Je, mamluki wa Wagner wanafanya kazi nchini Niger?

Baada ya mapinduzi ya Niger, madai ya uongo na taarifa potofu zinasambazwa mtandaoni, na hivyo kuongeza kwa wasi wasi kuhusu ya mustakabali wa nchi hiyo.

Tumeangalia baadhi ya madai yanayoshirikiwa zaidi.

Picha za zamani na zilizobadilishwa zinazoonesha 'Wagner troops' wakiwasili

Marekani imesema kundi la mamluki la Wagner la Urusi "linatumia " ukosefu wa utulivu nchini Niger kwa ajili ya kufanikisha maslahi yake - lakini hadi sasa hakuna ushahidi wa wapiganaji wa kundi hilo kupelekwa huko.

Vikosi vya Wagner vimekuwa vikifanya kazi katika nchi nyingine za Afrika kama vile nchi jirani za Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hata hivyo, video ya ndege ya kijeshi ya Urusi inayodaiwa kutua Niamey, mji mkuu wa Niger, imekuwa ikisambaa - pamoja na uvumi kwamba "vikosi vya Wagner tayari vimeanza kuingia mjini".

Ndege iliyo kwenye video inalingana na ndege ya kijeshi ya Urusi IL 76, lakini picha ni za zamani.

Kitengo cha BBC cha kuhakikisha habari BBC Verify kilifanya utafiti wa matoleo ya awali ya video hii inayopatikana mtandaoni na kugundua kuwa ilichapishwa kwenye YouTube mwaka wa 2006, na ukweli unaonyesha kwamba ndege hili ilikuwa ikitua katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Video nyingine - iliyotazamwa zaidi ya mara 500,000 kwenye TikTok - inawasilisha kimakosa picha za zamani za wapiganaji wa Wagner barani Afrika kama uthibitisho wa kwanza wa kuonekana kwao nchini Niger.

Inatoka kwenye ripoti ya habari, iliyotangazwa na kituo cha habari cha France 24 Januari mwaka jana, ikizungumzia uwepo wa Wagner nchini Mali badala ya Niger.

Video inayosambazwa kwenye TikTok inaonekana imehaririwa ili kuondoa maelezo yote mawili yanayoonyeshwa eneo la tukio kwenye skrini kuwa Mali na na nchi katika ripoti yenyewe.

Kwingineko, picha ya zamani ya wapiganaji wa Wagner nchini Ukraine imeshirikiwa pamoja na madai kwamba kundi hilo lilikuwa linapanga kutuma wapiganaji wake nchini Niger.

Lakini, hakuna tangazo kama hilo ambalo limechapishwa katika vikundi vilivyounganishwa na Wagner kwenye Telegraph hadi sasa.

Madai ya uongo kuhusu kupiga marufuku usafirishaji wa uranium

Dai lingine la upotoshaji lililosambaa mtandaoni kufuatia mapinduzi ambalo lilidai kuwa viongozi wapya wa kijeshi "walipiga marufuku usafirishaji wa uranium hadi Ufaransa mara moja".

Niger ni koloni la zamani la Ufaransa na Ufaransa bado ina ushawishi nchini humo.

Baadhi ya machapisho, kama haya yaliyo hapo juu, yanajumuisha kwa kiasi kikubwa takwimu sahihi kuhusu mauzo ya uranium hadi Ufaransa na Umoja wa Ulaya, lakini hakuna ushahidi kwamba junta ilipiga marufuku uuzaji wa uranium nchini Ufaransa wakati ilipochukua hatamu.

Kampuni ya Ufaransa inayojihusisha na uchimbaji madini ya uranium nchini Niger, Orano Group, ilisema kuwa shughuli zake zimeendelea katika maeneo ya Arlit na Akokan na katika makao yake makuu mjini Niamey kufuatia mapinduzi hayo.

Jeshi la Niger kutowazuilia wageni

Huku baadhi ya nchi za Ulaya zikianza kuwahamisha raia wao kufuatia mapinduzi hayo, madai yasiyo na msingi yalianza kusambaa kwamba junta waliwaagizwa wanajeshi kuwaweka kizuizini raia wa Ulaya.

Ilidai hili lilifanywa ili nchi za Magharibi ziondoe majeshi yao kutoka Niger.

Madai hayo yanaonekana kutokana na wito wa vuguvugu la M62, ambalo ni kundi linalounga mkono utawala wa kijeshi na linaloipinga Ufaransa, kwa raia wa Ulaya kushikiliwa mateka hadi majeshi ya kigeni yatakapoondoka.

Kundi hilo, hata hivyo, haliwakilishi junta.

Kiongozi wa mapinduzi Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema wiki iliyopita kwamba raia wa Ufaransa hawana chochote cha kuogopa na "hawajawahi kuwa tishio hata kidogo".

Kwa sasa Niger ina vikosi vya wanajeshi wa Ufaransa na Marekani, na vikosi hivi bado vipo.

Algeria haikusema itaunga mkono Junta

Madai pia yameibuka kuhusu nchi jirani ya Algeria, kukiwa na fununu kwamba inaweza kuunga mkono serikali ya kijeshi ya Niger endapo kutatokea uingiliaji wowote wa kigeni.

"Algeria haitakaa kimya wakati uvamizi wa nchi jirani ukifanyika," chapisho moja la Twitter lilisema, likihusisha hili na "vituo vya habari vya Algeria".

Jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, imetishia kuingilia kati (ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuingilia kijeshi) ikiwa rais aliyeondolewa hatarejeshwa madarakani.

Hata hivyo, Mali na Burkina Faso, wanachama wa Ecowas wakiongozwa na viongozi wa kijeshi - walisema wataunga mkono utawala wa kijeshi endapo utatokea uingiliaji wowote kutoka nje.

Algeria imesema inapinga uingiliaji kati wa kijeshi, lakini muhimu zaidi, haijasema itawaunga mkono viongozi wa mapinduzi ya Niger iwapo uingiliaji kati wa nje utafanyika.

Baadhi ya machapisho yanayodai Algeria itaiunga mkono Niger dhidi ya uingiliaji kati wa kigeni yalitaja akaunti inayoitwa Intel Kirby kama chanzo cha madai yao.

Tuliangalia akaunti hii kwenye Twitter. Ilichapisha tarehe 30 Julai kwamba "Algeria haitakaa kimya wakati nchi jirani inavamiwa," lakini iliweka wazi kwamba huu ulikuwa ni uchambuzi wake wa kile kinachoweza kutokea - sio tamko la sera ya serikali.