Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Mitazamo mitatu namna mzozo huu utakavyoendelea 2024
Mzozo nchini Ukraine unakaribia kuingia mwaka wake wa tatu wa kalenda. Wanajeshi walio mstari wa mbele hawajaweza kusonga mbele katika miezi michache iliyopita. Je, mkondo wa vita unaweza kubadilika 2024?
Rais wa Ukraine, Volodomyr Zelensky amekiri mashambulizi ya nchi yake wakati wa msimu wa baridi hayakuwa na mafanikio aliyoyatarajia. Urusi bado inadhibiti karibu 18% ya Ukraine.
Tumewauliza wachambuzi watatu wa masuala ya kijeshi - watupe mitazamo yao kuhusu mwelekeo wa vita katika miezi 12 ijayo.
Vita vitaendelea 2024 lakini havitaendelea milele
Barbara Zanchetta kutoka Idara ya Mafunzo ya Vita, Chuo cha King College London anaeleza:
Hakuna matumaini ya kumalizikavita nchini Ukraine 2024. Vladimir Putin ana nguvu za kisiasa zaidi kuliko kijeshi.
Mashambulizi ya majira ya baridi ya Ukraine yanaonekana kusitishwa. Lakini Urusi pia haijafanikiwa kusonga mbele zaidi ya hapo awali. Matokeo ya vita hivi kwa upande wa Ukraine yanategemea maamuzi ya kisiasa yatakayofanywa huko Washington na Brussels.
Umoja ulionyeshwa na nchi za Magharibi mwaka wa 2022, na ukadumu mwaka mzima 2023, unaonekana kuyumba.
Msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine umekwama huko Washington. Na mustakabali wa msaada wa kiuchumi wa EU unaonekana kutatizika kutokana na msimamo wenye utata wa Hungary.
Mivutano katika miji mikuu ya nchi za Magharibi yamempa moyo Putin. Kuonekana kwake hadharani hivi karibuni na kauli za dharau - kunaonyesha ni kwa jinsi gani Urusi imejiandaa na vita hivi kwa muda mrefu zaidi.
Je, nchi za Magharibi zitakuwa na nguvu na uimara wa kuendelea kumpinga Putin?
Uamuzi wa EU kufungua mazungumzo ya uanachama na Ukraine na Moldova ni ya ishara tu. Yakimaanisha itaendelea kuunga mkono Kyiv, kwani mustakabali wa Ukraine ndani ya EU hautowezekana ikiwa Urusi itashinda vita.
Katika nchi za kidemokrasia, kuunga mkono vita kwa muda mrefu - daima ni maamuzi magumu kuliko katika nchi zinazoongozwa kiimla. Ingawa kuna uwezekano vita vitaendelea 2024, lakini haviwezi kuendelea milele.
Yasipotokea mapinduzi au suala linalohusiana na afya na kusababisha kifo au kuondoka Putin, hakutokuwa na namna nyingine zaidi ya kuwepo kwa mazungumzo ya amani – jambo ambalo kwa sasa pande zote mbili zinaendelea kulikataa.
Mwaka 2024 ni wa kujiimarisha
Michael Clarke, mkurugenzi mstaafu wa taasisi ya Royal United Services anaeleza:
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine 2022 ulishuhudia kurudi kwa vita katika bara la Ulaya. Mwenendo wa mzozo 2023 uliashiria ukweli kwamba vita vya wakati wa maendeleo ya viwanda vimerejea pia.
Vita vya namna hii huathiri Uchumi mzima - hasa utengenezaji wa nyenzo za vita kama mambo ya kipaumbele. Bajeti ya ulinzi ya Urusi imeongezeka mara tatu tangu 2021 na itatumia 30% ya matumizi ya serikali mwaka ujao.
Hii itafanya vita vya Ukraine kuwa vya muda mrefu na vyenye matukio mengi. Mwaka ujao tutaona kama Urusi - na washirika wake Korea Kaskazini na Iran - na Ukraine - na waungaji mkono wake wa Magharibi – ikiwa wamejitayarisha kukidhi matakwa mabaya ya vita vya enzi ya viwanda.
