Mapinduzi ya Niger: Kwanini operesheni ya kijeshi ya ECOWAS inaweza kuwa ngumu?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili

Siku saba zilizowekwa na Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, Ecowas kuwataka viongozi wa kijeshi Niger kuirudisha serikali ya kiraia, zimeisha na viongozi hao hawaonyeshi nia ya kuondoka madarakani. Nchi wanachama zimetishia kuingia kijeshi katika taifa hilo.

Ingawa asili ya kuanzishwa Ecowas ni kwa sababu za kiuchumi, jumuiya hiyo ina historia ya kuingilia kati migogoro ya wanachama kwa njia za kijeshi. Tangu mwaka 1990, tayari imeshaingia kwenye nchi sita.

Ecowas kupitia jumuiya yake ya uangalizi wa kijeshi, Ecomog, huingilia kati migogoro kwa sababu kadhaa, ikiwemo kuzuia uasi, kusimamia usitishwaji wa mapigano, kuondoa madikteta na kulinda amani.

Kuna wimbi la mapinduzi katika nchi wanachama. Tangu 2020 nchi nne zimefanya mapinduzi, ikiwemo Niger, na nyingine ni Mali, Burkina Faso na Guinea ambako kumetokea mapinduzi mara tano katika nchi hizo tatu. Niger si mgeni wa mapinduzi, nchi hiyo imekumbwa na mapinduzi mara nane.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Ecowas ilipeleka vikosi vyake Gambia kumfurusha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Yahya Abdul-Aziz Jammeh mwaka 2017, katika misheni iliyopewa jina la operesheni ya kurudisha demokrasia.

Je, kwanini operesheni ya kijeshi Niger inaweza kuwa ngumu?

Changamoto za Ecowas

Ingawa nchi nyingi wanachama wa Ecowas kuwa tayari kuchangia jeshi la kwenda Niger. Nigeria ambayo Rais wake Bola Tinubu ndiye mwenyekiti wa jumuiya hiyo na taifa lake ni lenye nguvu, amekumbana na upinzani mkubwa panapohusika wazo la kupeleka wanajeshi Niger.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimeripoti kuwa upinzani wa hatua hiyo umetoka katika baraza la juu la bunge, Seneti, licha ya kwamba linadhibitiwa na chama cha Bw Tinubu. Ikumbukwe kwamba, katiba ya Nigeria inasema rais hawezi kupeleka wanajeshi bila idhini ya Bunge.

Fauka ya hilo, nchi wanachama wa Ecowas wanakumbwa na matatizo yakiwemo ya kiuchumi na makundi ya watu wenye silaha. Nigeria na Senegal, wanachama wenye nguvu wa Ecowas, pia nchi hizo zipo katika ukanda wa Sahel ambao unakumbwa na changamoto za kuwepo makundi ya wapiganaji.

Kama yalivyo mataifa mengine ya Afrika, uchumi wa mataifa ya Ecowas umeathiriwa na janga la uviko 19 na vita vya Ukraine. Operesheni za kijeshi zina gharama, na gharama huzidi ukubwa ikiwa uchumi umeporomoka.

Uungwaji mkono wa Niger

Ecowas ina uungwaji mkono kutoka Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa, Nchi za Ulaya na Marekani, kwa upande mwingine yapo mataifa yametangaza yatakuwa tayari kusimama na Niger ikawa itavamiwa kijeshi.

Nchi jirani za Mali Mali na Burkina Faso ambazo pia zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi, zimetangaza kuunga mkono serikali ya kijeshi ya Niger. Na kueleza - uingiliaji kati wa kijeshi nchini Niger, watauhesabu ni tangazo la vita dhidi yao pia.

Pia, vyombo vya habari vimeripoti kwamba serikali ya kijeshi ya nchi hiyo imeomba usaidizi wa kijeshi kwa mamluki wa Wagner, siku chache kabla ya siku ya mwisho iliyowekwa na Ecowas kufika.

Ikiwa nchi hizo jirani na kundi la Wagner watakuwa tayari kukaa upande wa jeshi la Niger wakati ambao vikosi vya Ecowas vinaingia katika taifa hilo, hivyo vinaweza kuwa vita badala ya kuwa operesheni ya kumrudisha Mohammed Bazoum madarakani.

Uwezo wa Niger

Gambia nchi ndogo kieneo, ina jeshi dhaifu, wakaazi wake ni milioni 2.64 kwa mujibu wa Benki ya Dunia. Haikuwa kazi ngumu kwa vikosi vya Ecowas vilivyoongozwa na Senegal kuingia na kumfurusha Yahya Jammeh, bila upinzani wowote kutoka jeshi la nchi hiyo.

Niger nchi kubwa kieneo, ni kubwa mara mbili ya Ufaransa. Vikosi vyake vya kijeshi vimepokea mafunzo kutoka vikosi vya Marekani na chi za Ulaya. Jeshi lake limekuwa likipokea msaada wa vifaa kutoka mataifa yenye nguvu ili kupambana na makundi ya kislamu.

Fauka ya hilo, mkuu wa majeshi wa taifa hilo alitangaza kuunga mkono kundi la wanajeshi waliompindua Bazoum. Kwa lugha nyingine, jeshi lote la nchi hiyo liko upande mmoja na wanajeshi waliopindua serikali ya kiraia.

Mjumuiko wa hayo yote, kunaufanya uamuzi wa kuingia kijeshi kuzidi kuwa mgumu. Uwezo wa jeshi la Niger, ukubwa wa nchi hiyo na jeshi la nchi hiyo kuwa pamoja, kutaifanya operesheni ya Ecowas kuwa ngumu.

Diplomasia itafua dafu?

Kuingia Niger kijeshi kumedhihirika kuwa na changamoto nyingi. Hakuna uhakika ikiwa azimio la kuchukua hatua za kijeshi litafanyika au diplomasia itapewa nguvu zaidi. Lakini, maswali mawili muhimu yanabaki; itakuwaje ikiwa njia za kidiplomasia zitakwama?

Je, Ecowas itaamua kuingia kijeshi licha ya upinzani na changamoto zilizo mbele yao? Kwa hakika muda utasaidia kujibu maswali haya, wakati huu mgogoro huo ukizidi kufuka moshi Magharibi mwa bara la Afrika.