Siasa ngumu za Kenya zinavyotishia kurejea kwa maandamano mitaani

Chanzo cha picha, Getty Images
Kenya imerejea katika suala linalofahamika, inaendelea kukumbwa na mdororo wa kijamii na kiuchumi wa mara kwa mara huku upinzani ukitishia kuanzisha tena maandamano ya kuipinga serikali.
Muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja unasema kuwa utarejea kufanya maandamano ya kila wiki kuanzia leo Mei 2, 2023 ili kutoa shinikizo jipya kwa Rais William Ruto aweze kupunguza gharama ya maisha na kukubali mageuzi makubwa ya uchaguzi utakaohusisha pande mbili.
Aliyekuwa waziri mkuu wa taifa hilo, Raila Odinga amekuwa akiongoza maandamano hayo. Odinga alishindwa na Ruto katika uchaguzi wa Agosti 2022 - akiwania mara tano kiti cha urais. Aliyakataa matokeo ya uchaguzi akisema yalikuwa ya udanganyifu, licha ya kwamba yamethibitishwa na Mahakama ya Juu.
Odinga anasisitiza kuwa alishinda na anataka matokeo ya urais yachunguzwe upya kisayansi. Pia anataka mazungumzo ya kitaifa yafanyike kuhusu mageuzi ya kura na hatua za haraka za serikali kupunguza gharama ya maisha. Ruto anasema anakubaliana bunge kufanya marejeo kuhusu uteuzi wa makamishna wapya wa uchaguzi. Akaongeza kuwa uchaguzi wa mwaka 2022 umeshafungwa na kuhusu mfumuko wa bei anasema ni jambo la kimataifa lililo nje ya uwezo wake.
Washirika wakuu wa Ruto na Odinga wamekuwa na misimamo isiyobadilika ambayo imekuwa ikikinza juhudi za kuunda jopo la mazungumzo ya pande hizo mbili.
Maandamano ni jeraha jipa la kuidhuru nchi hiyo ambayo tayari imejeruhiwa kijamii na uchaguzi wa rais ulio na mzozo na nchi iliyoathiriwa kiuchumi kutokana na janga la Covid, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na ukame wa muda mrefu.
Pia wanadhoofisha sifa ya Kenya kama taifa imara katika eneo la mashariki na Pembe ya Afrika wakati ambapo majirani zake kadhaa wakionekana kutafuta msaada. Pia ni kuyumbisha uwekezaji wa kigeni katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi wa Afrika mashariki wakati ambao unauhitaji zaidi uwekezaji huo.
Polisi wapiga marufuku maandamano
Kenya haiwezi kuvumilia kuanzishwa tena kwa maandamano. Mfumuko wa bei ulishuka kwa miezi 10 hadi kiwango cha chini cha asilimia 7.9 mwezi Aprili, huku bei za vyakula zikitengemaa baada ya kuanza kwa mvua ndefu. Lakini Wakenya bado wanakabiliwa na ongezeko la gharama za umeme, nyumba, gesi ya kupikia na mafuta ya magari. Ukosefu wa ajira umeongezeka na inaweza kuwa sababu ya kuchochea machafuko.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tarehe 30 Aprili, Mkuu wa jeshi la polisi jijini Nairobi Adamson Bungei alipiga marufuku maandamano mapya, akibainisha kuwa "maandamano ya awali yalikumbwa na vurugu kwani waandamanaji walikuwa wamejihami kwa mapanga na kuwashambulia wananchi".
"Kwa hili, tunakataa kuruhusu timu ya Azimio kuendelea na maandamano na maandamano yoyote kama hayo yatatawanywa na maafisa wa polisi," Bungei alisema.
Odinga aliapa kwa kusema: "Iwapo utawala utaamua kugeuza shughuli zetu za amani na za kikatiba kuwa mapigano na mauaji ... na iwe hivyo, tuko tayari."
Hii inaweka mazingira kuwepo kwa makabiliano yanayoweza kusababisha vifo kati ya waandamanaji, wahalifu wakujichomeka na vikosi vya usalama.
Maandamano yaliyofanyika awali ya Machi 20, 27 na 30 yalikutana na ukinzani zaidi katika mji mkuu, Nairobi, na mji wa magharibi wa Kisumu. Miji hiyo miwili kihistoria imekuwa ngome za Odinga. Maandamano makali pia yalitokea Homa Bay, Migori na Siaya, katika eneo la nyumbani kwa Odinga kusini-magharibi mwa Nyanza.
Rasmi, watu watatu, miongoni mwao afisa wa polisi, waliuawa katika maandamano hayo. Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema mnamo Machi 29 kwamba maafisa wa polisi 51 na raia 85 walijeruhiwa kwenye maandamano hayo. Lakini ripoti za vyombo vya habari nchini humo zilionyesha kuwa takriban watu watano wameuawa.
Gazeti la Daily Nation liliripoti tarehe 2 Aprili juu ya madai ya njama za polisi kuficha idadi ya vifo vilivyotokea kwa sababu ya maandamano hayo. Hilo limezua hofu ya kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa maafisa wa usalama ambao wanadaiwa kutumia vibaya mamlaka yao.
Rais na maridhiano ya kisiasa

