejitokeza tena. Kwa zaidi ya miaka 20, Serikali mbali tofaiti za Kenya zimeshindwa kulisuluhisha swala hili. Sababu kuu zimekuwa za kisiasa. Kwa sasa, Serikali inapanga kuzifurusha familia 12,000 zinazoishi kwenye msitu huu muhimu kinyume cha sheria kwenye hekta 146,000 za msitu wa Mau.

Hata ingawa ni bayana kwa kila mmoja nchini Kenya kuwa eneo la Mau ni sehemu muhimu kwa uhifadhi wa mazingira nchini Kenya kwa kuwa ni sehemu hii ni nguzo muhimu katika kupatikana kwa maji kote Afrika Mashariki, haijabainika ni kwa nini viongozi wa Kenya hajalipata suluhu swala hili. Ukweli kwamba zaidi ya familia takribani 40,000 zinaishi eneo hili la Mau na zaidi ya familia nyingine elfu 20,000 katika eneo la Maasai Mau ambalo linasimamiwa na Serikali ya Kaunti ya Narok inaonyesha jinsi eneo hili lilivyo muhimu.

Sehemu kuu ya Mau inapatikana kilomita 170 Kaskazini-magharibi mwa Nairobi, ikiwa ndio msitu mkubwa zaidi ambao umesalia wenye miti ya kiasili. Msitu wa Mau una ukubwa hekta 400,000 na ndio chechemi kuwba zaidi ya maji ikipakana na kaunti ya Kericho upande wa magharibi, Narok upande wa kusini Nakuru upande wa kaskazini na Bomet upande wa kusini-magharibi.Msitu huu umegawanywa katika sehemu saba: Mau Kusini-Magharibi (Tinet), Mau Mashariki, Oldonyo Purro, Transmara, Maasai Mau, Mau Magharibi na Mau Kusini.

Kwa miaka mingi, mazingira ya msitu wa Mau nchini Kenya yamekuwa chemi chemi ya maji na nguzo muhimu kwa nchi ya Kenya yakihifadhi maji nyakati za mvua na kusaidia mamilioni ya Wakenya nyakati za ukame. Takribani watu milioni 10—bila kutaja wanyama wa pori wa kila aina—hutegemea mito ambayo chanzo chake ni katika msitu huu. Hata hivyo, kutokana na shughuli za binadamu kama vile ukataji miti, kilimo, na makazi eneo lililokuwa na msitu limepungua kwa zaidi ya robo tatu sasa, jambo ambalo limeharibu msitu wenyewe kama chanzo cha maji kwa maeneo ya karibu na mbali.

Historia ya msitu wa Mau inaonyesha kuwa kuwa kufanywa sehemu hii sehemu ya makazi ni shughuli iliyoanza miaka ya 1930 wakati serikali ya mkoloni nchini Kenya ilipokata miti katika sehmy yam situ huu ili kupanda miti ya kizungu. Ni katika wakati huu, watengenezaji mbao walipopata leseni zilizowaruhusu kukata miti kwa minajili ya kutengeneza mbao na mfumo wa shamba kuanzishwa kwenye msitu wa Mau. Mfumo huu mwanzoni uliwaruhusu watu wachache kuwalisha wanyama kwenye msitu, kukata kuni na ukulima kwa kiasi kidogo kwenye msitu chini ya usimamizi wa askari wa misitu.

Baadaye, hali hii ilibadilika na kuanza kuruhusu kwepo kwa mashamba makubwa kwenye msitu wa Mau kwa sababu idara ya misitu wakati huo ilitaka kupunguza gharama ya kulinda na kushughulikia maeneo haya. Hata hivyo, wakati huo, mfumo huu ulionekana kuwasaidia wakazi na chakula cha kutosha kwa wale wakazi ambao hawakuwa na mashamba yao, jambo lililowafanya wakazi waliokuwa katika maeneo ya karibu kuingia kwenye msitu wa Mau na kuyafanya makazi yao, hasa maeneo ambapo miti ilikuwa imekatwa na serikali.Kwa sababu ya hali hii, serikali za Kenya zilizofuata baadaye zilichukua sehemu kubwa yam situ wa Mau na kuwapa wale walioitwa "wasiokuwa na mashamba.

