Fahari ya Ethiopia - Kilichohitajika kujenga bwawa kubwa zaidi la umeme barani Afrika

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Kalkidan Yibeltal
- Nafasi, BBC News Addis Ababa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Ukubwa wa eneo la jengo kwanza ulikuwa mkubwa sana kwa mhandisi mchanga wa mitambo nchini Ethiopia.
Mamia walikuwa tayari wakichimba misingi katika mazingira magumu katika eneo ambalo sasa ni bwawa kubwa zaidi la umeme wa maji barani Afrika, linalozunguka Mto Blue Nile.
Moges Yeshiwas alikuwa na umri wa miaka 27 alipowasili katika eneo hilo lililo mbali la magharibi mwa Ethiopia mwaka wa 2012, akiwa na shauku ya kupata uzoefu muhimu katika taaluma yake.
Kukamilika kwa mradi huo kutabadilisha taifa lake, lakini pia kulibadilisha maisha yake.
Siku ya Jumanne, Waziri Mkuu Abiy Ahmed anatazamiwa kuzindua rasmi Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (Gerd), ambalo litasaidia kusambaza umeme nchini humo pamoja na kutoa umeme katika eneo hilo.
Ukuta wa bwawa hilo una urefu wa 1.78km (maili 1.1)mbali na urefu wa mita 145 (futi 475) - zilizojengwa kwa mita za ujazo milioni 11 za saruji. Imeunda hifadhi kubwa, inayoitwa Ziwa Nigat, lenya maana ya alfajiri katika lugha ya Kiamhari.
Ujenzi wa bwawa kwenye mkondo wa mto Nile, ambao hutoa maji mengi ya mto huo mkubwa, ulikuwa na utata na nchi za chini ya mto huo.
Mvutano wa kidiplomasia na Misri uliongezeka na kulikuwa na mazungumzo ya migogoro.
Lakini kwa Ethiopia bwala la Gerd limekuwa ishara ya fahari ya taifa na, kwa maoni ya Abiy, ameiweka nchi yake imara kwenye jukwaa la dunia.
I came seeking employment, but somewhere along the way, it stopped feeling like just a job"
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika ngazi ya kibinafsi, Bw Moges, ambaye sasa ana umri wa miaka 40, pia "alijivunia kuwa sehemu yake".
"Kutazama maendeleo ya bwawa siku baada ya siku kuliniridhisha sana. Nilikuja kutafuta kazi, lakini mahali fulani njiani, iliacha kuhisi kama kazi tu. Nilikua nikihusishwa na mradi huo, nikihangaikia mustakabali wake kana kwamba ulikuwa wangu."
Kulikuwa na changamoto.
"Kutengana kwa muda mrefu na familia ilikuwa ngumu," aliambia BBC. Bw Moges angeweza tu kwenda nyumbani kwao Bahir Dar - ilio umbali wa kilomita 400 kwa kutumia gari - mara mbili kwa mwaka.
Alihisi umbali wa eneo la bwawa na wakati fulani joto kali la kufikia nyuzi 45C - pia lilizua masuala. Zaidi ya hayo, Muda wa kufanya kazi pia ulikuwa mrefu .
"Zamu zetu zilianza saa saba asubuhi hadi saa saba mchana, tukiwa na mapumziko ya saa moja tu kwa chakula cha mchana. Kisha tukawakabidhi wafanyakazi wa usiku, kwa sababu kazi ilibidi iendelee saa nzima," Bw Moges alisema.
Kazi yake ilikuwa kuhakikisha kazi ya ujenzi ilikuwa nzuri kimuundo na viwango vya ujenzi vilidumishwa.
Mradi wa Gerd ulikuwa nguvu adimu ya kuunganisha kwani nchi hiyo ya Pembe ya Afrika imekumbwa na ghasia za kisiasa na mizozo ya kikabila katika muongo mmoja uliopita.
Wakati baadhi, kama mhandisi, walifanya kazi moja kwa moja kwenye bwawa, mamilioni ya Waethiopia wengine walikuwa, kihalisi, wamewekeza ndani yake.
Watu wa tabaka mbalimbali walichangia ujenzi wa bwawa hilo kupitia michango na ununuzi wa dhamana zilizotolewa na serikali.
Licha ya madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Washington ilisaidia kifedha ujenzi wa bwawa hilo, Addis Ababa inashikilia kuwa lilifadhiliwa kikamilifu na raia wa Ethiopia.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kampeni kadhaa za uchangishaji fedha zilifanyika ambazo ziliwashuhudia wananchi wakichangia mara nyingi.
Muuguzi wa kliniki Kiros Asfaw alikuwa mmoja wao
Licha ya kuwa anatoka eneo la Tigray, ambalo lilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili, alichangia alipoweza katika ujenzi wa bwawa hilo tangu mipango hiyo ilipotangazwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2011.
Anasema alinunua bondi za serikali zaidi ya mara 100 - ingawa alilazimika kusitisha ununuzi wake wakati wa vita, wakati huduma za kimsingi, ikiwa ni pamoja na benki, zilisitishwa huko Tigray.
Motisha ya Bw Kiros ilitokana na matamshi yaliyotolewa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia hayati Meles Zenawi, ambaye alisimamia mwanzo wa mradi huo, kwamba Waethiopia wote lazima waungane kuunga mkono bwawa hilo.
"Nilijiahidi kufanya kila niwezalo kusaidia kumaliza hadi mwisho," baba wa watoto watano aliambia BBC.
Sasa, mitambo yote ikifanya kazi, mawazo yanageuka na kuwa ni tofauti gani nguvu hizi za umeme zinaweza kuleta Ethiopia.
Kwa uwezo kamili linapaswa kuzalisha MW 5,100 za umeme - zaidi ya mara mbili ya kile ambacho nchi inazalisha bila bwawa na kutosha kusambaza umeme kwa makumi ya mamilioni ya nyumba zaidi nchini.
Hilo hata hivyo linategemea miundombinu iliyopo ili kubeba nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Waziri wa Maji na Nishati Habtamu Ifeta aliambia BBC kuwa karibu nusu ya watu milioni 135 nchini humo hawana umeme.
"Hilo ndilo tunalotaka kupunguza sasa katika miaka mitano ijayo. Nia yetu ni kufikia 2030 angalau asilimia 90 ya taifa letu lipate huduma ya umeme," alisema.

Chanzo cha picha, Amensisa Negera / BBC
Getenesh Gabiso mwenye umri wa miaka thelathini na tano, ambaye anaishi Alamura, kijiji cha wakulima nje kidogo ya Hawassa, jiji kuu kusini mwa Ethiopia, ni mmoja wa wale wanaofikiria tofauti ambayo inaweza kuleta.
Maisha yake yanaakisi yale ya mamilioni ya wengine katika maeneo ya mashambani ya Ethiopia.
Licha ya kibanda chake kidogo, kilichoezekwa kwa nyasi kuwa kilomita 10 tu kutoka Hawassa, Bi Getenesh, mume wake na watoto wake watatu hawana umeme.
Kwa kupikia yeye hutumia kuni zinazotoka karibu na shamba lao.
Na kwa mwanga hutumia taa zinazotumia mafuta ya taa. Mumewe, Germesa Galcha anajali afya ya familia yake.
"[Getenesh] alikuwa na macho makubwa na mazuri. Lakini miaka yote hii ya moshi unayaharibu," alisema.
"Nina wasiwasi ningefanya nini ikiwa moshi huo ungewaingia watoto na kuwadhuru ."
Kwa Bi Getenesh, ambaye, giza linapoingia, wakati mwingine hutegemea mwanga hafifu kutoka kwa simu ya mkononi ya mumewe, kuona tu usiku ndiko anakoota.
"Nataka kuona mwanga katika nyumba yangu. Bidhaa nyingine zote za umeme hazijalishi kwa sasa. Mwangaza tu jioni ndio ninachotaka," anaiambia BBC.
Wanatazamia tofauti ambayo nguvu kutoka kwa bwawa la Gerd inaweza kuleta. Lakini waziri wa serikali, Habtamu, anakubali kwamba mengi zaidi yanahitajika kufanywa kupanua miundombinu ya gridi ya taifa ya umeme.
Makumi ya maelfu ya kilomita za kebo bado zinahitajika ili kuhakikisha kuwa miji midogo na vijiji vya mbali vinaweza kuunganishwa.
Lakini kwa mhandisi, Bw Moges, umeme utakaozalishwa kwenye Blue Nile hatimaye italeta mabadiliko.
Ana mtoto wa kiume ambaye alizaliwa alipokuwa akifanya kazi kwenye bwawa hilo.
"Ninachukia ukweli kwamba sikuweza kumsaidia kama vile ilivyotakikana," anasema. "Lakini najua mustakabali wake utakuwa mzuri kwa sababu ya kitu ambacho nimechangia, na ninajivunia kumwambia hivyo atakapokuwa mkubwa."
Ripoti ya ziada ya Hanna Temurai

Imetafsiriwa na Seif Abdalla