Chanzo cha picha, Getty Images
Hapo awali Ruto alijibu tishio la Odinga la kufanya maandamano akionyesha ni kama jambo la kawaida kwa mwanasiasa huyo mkongwe kufanya maandamano.
Hata hivyo, rais alibadili 'gia angani' huku maandamano hayo yakishika kasi na kutikisa biashara, sio tu jijini Nairobi na Kisumu, bali pia katika maeneo mengine yenye shughuli za utalii katika eneo la Pwani na katika Bonde la Ufa
Maafisa wa serikali na viongozi wa sekta ya biashara wanakadiria kuwa Kenya ilipoteza angalau dola milioni 20 katika kila siku ya maandamano. Hiyo ni kiasi kikubwa kwa serikali inayohangaika kukusanya mapato, kulipa watumishi wa umma na kuhudumia deni kubwa la taifa.
Katika hotuba yake ya kw ataifa tarehe 2 Aprili, 2023 iliyorushwa moja kwa moja na vituo vyote vikubwa vya runinga nchini humo, Ruto alitoa wito kwa upinzani kukomesha maandamano hayo na kukubali kushiriki katika mazungumzo. Lakini alifutilia mbali hoja ya kugawana madaraka na Odinga, kama alivyofanya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta,mwaka 2018.
"Milango ipo wazi kwa mashauriano ya ukweli, yenye muelekeo na ya dhati kwa kuzingatia utawala wa sheria na katiba," rais aliongeza.
Nchi jirani ziko chonjo

Uganda iko macho huku kukiwa na hofu kwamba maandamano nchini Kenya yanaweza kusababisha machafuko sawa na hayo nchini humo. Vyombo vya habari vya Uganda viliripoti kwamba polisi walishiriki mazoezi ya kuzuia ghasia tarehe 27 Machi. Siku moja baadaye, polisi waliwakamata watu 11 kwa kushiriki maandamano ya kupinga ufisadi mjini Kampala.
Katika nchi jirani ya Tanzania, wafanyabiashara wa nafaka wana hofu kwamba wanaweza kupoteza soko kubwa nchini Kenya.
Kenya ni lango la biashara inayounganisha nchi zisizo na bandari katika Ukanda wa Maziwa Makuu kupitia bandari ya Mombasa. Kwa hivyo, umuhimu wake wa biashara kati ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DR Congo na Sudan Kusini hauwezi kupuuzwa.
Kuwepo kwa usumbufu wowote wakati wa kusafirisha bidhaa kupitia Kenya bila shaka utasababisha hasara na kuongeza gharama kwa nchi zinazopokea mizigo.
Maandamano ya muda mrefu nchini Kenya huenda yakainufaisha Tanzania, ambayo inatoa njia mbadala ya biashara kwa nchi za Maziwa Makuu zisizo na bandari. Ingawa njia ya Tanzania ni ndefu na kwa hiyo ni ya gharama zaidi, lakini haielekei kukumbwa na usumbufu unaochochewa na siasa.
Wanajeshi wa Kenya ni muhimu katika juhudi za kikanda za kuleta utulivu wa Somalia na kumaliza mzozo wa mashariki mwa DR Congo. Kenya inashiriki katika mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Ethiopia na makundi ya waasi. Pia inahusika katika juhudi za upatanishi wa Sudan baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya vikosi hasimu vya kijeshi tarehe 15 Aprili.
Seneta wa Marekani Chris Coons - mshirika wa karibu wa Rais Biden - alitembelea Nairobi tarehe 29 Machi na kufanya mazungumzo na Odinga na Naibu Rais Rigathi Gachagua. Coons alishiriki katika makubaliano ya 2018 kati ya Odinga na Kenyatta na ziara yake ya hivi majuzi ilizua uvumi kuwa Marekani ilikuwa ikijaribu kufanya makubaliano kama ya wakati ule kati ya Ruto na Odinga.












