Rais Samia atengua uteuzi wa Polepole, amuondolea hadhi ya ubalozi

Polepole

Chanzo cha picha, Polepole Instagram

Muda wa kusoma: Dakika 2

Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia Katibu Mkuu wake, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo imeeleza kwamba imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka ikitaarifu kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Hamphrey Polepole aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kumuondolea hadhi ya ubalozi. Mwananchi imeripoti.

Uamuzi huo wa Rais ni chini ya mamlaka aliyonayo chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Rais Samia, kwa mamlaka aliyonayo chini ya utumishi wa umma, amemuachisha kazi Polepole kwa manufaa ya umma.

Kwa mujibu wa barua hiyo, uamuzi huo umeanza tangu julai 16 mwaka 2025.

Balozi huyo alijiuzuru siku ya Jumatatu akidai hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi.

Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan na Dr Emmanuel Nchimbi kama wagombea wa Urais na Makamu katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba Mwaka huu.

"Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara" alisema Polepole.

Katika barua kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyochapisha katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Polepole alitilia doa mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya chama hicho huku taifa hilo likijiandaa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Mbunge huyo wa zamani wa kuteuliwa ambaye pia aliwahi kuhudumu kama balozi wa Tanzania nchini Malawi amesema kauli maarufu ya CCM ya "Chama kwanza mtu baadaye" inafanyika vinginevyo.

"Kwa kuwa siwezi kuendelea kuwa sehemu ya uongozi usiohamasika na utii wa misingi ya Katiba ya nchi na chama, haki, maadili, utu na uwajibikaji wa wananchi, nimeamua kwa hiari yangu kujiuzulu nafasi yangu ya uongozi na utendaji serikalini," alisema Polepole, akiongeza kuwa ataendelea kuwa mwanachama wa kawaida wa CCM.

Humphrey Polepole ni nani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Humphrey polepole amekuwa mwanasiasa maarufu kwa takriban miaka 10 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Malawi mwaka 2022. Alikulia katika Umoja wa Vijana wa CCM.

Alianza kujulikana zaidi mwaka 2012 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na kumaliza kazi yake mwaka 2014.

Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, alikohudumu kwa miezi michache kisha kuhamishiwa Ubungo Dar es Salaam kwa nafasi hiyo hiyo ya ukuu wa wilaya na kuhudumu kwa miezi michache pia.

Umaarufu wake uliongezeka alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo kimsingi ni ya kuwa msemaji wa chama.

Anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020. Rais Samia alipoingia madarakani Machi 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaji kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.

Anajulikana pia kwa kauli tata au ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwa kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa.

Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa. Linalongojewa sasa ni kuona mustakabali wake kisiasa baada ya kujiuzulu ubalozi na nafasi nyingine za umma.