Sheria dhidi ya LGBT Uganda: Simulizi za waathiriwa wanavyopigwa na kulazimishwa kutoroka

By Pete Allison

BBC Newsbeat

Mwezi uliopita bunge la Uganda lilipitisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja unaomaanisha kuwa mtu yeyote anayejitambulisha kama LGBT anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Sehemu hiyo sasa imeondolewa katika toleo lililofanyiwa marekebisho lakini bado ni mojawapo ya sheria kali dhidi ya mapenzi ya jinsia moja barani Afrika.

Mswada huo mpya - ambao haujatiwa saini kuwa sheria na rais bado - umekosolewa vikali na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu.

Unaeleza adhabu ya kifo kwa kile inachotaja kuwa makosa makubwa kama vile unyanyasaji wa watoto.

Na wamiliki wa nyumba wanaokodisha majengo yao kwa ajili ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja pia wapo katika hatari ya kufungwa jela kwa miaka saba.

Mwezi uliopita, BBC ilifanikiwa kuingia katika makazi ya siri nchini Uganda ambapo watu wa LGBT wametafuta hifadhi baada ya kufukuzwa kutoka kwa nyumba zao.

Na sasa idhaa ya Newsbeat imezungumza na vijana wawili ambao wametoroka taifa hilo la Afrika Mashariki na kuelekea nchi jirani ya Kenya kwa sababu ya sheria hizo kali.

'Kitu kibaya kimeingizwa katika jamii'

Diane* - ambaye yuko katika miaka yake ya 20 - alitengwa baada ya watu kuibua tuhuma kuhusu mpenzi wake na kupitia simu yake.

Anasema mpenzi wake alipigwa kikatili, akiwemo na babake mzazi, kabla ya kumfuata na kumpiga pia yeye.

“Baba alikuja na wanaume wengine wawili, wakaanza kutupiga,” anasema.

“Nilipopata fahamu nikagundua wamefunga mlango na kuondoka na funguo.

"Walitufungia ndani ya nyumba kwa siku tatu."

Hatimaye wanandoa hao walifanikiwa kuwasiliana na rafiki yao mmoja kutoka jamii ya LGBT ambaye alikuja kuwaokoa.

"Ilibidi avunje kufuli," Diane anasema.

“Walitukuta na michubuko mingi, hatukuweza kutembea vizuri kwa sababu tulipigwa vibaya sana.

"Ilitubidi kuondoka nyumbani kwangu usiku kwa sababu hatukuweza kuondoka mchana.

"Maafisa wa usalama walianza kututafuta, kwa hivyo tulilazimika kujificha kwa rafiki huyo

Rafiki huyo aliwaruhusu wanandoa hao kukaa naye kwa wiki moja lakini hii ilikuwa wakati ambapo mswada wa kupinga LGBT ulikuwa ukipitishwa bungeni mwezi Machi.

Diane anasema walijua hawakuwa salama kwa hivyo walichukua tahadhari ya kutafuta usaidizi kwenye TikTok na Twitter.

Walikutana na akaunti ya Twitter ya Trans Rescue - ambayo husaidia watu kutoroka kutoka sehemu hatari duniani kote - ambao waliwasaidia kufika Kenya salama.

"Ni jambo la kutisha kuacha yote uliyoyajua - bila chochote - na kujaribu kuanza upya," anasema.

"Kitu kibaya kimeingia katika jamii. Tungeshambuliwa, tusingekuwa salama, Uganda haiko salama."

‘Tulitoroka kuokoa maisha yetu’

Jeff* ni Mganda mwingine aliyekimbilia Kenya baada ya kutengwa kama mpenzi wa jinsia moja

Alikuwa kwenye kongamano moja wakati bosi wake alipomwona akizungumza na mwanamume mwingine ambaye baadaye alikamatwa kwa kuwa mpenzi wa jinsia moja

Jeff, ambaye ni daktari anayejifunza taaluma hiyo, aliombwa aeleze uhusiano wake na mwanamume huyo.

Sawa na Diane, anasema waajiri wake walimfanya afungue simu yake na kupitia jumbe zake, kabla ya kuambiwa hawezi kusalia katika wadhifa wake.

Uvumi huo ulimfikia mwenye nyumba wake ambaye alimfukuza kwa sababu sheria mpya inamzuia kukodisha nyumba.

"Baada ya kufurushwa na uvumi huo kuanza kuenea, sikuweza kutembea wakati wa mchana," anasema.

"Nilipotembea mchana watu walikuwa wakinisaka .

"Siku hiyohiyo niliporudi nyumbani, nilishindwa kulala nyumbani."

Jeff, ambaye yuko katika miaka yake ya mapema ya 30, anasema hakuweza kuwasiliana na familia yake na ilibidi ajaribu kuishi bila kazi na mahali pa kuishi.

“Hawa watu walikuwa wakinitafuta ili kunipiga, walikuwa karibu na zahanati niliyokuwa nafanyia kazi,” anasema.

"Ndiyo sababu sikuweza kutembea mchana."

Jeff anasema alihisi hangeweza kumwamini mtu yeyote hivyo ilimbidi "kutoroka kuokoa maisha yake".

Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Kenya chini ya sheria iliyoanzishwa ilipokuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza - na mahakama yake kuu ilikataa jaribio la kubatilisha sheria hizo mwaka wa 2019.

Lakini Jeff anasema sasa anajisikia salama zaidi huko na haoni jinsi anavyoweza kurejea Uganda.

"Ninaamini kurejea Uganda si salama kwa sababu hakuna jinsi ningeweza kuishi huko," anasema.

Anahisi bunge la Uganda linaona mapenzi ya jinsia moja kuwa "tishio kwa utamaduni wao" na halitayumbishwa kirahisi na pingamizi ya kimataifa.

Wote Jeff na Diane wanakubali kwamba wanataka mustakabali usio na ubaguzi na unyanyasaji - hata kama kuna uwezekano wa kuwa nchini Uganda.

"Kwa kweli nataka tu kuishi kwa uhuru," asema Diane.

Anasema ameshuhudia tabia ya matusi na "kulaumiwa", huku watu wa LGBT wakiitwa "mashetani" na wapita njia, na anataka kuepuka hili.

Jeff anakubali: "Ninahitaji tu kuishi mahali ambapo niko huru kutekeleza haki zangu."

Anasema kutunza jinsia yako kwa siri kunaleta madhara makubwa.

"Unajificha tu, lazima ufanye kila kitu bila mtu kujua," anasema.

"Utakuwa unaficha tu jinsia yako ambayo inaweza kukusababishia kiwewe kikubwa."

*Majina yamebadilishwa ili kulinda utambulisho