Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mgogoro wa mapinduzi Niger: Wahusika wakuu ni akina nani?
Kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum wa Niger na viongozi wa mapinduzi wakiongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani kumeitumbukiza Afrika Magharibi katika mgogoro wa kikanda.
Kuwasili kwa utawala mwingine wa kijeshi kunatishia kusababisha kukosekana kwa utulivu katika eneo linalokumbwa na ukosefu wa usalama unaochangiwa na uwepo wa wanamgambo wa Kijihadi.
Lakini athari ya mapinduzi hayo yanaonekana kuwa makubwa zaidi, huku jumuiya ya kimataifa kwa kiasi kikubwa ikiungana katika kulaani. Lakini je, wahusika wakuu katika mzozo huu ni akina nani na ni nini kiko hatari?
Jeneral Abdourahamane Tchiani
Jenerali Tchiani, mwenye umri wa miaka 62, amekuwa kamanda wa Walinzi wa Rais tangu 2011 na ni mshirika wa karibu wa Rais wa zamani Mahamadou Issoufou. Alijitangaza kama kiongozi wa serikali mpya ya kijeshi ya Niger baada ya mapinduzi.
Ni machache yanajulikana hadharani kuhusu maisha ya kibinafsi ya Tchiani, elimu au kazi yake ya kijeshi, lakini amekuwa akitajwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari vya Niger kuhusiana na jaribio la mapinduzi ya 2015 dhidi ya Issoufou.
Tchiani alifikishwa mahakamani mwaka wa 2018 na kukanusha madai hayo na hatimaye akaondolewa mashtaka ya kuhusika.
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni tarehe 2 Agosti, Tchiani alisema wanajeshi hawatakubali shinikizo la kikanda la kumrejesha madarakani Rais Bazoum.
Rais Mohamed Bazoum
Rais Bazoum aliapishwa kauwa kiongozi wa Niger tarehe 2 Aprili 2021, akimrithi Mahamadou Issoufou ambaye alikuwa ameongoza nchi hiyo kutoka 2011 hadi 2021. Bazoum ni mshirika wa karibu wa mataifa ya Magharibi na aling'olewa madarakani na utawala wa kijeshi tarehe 26 Julai 2023.
Waangalizi wanaamini kuwa anazuiliwa nyumbani kwake katika mji mkuu wa Niamey. Utawala wa Bazoum umeshirikiana na nchi za Ulaya katika jitihada za kujaribu kuzuia mmiminiko wa wahamiaji katika Bahari ya Mediterania.
Alikubali kurejesha mamia ya wahamiaji kutoka vituo vya kizuizini nchini Libya na pia kukabiliana na walanguzi wa binadamu katika vituo muhimu vya usafiri kati ya Afrika Magharibi na Kaskazini. Baada ya utawala wa Bazoum kutimuliwa madarakani, jambo hili sasa linaweza kutiliwa shaka.
Jeshi la Niger
Jeshi la Niger limeunga mkono kuondolewa madarakani kwa serikali ya Rais Mohamed Bazoum, likitaja kuzorota kwa hali ya usalama na "utawala mbovu wa kiuchumi na kijamii". Limeonya dhidi ya uingiliaji kijeshi wa kigeni.
Maafisa wakuu wa kijeshi walibunia utawala unayoitwa Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi ya Baba (CNSP). Mkuu wa Majeshi ya Jeshi la Niger Abdou Sidikou Issa alisema jeshi lilitangaza utiifu kwa vikosi vya ulinzi na usalama vilivyopindua Bazoum ili "kuepusha makabiliano mabaya kati ya vikosi mbalimbali".
Vuguvugu la M62
Kundi hilo la mashirika ya kiraia lilianza kushadidia maandamano ya kupinga Wafaransa katikati ya mwaka wa 2022, wakati serikali ya Bw Bazoum ilipodhinisha kuletwa tena kwa wanajeshi wa Ufaransa wa Barkhane nchini Niger baada ya kuagizwa kuondoka Mali.
