WARIDI WA BBC: 'Hasira ilivyonihangaisha maishani'

Chanzo cha picha, Liz Njau
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Liz Njau ni mke na mama wa watoto watatu kutoka nchini Kenya. Katika utu uzima wake akiwa na umri wa miaka 38 anasimulia matukio aliyokumbana nayo akiwa mdogo yalivyomuathiri vibaya kiakili akiwa mtu mzima.
Mwanadada huyu anasema kuwa wazazi wake walifanya kila wawezalo kuwalea yeye na ndugu zake kadiri ya uwezo wao kwa kuwapa mahitaji yao ya kimsingi.
Ila nyuma ya pazia, Liz alikuwa anapitia mahangaiko ya dhuluma za ndani ya familia na kulingana na simulizi yake alidhani kuwa ni kitu cha kawaida.
Japo aliwafahamisha wazazi wake baadhi ya matukio aliyokumbana nayo, na hatua kuchukuliwa katika kiwango cha familia hakujua kuwa makovu ya dhuluma hizo yalikuwa tayari yameathiri vibaya moyo wake.
“Unajua ukiwa mdogo unapitia mambo ambayo huelewi na wakati mwingine unaishia kufikiria ni hali ya kawaida kudhulumiwa na mtu wa karibu wa familia, ila katika utu uzima wangu nikirejesha mafikira nyuma nahisi nilipitia mambo ambayo hayakustahili,” anasema Liz.
Hasira ya kupitiliza
Baada ya kumaliza shule ya sekondari mwanadada huyu alifanikiwa kuingia katika taasisi moja jijini Nairobi.
Wakati akiwa chuoni alikutana na mtu ambaye walipendana na mambo yakaonekana kwenda vizuri kiasi cha kumtambulishampenzi wake kwa wazazi kwa ajili ya mipango ya kufunga pingu za maisha.
Ni wakati huo ndipo aligundua kwamba amepata ujauzito kabla hawajafunga ndoa.
Mwanamke huyu anasimulia kisa kilichotokea wakati alipoamua kukutana na mpenzi wake ili kumfahamisha kuhusu ujauzito wake.
Lakini habari hizo hazikupokelewa kama alivyotarajia, kwani mpenzi wake hakuwa tayari kuwa mzazi na aliishia kumshauri atoe mimba hiyo. Wazo ambalo Liz hakulichukulia kwa wepesi.
Anasema ghafla alipandwa hasira na kumgeukia mpenzi wake na kumgonga na kile kilichokuwa karibu naye.
“Nilichukua glasi iliyokuwa juu ya meza na kumrushia, nilimuumiza sehemu ya uso na kuzua vurugu,” Liz anasema.
Mwanadada huyu anakumbuka akimpigia simu baba yake na kumsimulia kile kilichotokea. Wazazi wake walikubali kumshughulikia na ujauzito wake hadi akajifungua.
Liz alimzaba kofi meneja wake usoni kwa hasira

Chanzo cha picha, Liz Njau
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya kujifungua Liz alifanikiwa kupata kazi na moyoni mwake akahisi kuwa mzigo mzito uliokuwepo umepungua.
Anasema kuwa alifanya kazi katika ofisi yenye mameneja wawili.
Mwanamke huyu anasimulia kisa ambacho kilifanyika siku mmoja kati ya meneja wake mmoja na kiliishia pabaya kwani katika purukushani za kujibizana kuhusu kazi, Liz alimzaba kofi usoni kwa hasira.
“Sikutarajia tukio kama hilo kazini. Nilikuwa nimejawa na hasira nisielewe ni kitu gani kinanisukuma. Baada ya hapo, nikaanza kuona kwamba nina hasira ambazo zilikuwa zinanifanya nisiishi vyema na watu waliokuwa karibu na mimi” Liz anakumbuka.
Visa hivi na baadhi ya visa vingine vingi alivyokabiliana navyo hadi wakati mmoja akaanza kujiuliza maswali kwa nini aliishi na machungu, hasira na kero za kila wakati.
Harakati za kujiuliza maswali hayo zilimuweka karibu na watu ambao pia walianza kuona ishara za mwanamke aliyekuwa na mahangaiko ya kiakili ambayo huenda ndio chanzo cha hasira zake japo hajawahi kumwambia mtu yeyote.
Lizz alifunga ndoa mwaka wa 2012, amejaaliwa watoto watatu na anasema kuwa ndoa sio lele mama hasa katika kipindi ambapo yuko kwenye hatua za kupona kutokana na hasira, kero na machungu maishani mwake.
“Nimekuwa mama ambaye najirekebisha kila uchao. Nakumbuka wakati watoto wangu walikuwa wananiogopa mno kutokana na hasira ambazo zingejitokeza wakati wowote nyumbani,” anasema Liz.
Hatua ya kujirekebisha

Chanzo cha picha, Liz Njau
Kwake Liz imekuwa ni safari ndefu akipiga hatua za kusamehe na kuachilia matukio ambayo hana udhibiti nayo,
Mwanadada huyu anasema dada yake ndiye aliyemweleleza hali halisi juu ya hisia alizokuwa nazo ambazo haziokuonekana za kawaida.
Liz anasema “usipopona maumivu yako, utaendelea kuelekeza hasira na machungu yako kwa watu wengine ambao hawajui ni nini kilichokuumiza.”
Matamshi haya kutoka kwa dada yake Liz yalimfanya abubujikwe na machozi hasa alipoanza hatua ya kujitathmini kwa undani na kung’amua kuwa kwa miaka kadhaa tangu akiwa msichana mdogo matukio ya dhuluma na hata kukataliwa na mpezi wake yalikuwa ni mojawapo ya mambo yaliyomfanya kuwa na hasira kupitiliza kwana hakujua la kufanya.
Ila aliamua kukubali hatma yake na kuanza safari ya kupona na kuanza kuachilia mambo ambayo hana uwezo wa kubadilisha.
Ni muda sasa tangu alipoanza hatua za kujirekebisha, kujikubali na vile vile kuondoa machungu ya kale na badala yake kujijaza na amani, furaha na hali ya kujikubali.
Liz Njau japo anafanya kazi na Huduma Ya Vijana kwa Taifa (NYS) kama sajenti kazi zake zingine ni kutoa ushauri nasaha, kuzungumza na watu katika jamii ambao wanaishi na changamoto za magonjwa ya kiakili na kadhalika.












