Neymar kwenda Al-Hilal: Kwa nini Saudi Pro League inawasajili nyota wa klabu za Ulaya?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema msimu huu Gary Neville alitoa wito kwa Ligi Kuu ya `Premia kusitisha uhamisho wa wachezaji kwenda Saudi Arabia kwa sababu za "uadilifu", lakini inaendelea kuwa hadithi kubwa zaidi ya kandanda katika msimu huu.
Al-Hilal waliwashangaza wengi kimataifa kwa kutoa rekodi ya dunia ya £259m kwa Kylian Mbappe wa Paris St-Germain, huku nahodha wa Liverpool Jordan Henderson akiamua kuhamia Al-Ettifaq ya Steven Gerrard.
Mchezaji mwenzake wa zamani wa Henderson, Fabinho amehusishwa na kiungo wa zamani wa Chelsea, N'Golo Kante katika klabu ya Al-Ittihad, huku Manchester City wakimuuza Riyad Mahrez kwa Al-Ahli kwa pauni milioni 30 na Al-Nassr wakimleta beki wa pembeni Alex Telles kutoka Manchester United. Na sasa kiwango cha Ligi Kuu ya Saudi kimefikia kilele kingine.
Al-Hilal wanaonekana kukaribia kukamilisha moja ya matukio makubwa zaidi katika dirisha la usajili baada ya kukubali dili la kumnunua nyota wa Brazil Neymar kutoka PSG kwa pauni milioni 77.6, pamoja na nyongeza.
Kiasi cha uhamisho, pesa zinazolipwa na majina ya wachezaji wanaohama, yote yanadhihirisha azma ya ligi hiyo kuwa mojawapo ya mashindano bora zaidi duniani katika miaka michache ijayo.
Beki wa zamani wa Manchester United na England Neville, hata hivyo, ni miongoni mwa wale ambao wameuliza nini maana ya shughuli hii yote.
Mwezi Juni, Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF), ulithibitisha kuchukua vilabu vinne vinavyoongoza nchini, ikiwa ni pamoja na Al-Nassr, iliyomsajili Cristiano Ronaldo mwezi Desemba.
Kuna sintofahamu juu ya iwapo PIF inamiliki hisa miongoni mwa wamiliki wa mwisho wa Chelsea, kampuni ya kibinafsi ya Clearlake Capital, ingawa vyanzo vya klabu vimekataa mapendekezo ya kuhusika moja kwa moja.
Na kulikuwa na wasiwasi zaidi baada ya Newcastle United kumuuza Allan Saint-Maximin kwa Al-Ahli, ambayo inasimamiwa na PIF ya nchi hiyo - ambayo pia inamiliki klabu hiyo ya Tyneside.
Lakini wakati Neville ametoa wito wa "kuzuiliwa mara moja" kwa shughuli ya uhamisho wa Saudi, mkuu wa Ligi ya Premia Richard Masters aliiambia BBC Sport mwezi Julai kwamba sheria zake za kuzuia ada za uhamisho zilizopanda ni "kubwa".
Masters alisema "hakuwa na wasiwasi sana" na akasisitiza vilabu vya Saudi vina "haki kubwa ya kununua wachezaji kama ligi nyingine yoyote".
Aliongeza: "Wanawekeza kwa wachezaji na wasimamizi ili kujaribu kuinua hadhi ya ligi na klabu.
"Imetuchukua miaka 30 kufikia nafasi tuliyonayo kwa wasifu, ushindani na njia za mapato tulizonazo."
Suala la kifedha

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ruben Neves alikuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa Wolves na pia alikuwa akinyatiwa na Barcelona.
Ongezeko la matumizi ya fedha za Saudi Arabia limekuja wakati huo huo huku baadhi ya klabu za Uingereza zikikabiliwa na changamoto ya kusawazisha vitabu vyao vya kifedha.
Chelsea na Wolves wamekabiliwa na maamuzi magumu kuhusu kuajiri wachezaji msimu huu huku wakijaribu kuweka ndani ya kikomo cha miaka mitatu cha Premier League cha hasara ya £105m chini ya sheria za Financial Fair Play (FFP).