Waliongoza wito dhidi ya utawala duni, kupanda kwa gharama ya maisha na uwepo wa vikosi vya Ufaransa. Maandamano yaliyopangwa na M62 yalipigwa marufuku au kukandamizwa kwa nguvu na mamlaka ya Niger na kiongozi wake Abdoulaye Seydou alifungwa jela kwa miezi tisa mwezi Aprili 2023 kwa "kuvuruga utulivu wa umma".
Kundi hilo linaonekana kuimarika baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Bazoum, na kuandaa maandamano katika mji mkuu wa Niger Niamey kuunga mkono mapinduzi hayo.
Mataifa jirani
Burkina Faso
Nchi jirani na Niger ambayo ilikumbwa na mapinduzi mawili Januari na Septemba 2022.
Uongozi wake wa kijeshi umeonya kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya viongozi wa mapinduzi ya Niger utachukuliwa kuwa "tangazo la vita" dhidi ya Burkina Faso.
Mamlaka ya kijeshi ya Burkinabei ilisema "inapinga utekelezaji" wa vikwazo "haramu, na ya kinyama dhidi ya watu na mamlaka ya Niger". Tangu mapinduzi yake, Burkina Faso imeegemea Urusi.
Mali
Nchi jirani na Niger, ambayo ilikumbwa na mapinduzi ya mwezi Mei 2021. Serikali yake ya kijeshi ilitoa taarifa ya pamoja na Burkina Faso kuunga mkono mapinduzi hayo.
Uongozi wa Mali ulisema uingiliaji wowote wa kijeshi dhidi ya Niger utakuwa "sawa na kutangaza vita" dhidi ya nchi zote mbili na unaweza kusababisha "matokeo mabaya" ambayo yanaweza "kuyumbisha eneo zima".
Mali inaungwa mkono na Urusi na kama Burkina Faso imejenga uhusiano wa karibu na Kremlin tangu mapinduzi yake.
Nigeria
Rais mpya wa Nigeria Bola Tinubu ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na mapinduzi ya Niger yatakuwa mojawapo ya changamoto zake kuu za kwanza za sera za kigeni. Nigeria inashiriki mpaka wa kilomita 1,500 (maili 930) na Niger kwa hivyo usalama wa nchi zote mbili umeunganishwa.
Tinubu alishiriki katika kampeni dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Nigeria katika miaka ya 1980 na kujiona kama mwanademokrasia.
Wole Ojewale, mchambuzi wa Nigeria katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama, anasema: "Nadhani anaona [mapinduzi] haya kama dharau kwa sifa zake za kidemokrasia, hasa wakati anashikilia uenyekiti wa Ecowas."
Tinubu alijibu kwa haraka mapinduzi hayo kwa kuitisha mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika Magharibi nchini mwake. Nigeria imepunguza usambazaji wake wa umeme kwa Niger kama sehemu ya vikwazo vilivyowekwa na Ecowas.
Chad
Chad si mwanachama wa Ecowas lakini kiongozi wake, Mahamat Idriss Déby Itno, alisafiri hadi Niger kuwataka watawala wa kijeshi kuzingatia makataa ya kambi ya kikanda ya kumrejesha madarakani Rais Bazoum.
Akiwa shujaa wa kijeshi mwenyewe, Bw Déby anaonekana kama mpatanishi muhimu ambaye anaweza kuwa na urafiki na viongozi wa mapinduzi ya Niger.
Jamii ya kimataifa
Kundi la Wagner
Kiongozi wa kundi la Wagner la mamluki wa Urusi, Yevgeny Prigozhin, ameripotiwa kulielezea mapinduzi hayo kuwa ushindi.
"Kilichotokea Niger si kingine bali ni mapambano ya watu wa Niger dhidi ya wakoloni wao," alinukuliwa akisema kwenye chaneli ya Telegram inayohusishwa na Wagner, ingawa maoni hayo hayajathibitishwa.
Mamluki wa Wagner wanashutumiwa kwa kutumia ushawishi mbaya nchini Niger.
Rais Bazoum alikuwa amelalamikia "kampeni za upotoshaji" za Wagner dhidi ya serikali yake kabla ya mapinduzi. Lakini Marekani imesema hakuna dalili kwamba vikosi vya Wagner vilihusika katika mapinduzi ya Niger.
