Uchaguzi wa Marekani 2024: Kubabaika kwa Biden katika mdahalo kwaongeza hofu kuhusu umri wake

    • Author, Anthony Zurcher
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kabla ya siku ya Alhamisi, Wamarekani wengi walikuwa tayari wana wasiwasi juu ya umri wa Joe Biden na ikiwa anafaa kuwa rais.

Rais huyo aliingia kwenye mdahalo watu wakiwa tayari wana wasiwasi nae, na amebabaika. Alikuwa mnyonge. Alikuwa akijikanyaga. Hakuwa muwazi.

Katikati ya mdahalo huo, timu ya kampeni ya Biden iliwaambia waandishi wa habari, 'rais anapambana na baridi' - jaribio la kutetea sauti yake ya mkwaruzo.

Ndani ya dakika 90 za mdahalo, Joe Biden alikuwa kwenye shida. Baadhi ya majibu yake hayakuwa na mantiki. Alikuwa akipoteza mtiririko wake wa mawazo.

Mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano wa Biden, Kate Bedingfield alihojiwa na CNN mara baada ya mdahalo kumaliza, na alisema: "Hakuna ubishi kuhusu hilo, huu haukuwa mdahalo mzuri kwa Joe Biden."

Alisema changamoto yake kubwa ilikuwa ni kuthibitisha, ana nguvu na ushupavu, na hakufanya hivyo.

Wakati mdahalo ukiendelea, kama bondia kwenye ulingo, Biden alimjaribu mpinzani wake katika jaribio la kubadilisha hali ya mambo. Majaribio machache kati ya hayo yalifanikiwa, na kumfanya rais huyo wa zamani kuwa na majibu ya hasira

Maswali ya kwanza yaliyotolewa na wasimamizi wa CNN yalikuwa kwenye masuala ya uchumi na uhamiaji. Kura za maoni zinaonyesha Wamarekani wanamwamini zaidi Donald Trump kuliko Biden katika mambo hayo.

"Kwa kweli sijui amesema nini mwishoni mwa sentensi hiyo, na sidhani kama kasema kitu," Trump alisema baada ya jibu la Biden.

Pia unaweza kusoma

Trump alikuwa makini

Rais huyo wa zamani kwa kiasi kikubwa alikuwa mwenye nidhamu na mwepesi. Aliepuka kudakia na uchokozi, mambo ambayo yalidhoofisha mjadala wake wa kwanza 2020 na akaugeuza mdahalo kuwa dhidi ya rekodi ya Biden kila ilipowezekana.

Mara kwa mara alitoa madai ambayo hayakuwa na ushahidi na ni ya uwongo mtupu, lakini Biden kwa kiasi kikubwa hakuweza kumdhibiti.

Mada ilipogeukia kwenye uavyaji mimba, rais huyo wa zamani alielekeza hoja yake kwenye kile alichokiita ni itikadi kali za chama cha Democratic. Alitoa madai ya uongo, kwamba Wanademocratic wanaunga mkono uavyaji mimba baada ya watoto kuzaliwa.

Uavyaji mimba ni suala ambalo linampa changamoto Trump na Warepublican kwa ujumla tangu kupinduliwa kwa sheria ya Roe v Wade na Mahakama ya Juu mwaka 2022, sheria ambayo ilikuwa ikilinda haki ya kikatiba ya kutoa mimba -.

Mashambulizi ya Biden katika eneo hilo dhidi ya Trump yangempa pointi nyingi, lakini yalishindwa. "Ni jambo baya sana ulilofanya," rais alisema.

Muda mfupi baada ya mdahalo kukamilika, Makamu wa Rais Kamala Harris alikiri kwamba rais "alianza vibaya" lakini akasema alimaliza vyema.

Hayo ni matumaini, lakini ni kweli Biden alijiweka sawa wakati mdahalo ukiendelea.

Biden alisema kukutwa na hatia Donald Trump katika mashtaka yaliyotokana na madai ya uhusiano wa kimapenzi na nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels ni "maadili mabovu."

"Sijafanya ngono na nyota huyo," alijibu Trump.

Trump pia alionekana kushindwa kunyoosha maelezo alipoulizwa juu ya uvamizi katika Bunge la Marekani Januari 6, 2021. Alijaribu kugeuza swali kuhusu kuhusika kwake katika ghasia hizo kwa kulaani rekodi ya Biden, lakini rais hakumruhusu kufanya hivyo.

"Aliwahimiza watu kwenda Capitol Hill. Alikaa kwa saa tatu huku wasaidizi wake wakimsihi asawazishe hali hiyo. Lakini hakufanya kitu," alisema Biden.

Rais huyo wa zamani pia alikwepa mara kwa mara, alipoulizwa iwapo atakubali matokeo ya uchaguzi wa 2024.

Kipi kitatokea baadaye?

Huu ulikuwa mdahalo wa mapema zaidi katika historia ya siasa za Marekani.

Watu wengi watazungumzia utendaji kazi wa Biden baada ya mdahalo huu kuliko ule wa rais wa zamani.

Wana-democratic wana kongamano lao la chama mwezi Agosti, wataweza kutoa maono yao kuhusu muhula wa pili wa Biden. Na kuna mjadala mwingine uliopangwa kufanyika Septemba, (ikiwa utafanyika) – kuelekea uchaguzi wa Novemba.

Wana-democratic wengi watakuwa wanafikiria ikiwa mjadala wa pili dhidi ya Trump utakuwa tofauti kwa Biden. Na wengine wanafikiria ikiwa ni bora kupata mgombea mwingine wa urais.

Timu ya kampeni ya Biden ina miezi miwili ya kutuliza hali ya mambo. Biden alishinda kura za mchujo za chama ili kugombea na hadi sasa hakuna mwanasiasa wa ngazi ya juu wa Democratic ambaye amesema hadharani Biden abadilishwe.

Alipoulizwa na BBC kuhusu uwezekano wa kufungua kongamano la chama kwa kuruhusu wagombea wengine au kumbadilisha mgombea wa sasa, Naibu Meneja wa Kampeni Quentin Fulks alisema "hatutolipa suali hilo umuhimu kwa kulijibu."

"Rais Biden atakuwa mgombea wa Democratic, na Rais Biden atashinda uchaguzi huu," aliongeza.

Baada ya mdahalo, wafuasi wengi wa Democratic watakuwa na mashaka makubwa juu ya matarajio ya Biden mwezi Novemba.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga