'Mungu aliniumba na anajua kwanini mimi ni mpenzi wa jinsia moja'

    • Author, Patience Atuhaire
    • Nafasi, BBC News, Kampala

Bunge la Uganda wiki iliyopita lilipitisha mojawapo ya sheria kali zaidi duniani dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, na hivyo kuzua mjadala mkali. Ikiwa rais atatia saini mswada huo kuwa sheria, mtu yeyote anayejitambulisha kama LGBT anaweza kufungwa jela.

Pia inatishia kuwepo kwa hifadhi chache ambapo watu wa LGBT wametafuta makazi baada ya kufukuzwa nyumbani. BBC ilipata fursa ya kufika makazi hayo ya siri na ilizungumza na wakazi juu ya maisha na wasiwasi wao.

Ali alikuwa ameficha mwelekeo wake wa kijinsia lakini alifukuzwa baada ya kukamatwa wakati polisi wa Uganda walipovamia kisiri baa ya wapenzi wa jinsia moja katika mji mkuu, Kampala, mwaka wa 2019.

"Baba yangu alisema: 'Sitaki kukuona tena. Wewe si mtoto wangu. Siwezi kuwa na mtoto kama wewe,' anasema Ali, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake.

Licha ya kiwewe alichopata kutokana na tukio hilo kijana huyo, mwenye umri wa kati ya miaka 20, anaongea kwa upole na utulivu.

"Alikuwa akinitafuta ili anipige lakini mama aliniambia nijifiche, sikuwa na mpango, lakini nilijua lazima niondoke nyumbani."

Hadithi yake ya unyanyapaa, vurugu na woga inatoa taswira ya maisha ya watu wa LGBT nchini Uganda.

Mapenzi ya jinsia moja tayari yamepigwa marufuku nchini humo, lakini Mswada mpya wa Kupinga mahusiano ya jinsia unaenda mbali zaidi.

Hatua hiyo, ambayo bado inasubiri kuidhinishwa na rais kabla ya kuwa sheria, inaagiza kifungo cha maisha jela kwa mtu yeyote anayejitambulisha kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja, pamoja na adhabu ya kifo kwa unyanyasaji wa kingono wa watoto unaofanywa na wapenzi wa jinsia moja. Kubaka mtoto chini ya miaka 14, au kama mkosaji ana VVU, tayari ana adhabu ya kifo lakini hii haifanyiki mara chache.

Inaweza pia kusababisha kufungwa kwa makazi yoyote ambapo watu wameenda kutafuta usalama, kwani inafafanua kama kosa mtu yeyote anayekodisha mali "kwa madhumuni ya kufanya shughuli zinazohimiza mapenzi ya jinsia moja". Pia zinaweza kutafsiriwa kama danguro.

Baada ya kutoroka nyumbani kwao miaka minne iliyopita, Ali alifahamishwa kuhusu mahali ambapo angeweza kuishi kwa usalama wa kadiri ambayo pia ilitoa chakula na kufanya jitihada za kutafuta kazi kwa wapenzi wa jinsia moja wasio na makazi.

Mfanyikazi wa zamani wa mkahawa alikuwa amekuwepo kwa miezi michache tu wakati amri ya kutotoka nje ili kuzuia kuenea kwa corona ilipoanza kuzingatiwa.

"Mnamo 2020, makao hayo yalivamiwa na polisi. Tulipanga mstari na watu waliitwa kututazama, kutudhihaki na kutudhalilisha. Watu walikuwa wakitutemea mate," Ali anaiambia BBC.

Yeye na wanaume wengine zaidi ya 20 walikamatwa, kushtakiwa mahakamani kwa kukiuka vikwazo vya janga la corona la kuzuia mikusanyiko, na kupelekwa gerezani.

"Tulipowasili gerezani, baadhi ya wafungwa tayari walikuwa wanajua hadithi yetu, walikuwa wameisoma kwenye magazeti, ilibidi tukane kwamba sisi ni wapenzi wa jinsia moja ili tuwe salama," aeleza.

Tabia yake ya urafiki inakanusha kiwewe anachosema alikumbana nacho alipokuwa kizuizini.

"Mlinzi wa gereza ambaye alikuwa ameona maelezo ya kesi yetu aliamuru wafungwa wengine watupige, naye akajiunga, marafiki zangu wengine walichomwa sehemu zao za siri na makaa ya kuni, tulipigwa kwa takriban masaa matatu, kwa waya na mbao. ya mbao," anasema, akionyesha makovu kwenye mikono yake.

Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini Uganda Frank Baine anakanusha kuwa watu hao walivamiwa wakiwa kizuizini. "Walipokuwa huko, hawakujulikana kama mashoga [wanaume]. Hakuna mtu aliyewatesa na kulingana na afisa mkuu, hakukuwa na alama za kuteswa. Waliwekwa rumande hadi walipopewa dhamana," anaambia BBC.

Baadaye serikali ilifuta mashtaka dhidi ya kundi hilo, na waliachiliwa baada ya siku 50. Ali alihamia kwenye makazi mengine tena.

Zaidi ya nyumba 20 kama hizo zipo kote Uganda, zikifanya kazi kwa viwango tofauti vya usiri.

"Kwa kawaida tuna watu wapatao 10 hadi 15 katika makazi wakati wowote," anasema John Grace, mratibu katika Muungano wa Uganda Minority Shelters Consortium.