Urusi
Ikulu ya Kremlin imesema kuwa hali ya Niger "inazua wasiwasi mkubwa" na imetoa wito kwa pande zote katika mzozo huo kujitathmini. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi Maria Zakharova alisema ni muhimu kuwe na "mazungumzo ya kitaifa kwa lengo la kurejesha amani na utawala wa sheria".
Baadhi ya wafuasi wa mapinduzi hayo walionekana wakipeperusha bendera za Urusi pamoja na bendera ya Niger.
Sasa kuna wasiwasi miongoni mwa waangalizi wa Magharibi kwamba uongozi mpya wa Niger unaweza kufuata nyayo za Mali na Burkina Faso na kujitenga na washirika wa Magharibi na kuwa karibu na Urusi.
Ufaransa
Mtawala wa zamani wa kikoloni wa Niger ana wanajeshi 1,500 nchini humo. Iligeukia Niger kuweka idadi kubwa ya vikosi vyake kufuatia mapinduzi ya Mali na Burkina Faso. Ufaransa imelaani vikali mapinduzi hayo.
Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa ilisema Rais Bazoum ndiye kiongozi pekee wa Niger na kwamba haitambui viongozi hao wapya wa mapinduzi.
Iliongeza kuwa Ufaransa "ilithibitisha kwa maneno makali zaidi matakwa ya wazi ya jumuiya ya kimataifa yanayotaka kurejeshwa mara moja kwa utaratibu wa kikatiba na serikali ya kiraia iliyochaguliwa kidemokrasia nchini Niger".
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Sébastien Lecornu alisema zaidi ya raia 1,000 wa Ufaransa na Wazungu wengine wamehamishwa kutoka Niger.
Marekani
Serikali ya Marekani imelaani vikali mapinduzi ya Niger, huku Waziri wa Mambo ya Nje Anthony Blinken akitoa wito wa kuachiliwa huru kwa rais huyo mara moja.
Marekani ina takriban wanajeshi 1,000 nchini Niger na imedumisha vikosi vyake nchini humo tangu 2013 kuunga mkono juhudi za kukabiliana na ugaidi.
Marekani ina kambi ya anga nje ya mji wa Agadez ambapo inaendesha operesheni za ndege zisizo na rubani. Agadez iko zaidi ya maili 500 kutoka Niamey, mji mkuu wa Niger. Marekani imeamuru kuhamishwa kwa sehemu ya ubalozi wake nchini Niger.
Ujerumani
Ujerumani ina taasisi ya ulinzi katika mji mkuu wa Niamey wa Niger. Imesitisha malipo yote ya moja kwa moja ya msaada kwa serikali kuu ya Niger hadi ilani nyingine itakapotolewa.
Ujerumani pia imeonya kwamba hatua zaidi zinaweza kuchukuliwa kulingana na jinsi mzozo huo unavyotokea.
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ilisema inafuatilia matukio nchini Niger kwa "wasiwasi mkubwa sana"
Uturuki
Tangu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Niger mnamo 1967, Uturuki imekuwa ikiimarisha uhusiano na nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema tangu kufunguliwa kwa ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Niger Niamey, mikataba 29 ya pande mbili imetiwa saini, na thamani ya biashara kufikia dola milioni 72 mwaka 2019.
Uturuki imetoa ndege zisizo na rubani kwa Niger na Mali pamoja na misaada ya kimaendeleo. Mnamo 2021, Niger ilipokea ndege sita zisizo na rubani za Uturuki aina ya Bayraktar katika mkataba wa silaha.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika taarifa yake: "Tunafuatilia kwa wasi wasi mkubwa jaribio la mapinduzi lililofanywa na kitengo cha Vikosi vya Wanajeshi nchini Niger."
Mashirika ya kimataifa
Umoja wa AfrikaAU, Umoja wa Ulaya,EU na Umoja wa Mataifa, UN zote zimelaani mapinduzi hayo.
AU ilitoa wito kwa jeshi la Niger kurejea kambini ndani ya siku 15, wakati EU imesimamisha shughuli zote za usalama nchini humo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea mshikamano wake na Rais aliyeondolewa madarakani Bazoum na kuwataka viongozi wapya wa kijeshi wa Niger kumwachilia huru bila masharti yoyote.