Dirisha la Uhamisho England : Je, wachezaji hawa wanaelekea wapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wiki zilizosalia katika dirisha la uhamisho la Ulaya zitasheheni shughuli nyingi.
Dirisha la uhamisho la wachezaji linafungwa kwa chini ya wiki mbili na kuna idadi ya wachezaji ambao mustakabali wao haujulikani.
Raheem Sterling atakuwa wapi mwezi ujao? Je, Ivan Toney ataondoka Premier League? Je, Arsenal wataongeza kikosi chao?
Tunaangazia baadhi ya wachezaji ambao wanaweza kuhama.
Raheem Sterling
Ni wapi pengine pa kuanzia isipokuwa kwa Sterling?
Mustakabali wa Raheem Sterling Chelsea haukuwa shakani hadi saa moja kabla ya mechi yao ya kwanza ya ufunguzi dhidi ya Manchester City Jumapili.
Kutokuwepo kwake kwenye kikosi na kufuatiwa na taarifa kutoka kwa wawakilishi wa Sterling wanaotaka "uwazi" kuhusu jukumu lake katika klabu hiyo kunapendekeza kwamba anaweza kutaka kuondoka.
Akiwa na umri wa miaka 29 tu, fowadi huyo wa zamani wa Liverpool bila shaka angehitajika? West Ham na Crystal Palace tayari wamehusishwa na uwezekano wa kumnunua.
Ameichezea Chelsea mechi 81 tangu ajiunge nayo kutoka Manchester City kwa £50m Julai 2022.
Joao Felix, Ben Chilwell, Conor Gallagher - Chelsea inaweza kuwa na shughuli nyingi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Haishangazi kuona kwamba kuna dalili za wasiwasi huko Stamford Bridge.
Chelsea imetumia takriban pauni milioni 185 kununua wachezaji 11 msimu huu, na kumwacha kocha Enzo Maresca na kikosi cha zaidi ya wachezaji 40.
Huwezi kufurahisha kila mtu.
Kuondoka kwa Conor Gallagher katika daraja la Stamford Bridge kwa hakika bado ni jambo lisiloepukika - ingawa uhamisho wake wa kwenda Atletico Madrid bado umesitishwa - wakati Ben Chilwell ni mwingine ambaye anaweza kutafuta kuondoka baada ya kuachwa nje ya kikosi cha Jumapili.
Wachezaji wengine wa Chelsea ambao hawakushiriki katika wikendi ya ufunguzi wa Ligi ya Premia ni pamoja na beki Trevoh Chalobah na kiungo Noni Madueke.
Huku Maresca akiwa na hamu ya kuwatoa baadhi ya wachezaji wake, jiandae kwa uhamisho wa kushangaza katika Uwanja wa Stamford Bridge siku zijazo.
Mshambulizi Romelu Lukaku ni uhamisho mwingine wa Chelsea ambao unaweza kutokea mwezi huu - ndio, bado yuko katika timu ya Chelsea .
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ametumia miaka miwili iliyopita kwa mkopo nchini Italia na sasa anasakwa na Napoli - dili la kubadilishana Victor Osimhen ni chaguo mojawapo ambalo linaweza kupendekezwa.
Mchezaji mwengine mpya anayetarajiwa kuhamia Chelsea ni Joao Felix wa Atletico, ambaye klabu hiyo ya Uhispania inataka kumjumuisha katika dili la Gallagher.
Ivan Toney
Mkufunzi wa Brentford Thomas Frank hangeweza kusema kabisa Ivan Toney alikuwa amecheza mechi yake ya mwisho, lakini inaonekana kuna uwezekano mkubwa.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aliachwa nje katika mechi ya ufunguzi ya Brentford dhidi ya Crystal Palace baada ya dau la pauni milioni 35 ili ajiunge na klabu ya Saudia ya Al-Ahli wiki jana kukataliwa.
Alipoulizwa na BBC Radio 5 Live iwapo ilikuwa ni suala la wakati kabla ya Toney kuondoka, Frank aliongeza: "Ndiyo, nadhani hiyo ni haki."
Toney amekuwa Brentford kwa miaka minne iliyopita na alifunga mabao 20 katika mechi 33 za Premier League msimu wa 2022-23.
Mkataba wake unamalizika msimu huu na amekuwa akihusishwa na kuhamia kama Arsenal na Chelsea hapo awali - lakini uhamisho wa kuelekea Saudi sasa unaonekana kama kitu anachopenda
Marc Guehi
Je, Marc Guehi bado atakuwa Crystal Palace katika muda wa wiki mbili? Hakuna aliye na fununu kwa sasa.
The Eagles wamekataa ofa tatu kutoka kwa Newcastle kwa ajili ya kumnunua beki huyo wa Uingereza, toleo la hivi punde likiwa la takriban pauni milioni 60.
Beki huyo wa kati alikuwa nahodha wa Palace katika kushindwa kwao na Brentford siku ya Jumapili, lakini bado haijajulikana kama Newcastle wako tayari kuongeza ofa yao.
Joe Gomez
Iwapo Newcastle watakata tamaa katika kumsaka Guehi, mchezaji wa Liverpool Joe Gomez anatajwa kuwa mbadala wake.
Beki huyo aliachwa kwenye kikosi cha kwanza cha Arne Slot cha Ligi Kuu ya Uingereza Jumamosi na sasa anahusishwa pakubwa na kuondoka Anfield.
Vilevile Newcastle, Aston Villa, Fulham na Crystal Palace - kama mbadala wa Guehi - wanaripotiwa kumtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27.
Mikel Merino

Hili linaonekana kuwa suala la muda tu.
Arsenal wapo kwenye mazungumzo na Real Sociedad kuhusu kumsajili kiungo wa kati wa Uhispania Merino.
Alikuwa sehemu ya kikosi cha Uhispania ambacho kilishinda Euro 2024 na kushiriki katika mechi zote saba za mashindano hayo, akifunga bao la ushindi dakika za lala salama dhidi ya Ujerumani katika robo fainali yao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 amebakiza chini ya mwaka mmoja kwenye mkataba wake, jambo ambalo linaweza kusaidia Arsenal kukamilisha dili kwani ataweza kuzungumza na vilabu kuhusu kusaini kwa uhamisho wa bure mwezi Januari.
Jarrad Branthwaite
Everton wanataka kumzuia beki wao wa kati mwenye umri wa miaka 22 - lakini 'kelele' ya uhamisho ni kubwa sana.
The Toffees tayari wamekataa ofa mbili kutoka kwa Manchester United kwa ajili ya Jarrad Branthwaite mapema msimu huu , huku timu hiyo ya Old Trafford ikiwa imemsajili Matthijs de Ligt kutoka Bayern Munich.
Kuna pande nyingi zinazoripotiwa kuvutiwa naye huku timu ya hivi karibuni ikiwa Liverpool .
Scott McTominay na Jadon Sancho

Chanzo cha picha, Getty Images
Kunaweza kuwa na wachezaji wazuri ambao huenda wakaondoka Manchester United msimu huu
Jadon Sancho huenda akarejea Manchester United, baada ya kutofautiana na meneja Eric ten Hag kabla ya kuhamia Borussia Dortmund kwa mkopo, lakini swali ni kwa muda gani?
Sancho hakuhusika katika mechi ya kwanza ya Ijumaa dhidi ya Fulham na, huku wachezaji kadhaa waliokuwa majeruhi wakiwa bado hawajarejea, huenda akawa anajiuliza ni nafasi ngapi atakazopata.
Mchezaji mwingine anayehusishwa na kuondoka ni Scott McTominay baada ya kuachwa kwenye kikosi cha kwanza cha United katika ushindi dhidi ya Fulham.
Cottagers, Crystal Palace na Brighton ni baadhi tu ya vilabu vinavyoripotiwa kuwa na nia.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












