Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Donald Tsang: Kiongozi wa zamani Hong Kong afungwa jela
Kiongozi wa zamani wa Hong Kong Donald Tsang amehukumiwa kufungwa jela miezi 20 kwa kutumia vibaya mamlaka yake.
Tsang aliongoza Hong Kong kati ya 2005 na 2012 na ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi nchini humo kuwahi kushtakiwa kutokana na tuhuma za ulaji rushwa.
Alipatikana na hatia wiki iliyopita katika kesi iliyohusu nyumba ya kifahari nchini China.
Wakati wa kumhukumu, Jaji Andrew Chan alisema: "Daima, sijawahi katika kipindi changu kama jaji, kushuhudia mtu akishuka chini hivi kutoka kwenye upeo wa mamlaka."
Viongozi kadha wakuu wa zamani Hong Kong walikuwa wameandika barua kwa mahakama kumtetea Tsang.
Tsang aliondolewa makosa wiki iliyopita kuhusu shtaka la pili la kutumia vibaya mamlaka.
Jopo la waamuzi wa mahakama lilikosa kuafikiana kuhusu shtaka la tatu la kukubali manufaa kinyume cha sheria.
Baada ya kuhukumiwa, Tsang alitolewa kortini akiwa amefungwa pingu na kupelekwa hadi hospitalini ambapo amekuwa tangu Jumatatu baada ya kupatwa na maumivu ya kifua.