Itakuwa ni makosa kusema kwamba mstari wa mbele nchini Ukraine umekwama. Bado pande zote mbili zina uwezo wa kupigana huku kila mmoja akijaribu kutumia mbinu za kimkakati.
Vikosi vya Urusi vinaweza kujaribu kusonga tena mbele, angalau kulinda eneo lote la Donbas. Ukraine pengine itajaribu kutafuta udhibiti wa Bahari Nyeusi ya magharibi na ukanda wake muhimu wa kibiashara hadi Bosphorus.
2024 unaonekana kama mwaka wa kujiimarisha kwa Kyiv na Moscow. Urusi haina vifaa kwa sasa na wafanyakazi waliofunzwa kufanya mashambulizi ya kimkakati hadi mapema majira ya baridi 2025.
Wakati huo huo, Ukraine inahitaji fedha za Magharibi na usaidizi wa kijeshi ili kuendelea kupigana mwaka ujao - ili ijenga nguvu zake za ndani na kuunda mazingira ya mashambulizi ya kukomboa maeneo katika siku zijazo.
Mwelekeo wa vita 2024 yataamuliwa zaidi huko Moscow, Kyiv, Washington, Brussels, Beijing, Tehran na Pyongyang kuliko Avdiivka, Tokmak, Kramatorsk au mkoa wowote ulioharibiwa na mapigano.
Crimea ndio eneo la maamuzi
Ben Hodges, jenerali mstaafu wa Jeshi la Marekani huko Ulaya
Urusi haina uwezo wa kuichukua Ukraine yote na itafanya iwezalo kushikilia kile inachoshikilia kwa sasa, huku ikiimarisha ulinzi wake na kutumai nchi za Magharibi zitapoteza nia ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Lakini Ukraine haitoacha kupigana. Inapigania maisha yake na inaelewa nini Urusi itafanya ikiwa itaacha kupigana. Mataifa mengi ya Ulaya sasa yanazungumza juu ya hitaji la kuongeza msaada kwa wasiwasi kwamba Marekani inapunguza kasi katika ahadi zake.
Hata hivyo, ninatarajia mapema mwaka mpya Marekani itapitisha mfuko wa msaada wa kijeshi ambao umecheleweshwa katika Bunge la Congress mwezi Disemba.
Kwa hivyo, natarajia Ukraine itafanya yafuatayo katika miezi ijayo:
- Kuunda upya vikosi ambavyo vimechoka kutokana na mapigano – jambo hilo litakuwa muhimu kwa mashambulizi mapya.
- Kuboresha mfumo wa kuajiri ndani ya Ukraine ili kuongeza nguvu kazi watu.
- Kuongeza uzalishaji wa risasi na silaha.
- Kuboresha uwezo wake dhidi ya uwezo wa teknolojia za Urusi.
Kufikia mwanzoni mwa majira ya kiangazi Ukraine itakuwa na uwezo wa kutumia ndege za kivita za F16 zilizotengenezwa Marekani kwa mara ya kwanza. Zitaboresha uwezo wake wa kukabiliana na ndege za Urusi na kuimarisha ulinzi wake wa anga.
Sehemu muhimu zaidi ya kimkakati kwa Ukraine ambayo bado inadhibitiwa na Urusi ni Crimea, tunaliita "eneo la maamuzi."
Ukraine itafanya yote iwezayo kupambana na Urusi ili kulidhoofisha jeshi la wanamaji la Urusi huko Sevastopol, kambi chache za jeshi la anga katika eneo hilo na kambi yao ya usafirishaji ya Dzankoy.
Tayari wamethibitisha uwezo wao. Kwa kutumia makombora matatu yaliyotolewa na Uingereza, Storm Shadow cruise, wamemlazimisha kamanda wa Kikosi cha Bahari Nyeusi kuondoa theluthi moja ya meli zake kutoka Sevastopol.
Ukraine haina silaha nyingi na makombora ya masafa marefu. Lakini askari wa Urusi wako katika hali mbaya zaidi. Vita ni nia na mipango. Mipango ya Urusi ni dhaifu na iko chini ya shinikizo la Ukraine kila siku.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi