Vita vya Ukraine: Viongozi wa upinzani wa Urusi wako wapi sasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Vladimir Putin sasa anatawala Urusi bila kupingwa. Sauti nyingi za kukosoa ambazo ziliwahi kuongea zimelazimika kwenda uhamishoni, wakati wapinzani wengine wamefungwa - au katika matukio mengine kuuawa.
Kufikia wakati alipoanzisha uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022, zaidi ya miongo miwili ya kukomesha upinzani ulikuwa umemaliza upinzani nchini Urusi.
Mwanzoni kabisa mwa utawala wa Rais Putin, aliwashinda matajiri wenye nguvu wa Urusi - matajiri wakubwa wenye malengo ya kisiasa.
Mikhail Khodorkovsky, aliyekuwa mkuu wa kampuni kubwa ya mafuta ya Urusi Yukos, alikamatwa mwaka 2003 na kukaa jela miaka 10 kwa kukwepa kulipa kodi na wizi baada ya kufadhili vyama vya upinzani. Alipoachiliwa, aliondoka Urusi.
Boris Berezovsky, tajiri mwingine ambaye hata alimsaidia Putin madarakani - alitofautiana naye baadaye na alikufa uhamishoni nchini Uingereza mnamo 2013, ikiripotiwa kujiua.
Vyombo vya habari vyote muhimu nchini Urusi polepole vilianguka chini ya udhibiti wa serikali ya Kremlin.
Alexei Navalny
Kwa sasa kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi sasa ni Alexei Navalny, ambaye akiwa jela amemshutumu Putin kuwapaka matope mamia ya maelfu ya watu katika vita vyake vya "uhalifu na uchokozi".
Mnamo Agosti 2020, Navalny alitiwa sumu ya Novichok, wakati wa safari ya kwenda Siberia. Shambulio hilo lilikaribia kumuua, na ilibidi asafirishwe hadi Ujerumani kwa ajili ya matibabu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kurudi kwake Urusi mnamo Januari 2021 kuliwachochea waandamanaji wa upinzani kwa muda mfupi, lakini alikamatwa mara moja kwa ulaghai na kudharau mahakama. Sasa anatumikia kifungo cha miaka tisa gerezani, na ndiye aliyekuwa msisitizo wa filamu iliyoshinda tuzo ya Oscar.
Katika miaka ya 2010 Navalny alishiriki kikamilifu katika mikutano mingi ya kupinga serikali na mengi yaliyofichuliwa na chombo kikuu cha kisiasa cha Navalny, Wakfu wa Kupambana na Ufisadi (FBK), yamevutia mamilioni ya maoni mtandaoni.
Mnamo 2021 wakfu huo uliharamishwa kama wenye msimamo mkali na Navalny amepuuzilia mbali madai ya ufisadi akidai kuwa yalichochewa kisiasa.
Wengi wa washirika wake wamekumbana na shinikizo kutoka kwa vyombo vya usalama, na wengine wamekimbilia nje ya nchi, akiwemo mkuu wa zamani wa FBK Ivan Zhdanov, mwanasheria mkuu wa zamani wa FBK Lyubov Sobol na wengi, ikiwa sio wote, wakuu wa mtandao mpana wa ofisi za Navalny kote Urusi.
Mwanaume wa mkono wa kulia wa Navalny Leonid Volkov aliondoka Urusi wakati kesi ya utakatishaji fedha ilipoanzishwa dhidi yake mwaka wa 2019.
Upinzani wa vita
Mkosoaji mwingine mkuu wa Putin nyuma ya jela za Urusi ni Ilya Yashin, ambaye amekuwa akikosoa vikali vita vya Urusi.
Katika matangazo moja kwa moja kwenye YouTube mnamo Aprili 2022, alihimiza uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita unaowezekana kufanywa na vikosi vya Urusi na kumwita Rais Putin "mchinjaji mbaya zaidi katika vita hivi".
Matangazo hayo ya moja kwa moja yalisababisha kifungo cha miaka minane na nusu jela kwa kukiuka sheria dhidi ya kueneza "habari za uwongo kwa makusudi" kuhusu jeshi la Urusi.
Sheria hiyo ilipitishwa bungeni muda mfupi baada ya Urusi kuivamia Ukraine tarehe 24 Februari 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images
Yashin alijihusisha na siasa mwaka wa 2000 akiwa na umri wa miaka 17, mwaka ambao Putin aliingia madarakani.
Mnamo mwaka wa 2017, baada ya miaka mingi ya harakati za upinzani, alichaguliwa kuwa mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Krasnoselsky huko Moscow, ambapo aliendelea kutoa maoni ya kukosoa Kremlin.
