Kwa nini ni vigumu kusema ‘hapana?’

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Fernanda Paúl
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Umewahi kukubali kufanya kitu kwa sababu uliogopa kusema hapana? Ikiwa ndivyo, huko peke yako. Kulingana na tafiti mbalimbali, watu wengi wanaona vigumu kuweka mipaka.
Sababu? Hofu ya kutengwa, hofu ya kujijengea picha mbaya ua haja ya kufurahisha wale walio karibu nawe
Mwanasaikolojia kutoka Hispania, Alba Cardalda aliamua kusoma jambo hilo kwa kina baada ya kugundua kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wake walikuwa na shida katika mahusiano yao binafsi kwa sababu hawakuweza kusema hapana.
Kutokana na utafiti wake, kitabu How to Send People to Hell Politely, kiliibuka, na hapa anaeleza umuhimu wa kuweka mipaka.
Kusema hapana

Chanzo cha picha, Sabrina Solfa
Kwa sababu hatujaelimishwa kusema hapana tangu udogoni. Kinyume chake; tumeelimishwa kuwafurahisha wengine bila kuzingatia hisia zetu wenyewe.
Kwa kawaida tunaogopa kufikiriwa kuwa sisi ni watu wabinafsi au hata wabaya ikiwa tutakataa jambo fulani. Tunafundishwa kujali ambacho wengine wanataka au kudai na sio kuthamini hisia zetu binafsi au kuwa wa wazi kwa kile tunachotaka au tusichotaka.
Kwa sehemu kubwa, daima tunatafuta kukubalika kutoka kwa wale walio karibu nasi.
Kwa mfano, mfanyakazi mwenzako anapokuomba jambo fulani - kumlipia au kufanya baadhi ya kazi ambazo si zako - na huwezi kukataa.
Au marafiki na familia wanapopendekeza mpango fulani na wakati huo hujisikii kufanya kwa sababu umechoka lakini unaishia kufanya jambo ambalo hujisikii kufanya.
Kufanya mambo ambayo hatutaki kufanya - au ambayo huna wakati wa kufanya - huleta mawazo, mfadhaiko na wasiwasi.
Mipaka ya kimwili na ya kihisia

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa sababu ni mipaka ambayo haiwezi kuonekana, ni migumu. Sio kama kufunga mlango wa chumba. Kwa hiyo, ni muhimu kujielewa mwenyewe.
Moja ya mambo ninayopendekeza ni kutambua mipaka yako, juu ya yapi yanaweza kujadiliwa na yale ambayo hayawezi kujadiliwa kuhusu wewe. Jitahidi kuwa muwazi katika hilo.
Njia pekee ya kuhifadhi ustawi wetu ni kuweka mipaka. Kwa sababu pia hufafanua aina ya uhusiano tulionayo kwa wengine na hilo ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga uhusiano wenye afya na kuzungukwa na watu wanaotutendea vyema.
Nadhani watu ambao hawatutendei vizuri au hawaheshimu mipaka hiyo, lazima tujue jinsi ya kuwaweka umbali.
Wakati mtu anavuka mipaka tena na tena, ni halali kabisa kusema “ondoka.” Ndiyo njia pekee ya kuhifadhi utu wetu. Kufanya hivyo pia kunatoa amani kubwa ya akili na hilo ni muhimu kwa afya yako.
Ni wajibu kwako mwenyewe kuweka mipaka yako. Na kinachotokea ni kwamba ataanza kukuheshimu mara moja.
Kuwa na furaha

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ninachopendekeza kila wakati ni kuwa uwazi. Ikiwa mtu anakufanya ujisikie vibaya, kuwa muwazi na mwambie.
Imezoeleka kwamba mtu anapomfanyia mtu mwingine jambo zuri, bila kujua anamtarajia mwenzake afanye vivyo hivyo. Na asipofanya hivyo, tunakasirika.
Kulingana na utafiti juu ya furaha - uliofanywa na profesa wa magonjwa ya akili wa Chuo Kikuu cha Harvard, Robert Waldinger - watu wanakuwa na furaha zaidi wanapokuwa na uhusiano mzuri katika jamii na mazingira ya karibu.
Hapo awali ilisemwa ili kuwa na furaha ni lazima ufanye mazoezi au kuishi zaidi katika kuwasiliana na mazingira au kuwa na hali nzuri ya kiuchumi au kufanya kazi unayoipenda. Lakini utafiti huu unaonyesha jambo muhimu zaidi ni kudumisha uhusiano mzuri na watu wengine.
Na kwa mahusiano haya kuwa na afya, moja ya jambo muhimu ni lazima kuwe na uaminifu. Watu wanapaswa kuwa na uwezo wa kujieleza kwa uaminifu na uwazi. Na kutoruhusu mambo yanayokusumbua au kuvuka mipaka yafanyike.
Kwa hiyo, kumwambia mtu kitu usichotaka ndiyo njia ya kutuwezesha kujenga mahusiano yenye afya, imara na ya kudumu.
Kutojali ni muhimu

Chanzo cha picha, Getty Images
Haki ya kuwa na maoni yako mwenyewe, kusema hapana au kusema ndiyo, haki ya kutendewa kwa heshima na utu, kubadilisha mawazo yako, kuwa bwana wa wakati wako, mwili wako na maisha yako.
Haki hizi ni muhimu sana. Unapaswa kuwa muwazi juu ya haki hizo. Ingawa ni kweli tunahitaji idhini ya kikundi ili kuishi Lakini tatizo linakuja pale uidhinishaji huu wa kijamii unapokuwa mwingi.
Ikiwa mtu anahitaji idhini ili ajisikie kuwa wa thamani, utegemezi wa aina hii si sahihi kwa sababu tunapoteza uwezo wa kufanya maamuzi. Na hilo hutufanya tukose furaha kwa sababu tunafanya maamuzi yanayotegemea kuwafurahisha wengine.
Lakini kadiri miaka inavyosonga, kujali kwetu kunapungua. Na kusema hupendi au hapana kunazidi kuwa rahisi.
Unapaswa kuthamini mipaka yako ya kimwili na kiakili na usipoteze tena usingizi ikiwa mtu hapendi ulichomwambia.
Pia inahusiana na umri. Unapozeeka, unagundua jinsi wakati ulivyo na thamani, na namna unavyokwenda kwa kasi. Na hapo ndipo tunaelewa kipi hasa cha kuweka kipaumbele.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












