Saulos Chilima: Makamu wa rais wa Malawi ambaye alitoswa katika siasa kutoka sekta ya biashara

Na Basilioh Rukanga,BBC News

TH
Maelezo ya picha, Saulos Chilima amekuwa makamu wa rais kwa miaka 10

Makamu wa Rais wa Malawi Saulos Chilima amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 51 baada ya ndege ya kijeshi aliyokuwa akisafiria kuanguka katika msitu kaskazini mwa nchi hiyo.

Alikuwa makamu wa rais kwa miaka 10, awali chini ya Rais wa zamani Peter Mutharika, ambaye alimteua kutoka sekta ya biashara kwa wadhifa wa pili wa juu zaidi serikalini.

Alielezewa kama "mtendaji" na "mchapakazi" lakini akajikuta katikati ya tuhuma za ufisadi serikalini.

Kwanza kama mshitaki, na kisha kama mshitakiwa.

Kabla ya Dk Chilima kuwa makamu wa rais mwaka 2014, alikuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya simu ya Airtel Malawi, raia wa kwanza wa Malawi kuongoza shirika hilo.

Bw Mutharika alikuwa ameripotiwa kusema kuwa anashirikiana na mtu "anayetegemewa na mwenye tija".

Lakini miaka minne baadaye, Dk Chilima alitofautiana na rais, akiishutumu serikali kwa kutofanya vya kutosha kupambana na ufisadi na kulinda baadhi ya watu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Chini ya sheria za Malawi rais hawezi kumfukuza kazi makamu wa rais - Dk Chilima alikaidi wito wa kujiuzulu licha ya kupinga hadharani serikali aliyokuwamo.

Baadaye aliunda chama chake cha kisiasa, United Transformation Movement (UTM), akitoa wito wa mabadiliko makubwa na mageuzi nchini.

Aligombea urais mnamo 2019 kama mgombeaji wa chama na akaibuka wa tatu.

Bw Mutharika alishinda uchaguzi huo lakini ukabatilishwa na mahakama kuu ya Malawi kwa sababu ya dosari nyingi.

Ilikuwa ni mara ya kwanza barani Afrika kwa matokeo ya uchaguzi kubatilishwa na mahakama na kisha rais aliyeko madarakani kushindwa katika marudio ya uchaguzi.

Dk Chilima aliungana na Lazarus Chakwera kama mgombea mwenza wake katika marudio ya kihistoria ya 2020.

Bw Chakwera, ambaye alikuwa ameibuka wa pili katika kura iliyokataliwa ya 2019, alichaguliwa kwa njia ya kishindo kuwa rais, na Dk Chilima akawa makamu wake wa rais.

Lakini makamu wa rais hivi karibuni alikabiliwa na tuhuma za ufisadi, ambazo alikuwa amezipinga sana katika utawala uliopita.

Alikamatwa mnamo 2022 kwa madai kwamba alipokea pesa kama malipo kwa kushawishi utoaji wa kandarasi za serikali - ambayo alikanusha.

Rais aliwafuta kazi maafisa wengine waliotajwa pamoja naye.

Kwa vile hakuweza kumfukuza kazi makamu wa rais, Bw Chakwera aliahidi kwamba hatamkabidhi tena majukumu yoyote Dkt Chilima wakati akikabiliwa na kesi.

Lakini mashtaka hayo yalitupiliwa mbali mwezi uliopita bila sababu zilizotolewa - katika hatua iliyozua maswali kuhusu ushughulikiaji wa kesi za ufisadi.

Kabla ya nafasi yake kama kigogo kisiasa nchini Malawi, Dk Chilima alikuwa ameshikilia majukumu mengine ya juu katika sekta ya kibinafsi , ikiwa ni pamoja na Coca Cola na Unilever.

Alikuwa mchumi na alikuwa na PhD katika usimamizi wa maarifa.

Wakati akihudumu serikalini, pia alikuwa waziri anayehusika na mipango ya uchumi na mageuzi ya sekta ya umma.

Tovuti ya serikali ilisema alikuwa "mtendaji", "mchapakazi" na "mfanisi".

Dr Chilima alizaliwa tarehe 12 Februari 1973 katika wilaya ya Ntcheu katikati mwa Malawi.

Anaacha mke wake Mary na watoto wawili, Sean na Elizabeth.