Mnamo mwaka wa 2019, alitumia zaidi ya mwezi mmoja gerezani kwa jukumu lake kubwa katika maandamano dhidi ya kukataa kwa mamlaka kusajili wagombeaji huru na wenye nia ya upinzani kwa uchaguzi wa baraza la jiji la Moscow.
Mwandishi wa habari na mwanaharakati aliyeelimishwa Cambridge Vladimir Kara-Murza amewahi kudhulumiwa mara mbili kwa sumu ya ajabu iliyomwacha kwenye fahamu, mwaka wa 2015 na kisha 2017.
Alikamatwa Aprili 2022 kufuatia ukosoaji wake wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na kushtakiwa kwa kushiriki "habari bandia" kuhusu jeshi la Urusi, kuandaa shughuli za "shirika lisilofaa" na uhaini mkubwa. Wakili wake anasema anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 25 ikiwa atapatikana na hatia.
Ameandika makala nyingi zinazomkosoa Putin katika vyombo vya habari maarufu vya Urusi na Magharibi na mwaka 2011 aliongoza juhudi za upinzani ili kupata kupitishwa kwa vikwazo vya Magharibi vinavyolenga wale wanaokiuka haki za binadamu nchini Urusi.
Kupigania demokrasia
Kara-Murza alikuwa naibu mwenyekiti wa Open Russia, kikundi kikuu cha demokrasia kilichoanzishwa na tajiri aliyekimbia Mikhail Khodorkovsky.
Ilitambuliwa rasmi kama "isiyofaa" nchini Urusi na hatimaye kufungwa mnamo 2021. Mkuu wa Urusi, Andrei Pivovarov, anatumikia kifungo cha miaka minne jela kilichowekwa kwa kuhusika kwake katika "shirika lisilofaa".
Huenda Kara-Murza anakabiliwa na kifungo cha muda mrefu gerezani lakini angalau yuko hai, tofauti na rafiki wa karibu na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Urusi Boris Nemtsov.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kabla ya enzi ya Putin, Nemtsov aliwahi kuwa gavana wa mkoa wa Nizhny Novgorod, waziri wa nishati na kisha naibu waziri mkuu, na pia alichaguliwa katika bunge la Urusi. Kisha akazidi kutoa sauti katika upinzani wake kwa Kremlin, na kuchapisha ripoti kadhaa za kumkosoa Vladimir Putin na akaongoza maandamano mengi kumpinga.
Mnamo tarehe 27 Februari 2015, Nemtsov alipigwa risasi nne alipokuwa akivuka daraja nje ya Kremlin, saa chache baada ya kuomba kuungwa mkono kwa maandamano dhidi ya uvamizi wa awali wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2014.
Wanaume watano wa asili ya Chechen walipatikana na hatia ya mauaji ya Nemtsov, lakini bado hakuna uwazi kuhusu ni nani aliyeamuru au kwa nini.
Miaka saba baada ya kifo chake, uchunguzi ulionesha ushahidi kwamba katika miezi kadhaa kabla ya mauaji hayo, Nemtsov alikuwa akifuatwa kote Urusi na wakala wa serikali aliyehusishwa na kikosi cha siri cha mauaji.
Viongozi hawa wakuu wa upinzani ni baadhi tu ya Warusi wanaolengwa kwa kosa la kuonesha upinzani.
Tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana, vyombo vya habari huru nchini Urusi vimeona vikwazo au vitisho zaidi. Kituo cha habari cha TV Rain imelazimika kuhamia nje ya nchi, na kujiunga na tovuti ya habari ya Meduza ambayo tayari ilikuwa imeondoka Urusi.
Novaya Gazeta imesalia mjini Moscow lakini imeacha kuchapisha gazeti lake. Nyingine kama kituo cha redio cha Echo cha Moscow kilifungwa na mamlaka.
Wachambuzi wengi wamekwenda uhamishoni, kama vile mwanahabari mkongwe Alexander Nevzorov, aliyemtaja kama "wakala wa kigeni" nchini Urusi na kuhukumiwa kifungo cha miaka minane jela bila kuwepo kwa kueneza habari "feki" dhidi ya jeshi la Urusi.
Lakini sio lazima uwe na hadhira ya mamilioni ili kulengwa. Mnamo Machi 2023, Dmitry Ivanov, mwanafunzi wa hesabu ambaye aliendesha chaneli ya Telegraph ya kupinga vita, alipatiwa kifungo cha miaka minane na nusu gerezani - pia kwa kueneza habari "feki" kuhusu jeshi.
Ilimchukua Vladimir Putin zaidi ya miongo miwili kuhakikisha hakuna wapinzani wa kutisha waliokuwa huru kupinga mamlaka yake. Ikiwa huo ndio ulikuwa mpango wake, ungefanya kazi.















