Utafiti: Panya mwenye baba wawili atengenezwa maabara

Chanzo cha picha, Buena Vista Images
Katika jaribio la kwanza la kisayansi, panya aliye na wazazi wawili wa kiume amefanikiwa kukua.
Watafiti walifanikisha hatua hii muhimu kwa kutumia uundaji wa seli za kiinitete, kurekebisha kwa usahihi vinasaba muhimu vinavyohusika katika uzazi ili kuunda panya kutoka kwa baba-wawili.
Mbinu hii ya mafanikio iliwawezesha wanasayansi kushinda ugumu uliofikiriwa kutowezekana katika uzazi wa mamalia wa jinsi moja.
Katika majaribio ya hapo awali, viinitete vya panya havikuweza kukua kwa sababu kutumia panya wawili wa kiume kulisababisha matatizo ya vinasaba wakati wa urutubishaji, na kusababisha dosari za kimaumbile baada ya kuzaliwa.
Hata hivyo, wataalamu wa utafiti huu mpya walishuku kuwa masuala haya ya vinasaba yalisababishwa na kutotumia vinasaba vya asili - ambapo kwa kawaida lazima zirithiwe kutoka kwa mzazi wa kiume na wa kike.
"Sifa za kipekee za vinasaba visivyo asili zimewafanya wanasayansi kuamini kwamba ni kizuizi cha kimsingi kwa uzazi wa jinsi moja kwa mamalia," asema Prof Qi Zhou, mwandishi mwenza wa utafiti huo.
"Hata wakati wa kuunda viinitete vya mama wawili au baba-baba kwa njia ya kutengeneza, vinashindwa kukua vizuri, na hukwama wakati fulani wakati wa ukuaji kwa sababu ya vinasaba hivi."
Kutokana na nadharia hii, watafiti walirekebisha vinasaba 20 visivyo asili kwa kutumia mbinu mbalimbali kabla ya kupandikiza viinitete kwa 'mama mbadala'.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matokeo ya utafiti huo yalibaini kuwa mabadiliko haya ya vinasaba hayakuwezesha tu kutengenezwa kwa panya-mwenye baba wawili lakini pia, katika baadhi ya matukio, yaliwaruhusu kuishi hadi kufikia utu uzima.
"Matokeo haya yanatoa ushahidi thabiti kwamba dosari za kimaumbile ndio kizuizi kikuu cha uzazi wa mamalia wa jinsi moja," anasema mwandishi mshiriki Prof Guan-Zheng Luo wa Chuo Kikuu cha Sun Yat-sen.
"Njia hii inaweza kuboresha kwa kiasi kikubwa matokeo ya ukuaji wa seli za kiinitete na wanyama kutengenezwa, na kutoa hakikisho kwa maendeleo ya tiba.
Lakini sio habari zote njema. Watafiti hao waliripoti kuwa ni asilimia 11.8 tu ya viinitete vilivyokua hadi kuzaliwa, na hata hivyo, vingine havikuishi hadi utu uzima kwa sababu ya kasoro za ukuaji.
Aidha, wengi wa panya waliofikia utu uzima walikuwa na ukuaji usio wa kawaida na muda mfupi wa kuishi, na wale ambao walioweza kuishi pia walikuwa tasa.
Jopo la wataalamu linajitahidi kutatua matatizo haya kwa kuangazia jinsi ya kubadilisha vinasaba fulani kunaweza kusaidia viini-tete kukua vyema.
Pia wanapanga kujaribu utafiti wao juu ya wanyama wengine, kama nyani.
Hadi wakati huo, haijulikani sana ikiwa teknolojia hii itatumika kwa binadamu.















