Je, mwili wako unahitaji sukari kiasi gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Fatuma Maalim Abukar
- Nafasi, BBC
Siku hizi, vijana wengi wanaacha kutumia sukari. Hili linasababu kadhaa, kama vile mabadiliko ya mtindo wa maisha na lishe.
Lakini sababu kubwa zaidi ni hatari ambayo sukari inaweza kuleta kwa afya zetu.
Kupunguza ulaji wako wa sukari kuna faida zisizoweza kupingwa, ikiwa ni pamoja na kupunguza kalori, ambayo inaweza kukusaidia kupunguza uzito na pia kwa afya ya meno.
Mtaalamu wa magonjwa, Dkt. Abdirahman Dhiblawe, aliiambia BBC kutumia sukari kupita kiwango kinachopendekezwa kunaweza kusababisha kuongezeka kwa uzito.
"Uzito mkubwa huongeza magonjwa mengi, kama vile kisukari, shinikizo la damu, maumivu ya viungo na magonjwa mengine kama moyo," anasema.
Je, miili yetu inahitaji sukari?

Chanzo cha picha, Getty Images
"La msingi kujua ni kiasi gani mwili unahitaji sukari. Hatuwezi kusema mwili hauhitaji sukari. Sukari inatumiwa na ubongo wetu.
Aina tatu za vyakula vinavyotumiwa na ubongo ni protini, mafuta na sukari. Ubongo hauwezi kutumia mafuta na protini pekee.
"Ikiwa mwili hauna sukari, ubongo wetu hutengeneza sukari kutoka protini na mafuta. Hivyo sukari ni muhimu kwa mwili, lakini kiasi kinachoruhusiwa ni kidogo," anasema.
Kukosa sukari mwilini, kunaweza kuleta mabadiliko katika kemikali za ubongo na kusababisha athari mbaya.
Je, tunapaswa kuacha sukari inayoongezwa kwenye chai, kahawa na vitu vingine?
“Watu wanasahau kuwa vyakula vyetu vingi vinatengenezwa kwa sukari, ukila sana unakuwa na sukari nyingi.”
Aina ya sukari ambayo mwili wetu unahitaji inaitwa glucose. Madaktari wanasema mwili hupata nishati nyingi kutokana na glukosi.
Lakini hakuna haja ya kuongeza glukosi kwenye mlo wako kwa sababu mwili hufanya hivyo kwa kuvunja vyakula kama vile mafuta, protini na wanga.
Faida za sukari mwilini

Chanzo cha picha, FINMAIL
Mbali na ukweli kwamba sukari ni nzuri kwa ubongo wetu, ina faida nyingine kwa mwili.
"Inaongeza nguvu mwilini, huleta hisia za furaha, ngozi yako inang’aa na akili yako iko bara’bara," anasema Dkt.
Ubongo unahitaji zaidi ya gramu 100 ya sukari kwa siku ili kufanya kazi. Madaktari wanasema mtu anapohisi msongo wa mawazo, sukari hubadilisha hisia hiyo na huleta furaha.
Sukari pia hutumiwa kusafisha mwili, kuondoa ngozi iliyokufa.
Uhusiano kati ya sukari na kisukari

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wanaokula kiasi kikubwa cha sukari wako katika hatari ya kupata magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.
Lakini kuna sababu nyingine pia za kupata magonjwa hayo. Dkt. Diblawey anasema kuna mambo mengine mengi ambayo yanaweza kusababisha magonjwa hayo.
"Ugonjwa wa kisukari hujidhihirisha kwa njia kadhaa, na hausababishwi na sukari pekee. Unaweza kuwa wa kurithi," anaeleza.
Kuna aina mbili za kisukari. Aina ya 1 na 2.
Kulingana na madaktari, aina ya 1 haisababishwi na sukari ya kawaida, bali na seli zinazozalisha insulin. Dutu inayodhibiti sukari kwenye kongosho, ambayo huharibiwa na mfumo wa kinga.
Lakini aina ya 2 inaweza kusababishwa na sukari nyingi inayotumiwa moja kwa moja au katika vyakula na vinywaji tunavyotumia.
Kipi kitatokea unapoacha sukari?

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wanaoacha kutumia sukari hupata athari mbaya. Ni pamoja na maumivu ya kichwa, uchovu, au mabadiliko ya hisia. Sababu ni mabadiliko ya ubongo tuliyozungumza.
"Utakosa nguvu, uelewa mdogo, uchovu, furaha kidogo na jasho zaidi," anasema.
Dkt. Dhiblaawe anasema wapo watu wanaotumia sukari kwa wingi, lakini haiwaathiriki.
"Watu hao wako vijijini. Wanaweza kunywa kikombe cha chai yenye sukari nyingi, lakini wanatembea sana," alisema.
“Tunaposema watu waache, si sawa kila mtu aache sukari," anasema.
Anashauri watu kuonana na daktari, kupima urefu na uzito wao, na kuamua ikiwa wanahitaji kupunguza matumizi ya sukari yao au la.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












