Je, historia inajirudia kwa mabalozi wa kisiasa kupitia Polepole?

Wiziri ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania ilitangaza rasmi kwamba aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, amevuliwa rasmi hadhi ya ubalozi kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi wake na Rais Samia Suluhu Hassan.
Tangazo hilo lilihitimisha sura muhimu katika maisha ya mwanasiasa huyo machachari, ambaye siku chache kabla alikuwa tayari ametuma barua ya kujiuzulu kwa kile alichokieleza kuwa "kufifia kwa maadili ya uongozi wa kitaifa."
Lakini kwa waliowahi kuishi ndani ya dunia ya diplomasia, habari hii haikuwa ya kawaida. Kwao, kupoteza hadhi ya ubalozi si tu kufutwa kwa kazi, bali ni kuanguka kwa heshima ya kimataifa, kupotea kwa kinga ya kisheria, na mwisho wa maisha ya kifahari ambayo wengi huyaona kwenye sinema tu.
Humphrey Polepole alipanda kwa kasi inayopingana na jina lake si kwa polepole. Akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, sauti yake ilikua na uzito serikalini. Kisha akawa Mbunge wa kuteuliwa, nafasi iliyompatia jukwaa la kuchambua, kushauri, na wakati mwingine kuonyesha msimamo binafsi unaogusa mipaka ya ridhaa ya chama.
Baadaye, aliteuliwa kuwa Balozi. Japo hakuwekwa wazi aliteuliwa kwenda nchi gani mwanzoni, nafasi hiyo ilitosha kumuweka juu: kimuundo, kidiplomasia, na kijamii. Alikuwa sehemu ya mfumo wa kimataifa wa uwakilishi wa Tanzania. Hatimaye, akatumikia kama Balozi nchini Malawi, kisha Cuba. Lakini Agosti 2025, hadhi hiyo inafikia tamati hadhi ambayo, kama alvyowahi kusema mwandishi Pascal Mayalla, "huja na heshima, kinga, na nafasi ya kipekee, lakini si mali ya kudumu."
Fahamu heshima, hadhi na kinga anazokwenda kupoteza

Chanzo cha picha, Humphrey
Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia (Vienna Convention on Diplomatic Relations), mabalozi wanapopelekwa nchi za ugenini hubeba hadhi na kinga maalumu zinazowatofautisha na raia wa kawaida. Hata mabalozi walioko nyumbani, kama Polepole kabla ya kupelekwa Malawi na baadaye Cuba, hupata baadhi ya stahiki hizo kulingana na mamlaka waliyopewa na Rais.
Kwa mfano, balozi hupewa pasipoti ya kidiplomasia inayowawezesha kusafiri bila vizuizi, wakati mwingine bila kupekuliwa au kuulizwa maswali mengi, huku wakipita eneo la wageni wa heshima (VIP). Pia huwa na hadhi ya kutokamatwa au kushikiliwa wanapokuwa katika majukumu ya kidiplomasia, hasa kwa wale walioko nje ya nchi. Wanapewa msamaha wa kodi na ushuru kwa baadhi ya bidhaa na huduma, na pia hutangulizwa kwa heshima katika matukio ya kitaifa na kimataifa.
Kwa Polepole, kupoteza hadhi ya ubalozi kuna maana zaidi ya kuondolewa ofisini. Kuna athari za kijamii, kisiasa na hata kifamilia. Gari lake halitakuwa tena na namba za CDM (Corps Diplomatique). Hata akifika uwanja wa ndege, atalazimika kupitia msururu ule ule wa raia wengine.
Abbas Mwalimu, mchambuzi wa masuala ya diplomasia, anafafanua kwamba "balozi ni Taifa linalotembea" na taifa hilo linatambulika kwa alama, kinga, na heshima, si kwa jina tu. Mwalimu anaongeza kwamba uteuzi wa balozi unaweza kutokana na weledi au siasa. Kwa Polepole, ni dhahiri alikuwa miongoni mwa wateule wa kisiasa (political appointees), kundi ambalo linategemea upepo wa kisiasa. Kama barafu, hadhi ya balozi huweza kuyeyuka ghafla.. unaipata, lakini si lazima iwe ya kudumu.
Waliowahi kuvuliwa hadhi ya ubalozi kama Polepole

Chanzo cha picha, getty image
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Polepole si wa kwanza. Na pengine si wa mwisho. Historia ya Tanzania imewahi kushuhudia baadhi ya wanasiasa au maafisa walioteuliwa kuwa mabalozi kisha wakaondolewa kwa sababu mbalimbali kisiasa, kinidhamu au kwa mabadiliko ya kawaida ya kiutawala.
Balozi Ali Mchumo, aliyewahi kuhudumu pia kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kilimo la Kusini mwa Afrika (SACCAR), aliondolewa kimya kimya kabla ya kustaafu. Balozi Tuvako Manongi, aliyewahi kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, aliachishwa ghafla mwaka 2016, bila maelezo ya kina. Costa Mahalu, aliyewahi kuwa balozi nchini Italia, naye alitenguliwa lakini baadaye uteuzi wake ukarejeshwa. Alphayo Kidata, aliyekuwa balozi wa Canada, aliondolewa na Hayati Rais Magufuli mwaka 2018. Wilbroad Slaa, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, aliondolewa na Rais Samia Septemba 2023, na kisha kurejea tena katika siasa za upinzani.
Katika muktadha huu, mchambuzi Mayalla anasisitiza kuwa hadhi ya ubalozi inahitaji "nidhamu ya juu, lugha makini, na ukimya wenye hekima." Kwa maneno mengine, si kila aliyeteuliwa anaweza kubeba uzito wa bendera ya taifa bila kuyumba. Na pindi misingi hiyo inapodhoofika, nafasi hiyo huwa kama mzigo kuliko hadhi.
Kwa hiyo, tukimwangalia Polepole katika muktadha huu mpana, tunaona alichokumbana nacho ni sehemu ya utaratibu usioandikwa lakini uliozoeleka: ukiteuliwa kisiasa, unategemea neema ya kisiasa. Na neema hiyo ikiisha, pasipoti yako pia huisha hadhi yake.














