Ugomvi wa marais ambao hata kifo hakikuweza kuumaliza

Chanzo cha picha, AFP
Inawezekana ugomvi huo ulikuwa ni suala binafsi lakini limegeuka kuwa jambo la kisiasa nchini Zambia.
Maombolezo na maandalizi ya mazishi si jambo rahisi, lakini ukiongeza mzozo wa muda mrefu kati ya wanasiasa wawili wakuu wa nchi hiyo, Rais Hakainde Hichilema na mtangulizi wake marehemu Edgar Lungu, hapo unapata hali ya mivutano mikubwa.
Uhasama ulikuwa mkubwa kiasi kwamba familia ya Lungu ilisema moja ya matakwa yake ya mwisho kabla ya kufariki ilikuwa kwamba Hichilema asikaribie mwili wake hata kidogo.
Mzozo huu umevuruga mipango ya serikali ya kumuenzi rais huyo wa zamani, vilevile ukaleta mpasuko wa kihisia nchini humo kwa kuwaacha wananchi wakijiuliza mambo yalifikaje hapo.
Jumapili ilikuwa siku iliyopangwa kufanyika mazishi ya kitaifa ya kiongozi huyo aliyefariki akiwa na miaka 68, ambaye aliiongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia mwaka 2015. Lakini shughuli hiyo haitakuwepo na wageni mashuhuri, wala ukumbi mkubwa wa mikutano katikati ya mji mkuu, Lusaka – utabaki kuwa mtupu.
Dalili za mvutano zilianza kujionyesha mara baada ya kifo cha Lungu tarehe 5 Juni, kupitia ujumbe wa video uliowekwa na binti yake kwenye Facebook.
Akiwa amevaa koti jeusi zito huku akijizuia kulia, Tasila Lungu alisema baba yake alifariki katika hospitali nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akipatiwa matibabu kwa "heshima na faragha".
Katika tangazo la dakika moja alisema 'katika wakati huu wa majonzi tukiwa na ari ya Zambia Moja, Taifa Moja' kauli isiyopitwa na wakati iliyomuongoza Rais Lungu katika kulitumikia taifa letu."
Alilenga kuonesha haja ya mshikamano katika wakati ambapo mila zilitarajia taifa lionekane likiwa limeungana , jambo ambalo lilikuwa ishara kuwa hali haikuwa shwari.

Chanzo cha picha, RF
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Na swali lilikuwa yu wapi rais kutangaza?
Kauli ya Bi Lungu ilithibitisha uvumi wa mitandaoni kuhusu kifo cha baba yake. Ujumbe wa rambirambi ulikuwa tayari umeanza kutumwa, ikiwemo kutoka kwa Rais wa Kenya, lakini hakukuwa na taarifa yoyote kutoka kwa Rais Hichilema.
Wakati vyombo huru vya habari vilikuwa vikitoa taarifa hizo, shirika la taifa la utangazaji, ZNBC, lilibaki kimya.
Kisha, saa tatu baada ya ujumbe wa binti yake, kiongozi wa taifa la Zambia alishiriki mawazo yake kupitia chapisho la maandishi kwenye Facebook. Alitoa wito wake binafsi wa mshikamano, akiwataka wananchi "kudumisha maadili ya amani, heshima na umoja yanayotutambulisha kama Wazambia."
Waziri wa Habari, Cornelius Mweetwa, alipuuzia wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa Rais Hichilema kuzungumzia kifo hicho. Aliiambia BBC kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa awali, haikuwa wajibu wa kiongozi wa sasa kutangaza kifo cha mtangulizi wake.
Hata hivyo, wafuasi wa Lungu walihisi kuwa ujumbe wa Hichilema wa "umoja" haukuwa wa kweli.
Hichilema alifanikiwa kuwa rais katika jaribio lake la sita baada ya kumshinda Lungu kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2021. Huo ulikuwa ni mchuano wao wa tatu wa kisiasa, lakini uhasama wao ulizidi ushindani wa kisanduku la kura.

Chanzo cha picha, AFP
Msingi wa kuelewa hali hii ni siku zaidi ya 100 ambazo Hakainde Hichilema, akiwa kiongozi wa upinzani wakati huo, aliwekwa rumande mwaka 2017 akisubiri kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya uhaini.
Alishtakiwa kwa kuhatarisha maisha ya Rais wa wakati huo, Edgar Lungu, baada ya msafara wake kudaiwa kukataa kumpisha msafara wa rais barabarani.
Mashtaka hayo yalifutwa tu baada ya kuingilia kati kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola.
Baadaye mwaka huo, Hichilema aliiambia BBC kuwa alifungwa katika mazingira ya udhalilishaji na kinyume na haki za binadamu kwa siku nane za kwanza akiwa peke yake "bila umeme, bila maji, wala choo". Alimlaumu Lungu binafsi kwa kifungo hicho.
Hicho kilikuwa ni kisa kimoja tu kati ya mara 17 ambazo Hichilema alikamatwa. Wafuasi wa chama chake cha United Party for National Development (UPND) pia walikumbwa na vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa wafuasi wa chama tawala cha Patriotic Front (PF).
Uchaguzi wa mwaka 2021 ungeweza kuwa mwisho wa yote haya.
Lungu, ambaye alikataliwa na wapiga kura kwa tofauti ya karibu kura milioni moja kutokana na tuhuma za ufisadi na hofu kuhusu mienendo ya kidikteta, alijiondoa kwenye siasa za moja kwa moja.
Lakini kutokana na kuongezeka kwa hali ya kutoridhika na utawala wa Hichilema, hasa kutokana na ugumu wa maisha ya kiuchumi, Lungu aliona fursa na mnamo Oktoba 2023 alitangaza kurejea kwenye siasa za mstari wa mbele.
Muda mfupi baada ya tangazo hilo, serikali ilimvua Lungu mafao na stahiki zake za kustaafu kwa sababu alirudi kwenye siasa.
Uamuzi huo uliwakera sana Lungu na familia yake.