Watu wengi wa LGBT hupata usalama na hisia ya kuthaminiwa katika nyumba hizi za muda. Lakini hata hapa, hatari haiko mbali.

Ali anaeleza jinsi alivyoshambuliwa mwezi Novemba mwaka jana.

"Kundi la vijana lilianza kunifuata na kupiga kelele: 'Nyinyi wapenzi wa jinsia moja, tutawaua.' Sikuitikia nikaendelea kutembea.Mmoja akanipiga kichwani kwa nyuma.

"Nilipopata fahamu, nilikuwa hospitalini na nilikuwa na michubuko usoni kote na jeraha kubwa nyuma ya kichwa changu."

Nilipelekwa kwenye makao hayo, ambayo ameyaita nyumbani kwa miaka mitatu iliyopita, kupitia barabara za nyuma kuelekea mtaa wa kaskazini mwa Kampala. Wakazi wanakuwa waangalifu kuhusu ufichuzi wa eneo hilo.

Nyumba hiyo, ambayo mmiliki anaonekana kuwa aliianzisha kama nyumba ya familia imeanza kuchujuka kwani rangi yake imeharibika katika sehemu kadhaa. Iko kwenye eneo lenye lango lililotiwa kivuli na miti mikubwa ya muembe na mikoko, ambayo chini yake kuna nguo zilizoanikwa ili kukauka.

Kando na jikoni ambayo imejaa sahani, karibu kila mahali katika nyumba hiyo inatumika, ikiwa ni pamoja na karakana, imebadilishwa kuwa vyumba vya kulala.

Hisia za machafuko ni matokeo ya moja kwa moja ya uwezekano wa Mswada wa Kupinga Wapenzi wa jinsia moja kuwa sheria.

"Baada ya mswada huo kupitishwa, mwenye nyumba alituambia tuhame. Msimamizi wa makao hayo amesema kwamba tunapaswa kuwa na kila kitu tayari atakapopata nyumba mpya," Ali anaiambia BBC

Lakini matarajio si mazuri.

"Endapo wakaaji wa sasa wa makazi watafukuzwa na mwenye nyumba, hatuna chaguo lingine," anakiri Bw Grace kutoka kundi la makao hayo.

Zaidi ya hayo, kundi lake litakuwa hatarini siku zijazo.

"Ikiwa mswada huo utatiwa saini na rais, tunaweza kukabiliwa na mateso ya kisheria, ghasia, ubaguzi na unyanyapaa kwa ajili ya kupata makazi salama kwa watu walio katika mahusiano ya jinsia moja wasio na makazi na pia kujitambulisha kama wapenzi wa jinsia moja," anaongeza.

Tim - sio jina lao halisi - ni miongoni mwa wakazi wengine wa nyumba hii. Wazazi wake waliacha kumlipia karo ya chuo kikuu baada ya kufukuzwa. Baba yake mchungaji aliwakata kabisa.

Tim anakumbuka hatua ya chini kabisa.

"Nilifanya kazi ya ngono, nikilala na wanaume tofauti ili tu nipate chakula. Siku zingine nilijichukia. Ningeenda kuoga na kujisugua kama mara 10.

"Sikuwa na matumaini - nilikuwa nimepoteza familia yangu, nimepoteza elimu, nimepoteza mwelekeo."

Tim alikua mwathirika wa unyanyasaji wa mtandao siku ambayo Mswada wa Kupinga Mapenzi ya Jinsia moja ulipojadiliwa bungeni.

"Watu walikuwa wakinitumia ujumbe, wakisema: 'Ona kitakachokupata?'

“Baadhi yetu tulikuwa tumeanza kupata nafuu kidogo ya afya zetu za kiakili, sasa inanitia hofu kuwa sehemu kama hii inaweza kuwekwa alama ya danguro, nahisi tulikuwa na jeraha ambalo lilikuwa linaanza kupona na sasa limechanwa. ," Tim anaiambia BBC, akionekana kudhoofika.

"Sioni kama tunaweza kurejesha hali yoyote ya utu kwa sasa kwa sababu ya chuki ambayo imekuwa ikienezwa dhidi yetu."

Uganda tayari ni miongoni mwa nchi 32 za Afrika zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja kati ya watu wazima.

Mswada huo umelaaniwa vikali kimataifa, huku Marekani ikisema huenda ikazingatia vikwazo dhidi ya nchi hiyo, na Umoja wa Ulaya ukisema kuwa ni unapinga hukumu ya kifo kwa kila hali.

Makundi ya wanaharakati wa ndani na kimataifa pia yamejiunga na kilio hicho.

Alipoulizwa anapanga kufanya nini ikiwa makazi hayawezi kupata mahali pa kuhamia, sauti ya Ali ilififia kwa unyonge alisema, "Wazo lililo akilini mwangu ni: 'Nitaenda wapi?'

"Kila mtu anasema sisi sio watu wa kawaida, kwamba sisi sio wanadamu. Lakini hivi ndivyo nilivyo. Nimefikiria kurudi nyumbani, lakini baba yangu hawezi kuniruhusu kurudi nyumbani kwake," anasema.

Ili kupata msingi, Ali anashikilia imani yake ya Kiislamu.

"Najua Mungu ndiye aliyeniumba na anajua kwa nini mimi nashiriki mapenzi ya jinsia moja. Kwa hiyo naendelea kuomba. Hata sasa [wakati wa Ramadhani] nafunga," anasema.

Pia uanaweza kusoma: