INEC yamjibu Polepole, yasisitiza uhuru wa mifumo yake ya uchaguzi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (INEC) imekanusha vikali madai yaliyotolewa naaliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ambaye pia ni kada Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyejitokeza hivi karibuni kukosoa mamlaka.

Polepole, katika mazungumzo yake yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana, alidai kuwa mifumo ya CCM, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Uchaguzi imeunganishwa, kauli ambayo alidai inakiwezesha chama chake kupata ushindi hata kabla ya siku ya uchaguzi.

Madai haya yalizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii na kulazimisha INEC kutoa taarifa rasmi kupitia kurasa zake.

Katika taarifa hiyo, Tume imekanusha madai hayo, ikiyataja kuwa ni ya upotoshaji na kutokana na ukosefu wa uelewa. Taarifa hiyo, iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Uchaguzi, imefafanua kuwa daftari la kudumu la wapiga kura halijaunganishwa na mfumo wowote wa serikali au wa kisiasa.

"Mfumo wa upigaji kura, kuhesabu, na kutangaza matokeo hautumii mfumo wa aina yoyote ya kielektroniki," ilisema taarifa hiyo. "Badala yake, mfumo unatumia taratibu za kawaida (manual) kama ilivyozoeleka."

INEC pia imefafanua kuwa kitambulisho cha taifa hakitumiki kupigia kura, badala yake kinachotumika ni kadi ya mpiga kura inayotolewa na Tume yenyewe. Aidha, imebainisha kuwa vyama vya siasa hupewa nakala ya daftari inayoonesha idadi ya walioandikishwa katika vituo husika baada ya uboreshaji kukamilika.

Tume imetoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zenye lengo la kuzua taharuki na kuharibu sifa ya mfumo wa uchaguzi. Kulingana na INEC, kauli za aina hiyo zinatolewa na watu wasio na uelewa wa kutosha.