Wengi wa wale walioitwa "wasiokuwa na mashamba" walikuwa na nyadhifa kubwa katika serikali ama washirika wao katika serikali za awali nay a sasa nchini Kenya. Baada ya tukio hili, baadhi ya wanasiasa waliopewa sehemu kubwa za ardhi katika msitu wa Mau walihodhi mashamba yao huku wengine wakiyauza kwa watu wengine. Hivi ndivyo mzozo wa sasa kuhusu Msitu wa Mau ulivyoanza kwa kuyachanganya masuala ya uhifadhai wa misitu na siasa yote kwa pamoja.

Kufuatia ukame ulioikumba Kenya kwa muda mrefu miaka ya 2008-2009, serikali ilichukua hatua ya kuwafukuza wakazi "wasio halali" kutoka kwenye msitu wa Mau jambo ambalo limekuwa likileta utata hadi leo.

Sura ambayo imekuwa ikijitokeza katika mzozo kuhusu msitu wa Mau ni tofauti za kisiasa zenye misingi ya kikabila. Sehemu hii ina wakazi wa kabila la Wakalenjin kwa upand e mmoja na Wamaasai kwa upande mwingine. Hata hivyo, ni dhahiri kuwa iwapo siasa na ukabila zinginewekwa kando, uhifadhi wa mazingira na msitu wa Mau ungechukua nafasi kubwa hkwa sababu familia 30,000 wanautegemea msitu huu.

Katika hatua ya kuwafurusha wale wanaokaa kwenye msitu huu kinyume cha sheria, serikali ya Kenya inapanga kuwaondoa na kuchukua hekta 23,000 kwa minajili ya upanzi wa miti. Wanasiasa kutoka Kaunti za Narok wanaunga mkono suala la kuwafurusha wale wanaoishi kwenye msitu huu huku wanasiasa wa upande wa Bomet na Kericho wakipinga hatua ya serikali ya kuwafurusha watu wanaoishi kwenye msitu wa Mau.

Aidha, kuna swala lisilopata jibu la iwapo kuwapa mashamba na kuwalipa fidia baadhi ya wakazi ili wondoke katika shemu hii ni sehemu ya kupata suluhu kwa mzozo wa msitu wa Mau. Hatua hii inakataliwa na wahifadhi mazingira na baadhi ya Wakenya katika misingi kwamba katika sehemu nyingine za nchi ya Kenya ambapo watu wamepewa mashamba kwa mtindo huu, kumechipuka matatizo makubwa zaidi.

Pia, kuna tatizo kubwa kuhusiana na msitu huu kwa kuwa wengi wa wale wanaoishi kwenye msitu wa Mau kwa sasa ni wa kabila la Wakalenjin lakini wale waliofurushwa kutoka humu miaka ya awali ni pamoja na Wasabaot, Wamarakwet na Wakikuyu. Kwa jinsi hii basi, kuwalipa wale wanaoishi kwenye msitu wa Mau kwa sasa na kukosa kuwalipa wale waliofurushwa hapo awali litaonekana tukio la kulipendelea kundi moja na kuyabagua mengine.

Katika suala hili, makabila mengine kama vile Ogiek yamekuwa yakijihisi kukosewa kwa sababu tofauti na wengine, hawana vyeti vya mashamba, na hivyo hawawezi kulipwa fidia. Itakumbukwa kuwa watu wa jamii ya Ogiek limekuwa likiishi kwenye msitu kama makazi yao tangu jadi. Tayari jamii ya Ogiek imesema kuwa itarudi katika mahakama ya Afrika kuhusu Haki za Kibinadamu kudai haki yake. Msemaji wao, Joseph Towett, alieleza kuwa kufurushwa kwao kunakwenda kinyume cha agizo la mahakama hiyo ambapo mahakama iliagiza kuwa wale waliokuwa wamefurushwa hapo awali walipwe fidia.

Bila shaka, katika suala la msitu wa Mau nchini Kenya, kuna haja ya kushughulikia kati ya hali ya wakaazi walio kwenye msitu na uhifadhi wa mazingira. Hali ya kuichumi na maiahs ya wale wote wanaoishi kwenye msitu huu inafaa kushughulikiwa kabla ya kufurushwa na mpango mbadala kufikiriwa na serikali ya Kenya.

Jinsi atakavyolishughulikia swala hili ni jambo linalosubiriwa na Wakenya wengi kwa kuwa msitu wa Mau ni muhimu sana nchini Kenya. Kuna haja ya kubuni mfumo utakaohakikisha kuwa msitu wa Mau unahifadhiwa na kurejesha hali yake ya awali. Hali hii itahakikisha kuwa vizazi vya kesho vitafaidi kwa hali na mali.

Prof. Mogambi, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi: hmogambi @ yahoo.co.uk