Chanzo cha picha, andy lucky
Lungu pia alilalamikia kunyanyaswa na polisi. Wakati mmoja mwaka jana, alisema alikuwa "karibu sawa na kuwa chini ya kifungo cha nyumbani."
Mwaka 2023, polisi walimwonya Lungu dhidi ya kufanya mazoezi ya kukimbia hadharani, wakielezea mazoezi yake ya kila wiki kama "harakati za kisiasa".
"Siwezi kutoka nje ya nyumba yangu bila kukamatwa au kuzuiwa na polisi na kurudishwa nyumbani kwa nguvu," Lungu aliiambia BBC mwezi Mei 2024.
Katika mahojiano hayo, pia alidai kuwa alizuiwa kuhudhuria mkutano nje ya nchi na kunyimwa kibali cha kusafiri kwenda nje kwa ajili ya matibabu.
Waziri wa Habari, Cornelius Mweetwa, alikanusha vikali madai hayo, akisema kuwa haijawahi kuwepo marufuku ya kusafiri dhidi ya Lungu, na kueleza hoja kwamba alikuwa akizuiwa kusafiri ndani ya Zambia kuwa ni "hadithi ya kubuniwa na mawazo yenye misukumo ya kisiasa".
Mweetwa aliongeza kuwa licha ya kile Hichilema alichopitia akiwa upinzani, amedhamiria kutomfanyia Lungu mambo kama hayo.
Kuna pia tuhuma kuwa kampeni ya rais ya kupambana na rushwa imelenga watu wa karibu wa chama kilichokuwa kikitawala cha Patriotic Front (PF), akiwemo familia ya Lungu.
Mjane wake, ambaye bado anachunguzwa na mamlaka, amefikishwa mahakamani na kupoteza baadhi ya mali. Baadhi ya watoto wake, akiwemo Tasila, nao pia wamekumbwa na hali kama hiyo, wote wanakanusha kuhusika na makosa yoyote.
Kisha mwishoni mwa mwaka jana, Mahakama ya Katiba ilimpiga marufuku Lungu kugombea tena urais, ikiamua kuwa tayari alishahudumu kwa mihula miwili ambayo ndiyo kikomo kinachoruhusiwa kisheria.
Rais huyo wa zamani alikasirishwa na namna alivyohisi ametendewa.
"Hakukuwa na mapenzi kati ya wanaume hao wawili, na [Lungu] aliamini kwamba: 'Sitaki watu wajifanye wananijali baada ya kufa, ilhali walinidharau nikiwa hai'," alisema wakili wa familia hiyo, Makebi Zulu.
Hatimaye, Lungu alifanikiwa kusafiri hadi Afrika Kusini mwezi Januari, lakini Bw. Zulu alisema madaktari wake walimwambia kuwa iwapo angefika mapema kwa uchunguzi, matibabu yangekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa.
Haikufahamika alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani.
Kwa sehemu, kutokana na hilo, Lungu alisisitiza kwamba "hataki rais wa sasa kuhudhuria mazishi yake."
Serikali, hata hivyo, imekanusha madai kwamba Lungu alizuiwa kusafiri kwenda kuwaona madaktari wake Afrika Kusini.
Baada ya kifo chake, familia ya Lungu ilitaka iwe na mamlaka kamili juu ya maandalizi ya mazishi, lakini mamlaka za Zambia zilijaribu kuchukua udhibiti.
Licha ya uhusiano mbaya, mwishoni mwa wiki iliyopita ilionekana kana kwamba pande zote mbili zilifikia mwafaka na mipango ya mazishi ya kitaifa ikawekwa.
Hata hivyo, hali iliharibika tena baada ya familia kudai kuwa serikali ilikiuka makubaliano kwa kutoa ratiba ya mazishi iliyomuonyesha Rais Hichilema kushiriki zaidi ya ilivyopangwa awali.
Katika ujumbe wake siku ya Alhamisi, rais aliwashukuru Wazambia kwa "ustahimilivu, uvumilivu, mshikamano na utulivu katika kipindi hiki," lakini akaongeza kuwa baada ya "kufanya kila linalowezekana kuwasiliana na familia... tumefikia hatua ambayo uamuzi wa wazi lazima ufanyike."
Kwa mantiki hiyo, maandalizi ya mazishi nchini Zambia yalielekezwa kusitishwa, na kipindi cha maombolezo ya kitaifa kilikatizwa ghafla.
Sasa, mazishi yanatarajiwa kufanyika Afrika Kusini, na inaonekana kuwa ni vigumu kwa Rais Hichilema kuhudhuria.
Wazambia walikuwa na matumaini kwamba Hichilema na Lungu wangeweza kuzikwa tofauti zao, lakini kifo hiki na matukio yaliyofuata yamewanyima wananchi fursa hiyo ya maridhiano na kufunga ukurasa huo kwa amani.
Tofauti hizo pia zimewanyima mamilioni ya Wazambia nafasi ya kumuaga na kumpa heshima ya mwisho mtu ambaye aliwahi kuwaongoza.
Imetafsiriwa na Esther Namuhisa