Chelsea walitumia zaidi ya pauni milioni 400 katika uhamisho wa msimu uliopita, huku Wolves wakipoteza kwa pauni milioni 46.1 mwaka jana na mkufunzi wa zamani Julen Lopetegui alisema klabu hiyo ilihitaji "kusuluhisha" masuala ya FFP ili kushindana katika ligi kuu.
Wolves walidhani Neves angejiunga na Barcelona msimu huu wa joto. Hata hivyo, ada ya £47m iliyokubaliwa na Al-Hilal kwa kiungo huyo wa Ureno ilikuwa kubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Vyanzo vya Chelsea vinasema kuwa PIF ya Saudi Arabia haina "maslahi yoyote, kifedha au vinginevyo" katika klabu hiyo.
Haijawahi kukataa kuwa PIF inahusika na Clearlake lakini imesisitizwa kuwa kampuni hiyo ya hisa kutoka Marekani ina wawekezaji 400 tofauti katika mabara sita na inadhaniwa hakuna mtu anayemiliki zaidi ya 5% ya hisa
Umiliki wa klabu nyingi haujapigwa marufuku na shirikisho la Uefa ambalo hadi sasa limekataa kuzungumzia lolote.
Ligi ya Premia ina mfumo wa kutathmini thamani ya haki ili kujaribu kuhakikisha mikataba, ya kibiashara na uhamishaji, inafanywa kwa thamani ya soko. Mfumo wa kulinganisha wa uhamishaji wa Fifa umeundwa kufanya vivyo hivyo.
Lengo, hatimaye, ni kuhakikisha sheria zinafuatwa. Hakuna kazi rahisi, ikizingatiwa kuwa masoko hubadilika-badilika, na thamani ya mchezaji inaweza kubadilika.
Je, Saudi Pro League italeta athari kubwa kwenye soko hilo?
Je, ligi ina asili gani?
Saudi Arabia daima imekuwa na hamu kubwa katika soka – mbali na kumiliki ligi yenye ushindani mkubwa.
Timu ya taifa imefuzu kwa fainali sita kati ya nane zilizopita za Kombe la Dunia. Wameshinda vikombe vitatu vya Asia - ni Japan pekee iliyo na zaidi.
Katika Kombe la Dunia la Qatar mwaka jana, wachezaji wote 26 wa kikosi hicho walichezea klabu za nyumbani. Hakuna klabu iliyoshinda Ligi ya Mabingwa ya AFC mara nyingi zaidi ya klabu ya Al-Hilal ambayo iliibuka mshindi mara nne.
Katika miaka ya hivi majuzi, Saudi Arabia imekuwa mwonekano zaidi kwenye uwanja wa michezo, ikiandaa mbio za Formula 1 na ngumi za ndondi za ubingwa wa ulimwengu na pia kuanzisha LIV Golf.
Ununuzi wa kutatanisha wa Newcastle ulikuwa ushahidi zaidi wa kuongezeka kwa nia ya kutumia michezo kuionyesha Saudi Arabia kwa hadhira kubwa. Zabuni ya pamoja ya Kombe la Dunia la 2030 na Misri na Ugiriki imepangwa pia.
"Saudi Arabia inajiona kuwa kitovu cha utaratibu mpya wa dunia na kuwekeza katika michezo kunasaidia kuchangia katika nafasi hiyo ya kitaifa," Simon Chadwick, profesa wa michezo na uchumi wa kijiografia katika Shule ya Biashara ya Skema mjini Paris, alinukuliwa akisema hivi karibuni.
Kuboresha ligi ya Saudi Arabia ni sehemu ya mpango huo - kwa usaidizi wa majina ya hali ya juu.
Fowadi wa zamani wa Leeds na Wolves Helder Costa, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Argentina Ever Banega na mshambuliaji wa zamani wa Watford na Manchester United Odion Ighalo wote walishiriki msimu uliopita, wakati Al-Ittihad, inayonolewa na kocha wa zamani wa Wolves na Tottenham Nuno Espirito Santo, ilipomaliza kama mabingwa.
Je, hii ni Ligi nyingine ya Uchina?
Wakati ligi inakuwa mchezaji mkubwa katika soko la uhamisho la dunia, maswali kuhusu uendelevu wake wa kifedha yatafuata.
Ligi Kuu ya Uchina, kwa kipindi kifupi, ilivutia watu wengi na ililipa pesa nyingi kuvutia wachezaji wa hadhi ya juu, kama vile mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na City Carlos Tevez.
Viwango kama hivyo vya matumizi havikudumu.
Lakini Saudi Pro League inaamini kuwa imejengwa kwa misingi imara zaidi.
"Ligi imeimarika vyema, inaendelea tangu miaka ya 1970, na klabu zina mashabiki wa kweli wanaojali soka ambalo linaifanya kuwa ya kweli na sio ya usanii," chanzo cha ligi kuu kiliiambia BBC Sport.
"Ilipotokea Uchina, haikuwa pesa za serikali kwa uwazi, ilikuwa ni kuhimiza wajasiriamali kufanya mambo. Kisha ikakoma.
"Hapa ufadhili ni salama zaidi na ni sehemu ya mpango wa muda mrefu. Klabu zimeimarika katika jamii na mpira wa miguu nchini kote ndio mchezo nambari moja.
"Pamoja na kwamba ligi ina wachezaji wengi wa kigeni, ni nyota wakubwa ambao wanapata matangazo ya televisheni duniani kote.
Mara tu Ronaldo alipoingia, ligi ilianza kuonyeshwa katika kila soko kubwa. Inapata tahadhari hiyo mara moja.
"Tangazo kwamba klabu vnne bora zitamilikiwa na PIF kwa 75%, badala ya serikali, inazigeuza kuwa biashara inayofaa.
"Sio tu kuleta wachezaji wa juu lakini pia kubadilisha uchumi wa mchezo ili kuimafrisha sekta ya kibinafsi zaidi na kukuza klabu na kampuni na chapa.
"Uhamisho wa Ronaldo ulithibitisha kuwa unaweza kutokea. Ni jambo moja kusema 'tutasajili wachezaji bora zaidi duniani' lakini kwa mtu wa hadhi ya Ronaldo kuja, kuishi Riyadh na kucheza kila mchezo, ilikuwa ni mshangao kwa watu na kuonyesha tunaweza kupata wachezaji wengine kuja kujiunga na ligi hii."

Chanzo cha picha, reuters
Je, Ulaya ina wasiwasi kuhusu upungufu wa vipaji?
Kwa soka la Ulaya, kupanda kwa ligi ya Saudia kunaleta changamoto.
Kupoteza wachezaji muhimu sio jambo geni - Uchina na Ligi Kuu ya Marekani zimejaribu kufanya hivyo hapo nyuma. lakini, kuondoka kwa wachezaji katika ubora wao, kama vile Neves, ni jambo la kutia wasiwasi.
Hata kati ya 20 bora katika orodha tajiri ya Deloitte, fedha hazina kikomo na kanuni za kifedha zinapaswa kuzingatiwa. Iwapo watajaribu kushindana kwa muda mrefu, itaathiri gharama kubwa ya klabu - mishahara.
Na vipi kuhusu Ligi ya Mabingwa? Ikiwa ubora wake kama shindano la klabu ulianza kudhoofishwa na kukosekana kwa wachezaji wenye majina makubwa duniani, je, vkabu kutoka nje ya Ulaya zinaweza kupewa viingilio?
Rais wa Uefa Aleksander Ceferin haoni hivyo.
"Ni makosa kwa soka la Saudi Arabia," aliambia shirika la utangazaji la Uholanzi NOS. "Wanapaswa kuwekeza kwenye akademi, kuleta makocha wao na kukuza wachezaji wao.
"Mfumo wa kununua wachezaji ambao wanakaribia mwisho wa maisha yao sio mfumo wa kuendeleza soka. Ilikuwa ni makosa sawa na China wakati wote walinunua wachezaji ambao walikuwa wanaelekea kumaliza vipaji .
"Sio tu kuhusu pesa. Wachezaji wanataka kushinda mashindano ya juu. Na mashindano ya juu ni Ulaya."












