Maswali 4 kwa huduma ya Ujasusi Marekani baada ya Trump kushambuliwa

Maswali kadhaa makubwa yameibuka kwa Huduma ya Ujasusi nchini Marekani kujibu baada ya shambulio la risasi la Donald Trump kwenye mkutano huko Pennsylvania.

FBI imechukua jukumu la mpelelezi mkuu katika tukio hilo, ambapo mtu mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa vibaya - huku Trump akijeruhiwa sikio.

Huku Marekani ikidai majibu, mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi nchini humo ameitwa kutoa ushahidi mbele ya kamati ya Baraza la Wawakilishi la Marekani tarehe 22 Julai.

Haya hapa ni baadhi ya mambo ambayo wataalam wa usalama wanauliza.

Unaweza pia kusoma

Kwa nini paa la mtu mwenye bunduki halikuwekewa ulinzi?

Bado haijafahamika ni kwa jinsi gani mtu anayeshukiwa kuwa na bunduki Thomas Matthew Crooks alifanikiwa kupanda hadi katika paa la jengo karibu na mkutano wa hadhara ambao ulikuwa zaidi ya mita 130 (futi 430) kutoka kwa Trump.

Paa hilo lilikuwa hatari kabla ya tukio, kulingana na NBC News, ambayo ilitaja vyanzo viwili vinavyofahamu shughuli za shirika hilo la ujasusi.

"Mtu alipaswa kuwa juu ya paa au kulinda jengo ili mtu asiweweza kupanda juu ya paa hilo," NBC ilinukuu moja ya vyanzo vikisema.

Pamoja na swali la kufika katika eneo hilo, imependekezwa kuwa njia ya kutazama kutoka paa hilo hadi eneo la jukwaa la Trump ilipaswa kuwa imefungwa.

Hii ilikuwa "mojawapo ya vipengele vya msingi vya usalama, hasa (kwa) eneo ambalo liko nje na lisilodhibitiwa kwa kiasi kikubwa", kulingana na Naibu Mkurugenzi wa zamani wa FBI Andrew McCabe, akizungumza na CNN.

Je, maonyo kuhusu mtu mwenye bunduki yaliwasilishwa?

Mtu aliyeshuhudia ufyatuaji huo aliiambia BBC kwamba yeye na wengine walimuona Crooks akitambaa kwenye paa akiwa na bunduki.

Waliwaarifu polisi lakini mshukiwa aliendelea kutambaa kwa dakika kadhaa kabla ya kufyatua risasi na kisha kuuawa kwa kupigwa risasi, alisema.

Wakala maalum wa FBI Kevin Rojek alikiri "imeshangaza" kwamba mshambuliaji aliweza kufyatua risasi.

Sherifu wa kaunti amethibitisha kwamba Crooks alionywa na afisa wa polisi wa eneo hilo, ambaye hakuweza kumzuia kwa wakati.

Kitu ambacho bado hakijafahamika ni iwapo habari hii iliwafikia maafisa walio karibu na Trump.

Crooks tayari alikuwa kwenye rada za maafisa, kulingana na afisa mkuu wa utekelezaji wa sheria.

Habari hii inadaiwa ilitumwa kwa Huduma ya ujasusi.

Je, huduma ya ujasusi ilitegemea sana polisi wa eneo hilo?

Mshambuliaji huyo alifyatua risasi zake kutoka kwa kile ambacho polisi wamekielezea kuwa "pete ya pili ya usalama", ambayo ilikuwa inalindwa sio na Huduma ya ujasusi bali na maafisa wa polisi wa eneo hilo.

Ajenti wa zamani wa Huduma ya Ujasusi alisema mpango wa aina hii ulifanya kazi tu wakati kulikuwa na mpango wazi wa nini cha kufanya wakati hatari ilionekana.

"Unapotegemea washirika wa kutekeleza sheria wa ndani, ni vyema ukapanga kwa uangalifu na kuwaambia kile unachotarajia wafanye kuhusu tishio," Jonathan Wackrow aliiambia Washington Post.

Sherifu wa kaunti amekiri kuwa ‘’walishindwa" lakini akasema hakuna idara moja ya kulaumiwa .

Je, eneo hilo lilipangiwa usalama wa kutosha?

Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Uangalizi ya bunge amesema kuwa maafisa wa Huduma ya ujasusi walikuwa wachache sana", hatua ambayo ilizidisha swali la ni kwanini polisi wa eneo hilo "hawangepewa mafunzo" kulinda mkutano wa Jumamosi.

Jason Chaffetz, ambaye hapo awali aliripoti kushindwa kwa Huduma ya ujausi, aliiambia Washington Post hakuna "tishio" zaidi kuliko lile la Trump au Rais Biden, lakini kwamba hilo halikutiliwa maanani kuimarisha usalama huko Pennsylvania.

Huduma ya Ujasusi imekanusha kwamba ombi kutoka kwa timu ya Trump ya kuongeza maafisa lilikataliwa kabla ya mkutano huo.

Lakini gazeti la Post liliripoti kwamba liliona mabadilishano ya ujumbe ambapo afisa wa zamani wa Ujasusi aliwauliza wenzake jinsi mshukiwa huyo alivyopata bunduki na kuwa karibu na Trump. Aliripotiwa kupokea jibu: "Rasilimali."

Je, Trump alitolewa jukwaani haraka ipasavyo?

Maafisa waliomlinda Trump wamepokea sifa, akiwemo afisa wa zamani Robert McDonald, ambaye alisema walifanya "kazi nzuri" licha ya kuwa hakukuwa na mwongozo kamili kuhusu ni nini wangefanya katika hali kama hiyo.

Lakini swali pia limeulizwa ikiwa walikuwa na kasi ya kutosha kumpeleka rais huyo wa zamani hadi kwenye gari.

Picha za tukio hilo zinawaonyesha wakimzunguka kwa kasi mara baada ya milio ya risasi, lakini kisha wakaonekana kutulia huku Trump akiuliza kubeba viatu vyake.

Rais huyo wa zamani anaendelea kusukuma ngumi yake kwa wafuasi.

Afisa wa zamani wa shirika la Ujasusi nchini humo aliliambia gazeti la New York Times kuwa hangesubiri. "Ikiwa ni mimi , hapana. Tunaenda, na tunaenda sasa," Jeffrey James alisema. "Ikiwa ni mimi, ninamnunulia jozi mpya ya viatu."

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah