Jinsi vita vilivyoumiza matumaini ya Olimpiki ya Ethiopia

    • Author, Girmay Gebru
    • Nafasi, BBC Tigrinya
    • Akiripoti kutoka, Tigray
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Redae Gebreyesus angeweza kuiwakilisha Ethiopia kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris, lakini maisha yake yaliharibiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwanariadha huyo mwenye talanta ya mbio za kati aliuawa mwishoni mwa 2020, siku chache baada ya mzozo wa Tigray kuanza mwezi Novemba mwaka huo.

Tigray, jimbo la kaskazini mwa taifa hilo la Afrika Mashariki, ni nyumbani kwa wanariadha muhimu wa Ethiopia. Theluthi moja ya timu ya taifa ya nchi hiyo inayoshiriki mashindano katika mji mkuu wa Ufaransa inatoka katika eneo hilo.

Kulingana na kocha wake, Gebreyesus alikuwa na uwezo wa kuwa sehemu ya kikosi hicho - kama si vita vya umwagaji damu vya miaka miwili kati ya serikali ya Ethiopia na waasi katika eneo hilo.

"Bilashaka Redae, angeshinda medali," Getye Mekuria aliiambia BBC Tigrinya.

Mapigano yalimalizika baada ya serikali ya Ethiopia na Chama cha Ukombozi cha Watu wa Tigray walipotia saini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Umoja wa Afrika mwezi Novemba 2022.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Ghent unakadiria watu 600,000 wamekufa kwa sababu ya vita, huku zaidi ya milioni mbili wakikimbia makazi yao na karibu 900,000 wakilazimika kuwa wakimbizi.

Katika mji wa Edaga Arbi, kilomita 25 kutoka mpaka na Eritrea, mamake Gebreyesus bado anaomboleza kifo cha mwanawe.

"Nimepoteza kila kitu," anasema Hadera Seyum akiwa nyumbani kwake.

“Hata hivyo, nina watoto wake. Kama asingekuwa na mtoto, ningejiona sina kitu.”

Pia unaweza kusoma

Angekuwa nembo ya taifa

Gebreyesus alipata mafunzo katika kituo kikuu cha riadha cha Tigray huko Maychew na alishinda medali zinazoshindaniwa katika eneo la kikanda.

Alitiwa moyo na Hagos Gebrhiwet na Letesenbet Gidey, wakimbiaji wenzake kutoka eneo hilo ambao wameshinda medali za shaba katika Olimpiki ya mita 5,000 na 10,000 kila mmoja.

"Nakumbuka alianza mafunzo mwaka 2006," anasema mama yake mwenye machozi.

"Alikimbia mara tu baada ya kutoka shule, kabla ya kurudi nyumbani. Pia aliamka asubuhi mapema kwenda kwenye mafunzo.

“Alisema atafika kiwango cha juu sana. Aliahidi ataibadilisha familia yake.”

Gebreyesus, alifanya kazi ya ujenzi na kutengeneza vifaa kwa ajili ya kilimo kwa kutumia chuma. Alikuwa nyumbani siku wanajeshi waliposhambulia kijiji chake tarehe 19 Novemba 2020.

Mama yake na dada yake walipokimbia, alibaki kusaidia vikosi vya Tigrayan kulinda ardhi yao. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho familia yake kumwona.

Mjane wa Gebreyesus, alikutana na mumewe kupitia riadha kabla hata hawajabalehe, sasa anawatunza watoto wao na mama mkwe wake.

"Angekuwa nembo kwa nchi yake," anasema Timnit Aregawi.

"Alikuwa jasiri, sio tu kwa familia yake. Alikuwa kila kitu kwangu. Sijioni kuwa niko hai baada ya kifo chake. Ninakabiliwa na magonjwa na matatizo. Nimeathirika kisaikolojia, naumia.”

Majeraha ya vita

Huenda mapigano hayo yamemalizika zaidi ya miezi 20 iliyopita lakini athari za kihisia na kimwili za vita vya Tigray, vilivyosababisha njaa, bado ziko wazi katika eneo lote.

Kama ilivyo kwa kila sehemu, michezo pia iliathirika kutokana na uharibifu uliofanywa wa thamani ya dola za kimarekani milioni 1.7 kwa vifaa vya mafunzo.

Mkuu wa bodi ya michezo ya jimbo hilo anasema, mzozo huo umegharimu maisha ya takribani wanariadha 100, makocha na wasimamizi.

"Wengi wao wangeshiriki mashindano ya kimataifa," anasema Kidane Teklehaymanot.

"Wangeweza kuwa chanzo cha mapato kwa familia zao na nchi yao."

Kijana Belaynesh Yaya alikuwa mkimbiaji mwingine, aliyekuwa na mustakabali mzuri kwenye eneo huo.

Kaka yake Habtamu Yaya anasema, “kukimbia ni kama utamaduni katika wilaya yao. Belaynesh alijifunza kutoka kwa mababu zake. Niliamini angeweza kuiwakilisha nchi yake.”

"Angekuwa katika timu ya Olimpiki mwaka huu. Ndoto yangu ilikuwa ni kumuona katika mbio za kimataifa.”

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 18 alitarajia kufuata nyayo za mabingwa wa Olimpiki wa Ethiopia Meseret Defar na Haile Gebrselassie, lakini hali ya mambo ilimpeleka katika mwelekeo tofauti.

Alikuwa na uhitaji wa pesa kabla ya mzozo kuanza, alijiunga na jeshi la mkoa - kinyume na matakwa ya baba yake.

"Sikuwa na furaha," anasema Yaya Gebresamuel. “Baba hawezi kuruhusu mtoto wake aingie motoni. Nilipendelea sana kumuona katika riadha kuliko jeshi.”

Alikuwa akipigana karibu na kijiji cha familia yake na akamwambia baba yake kwamba marafiki zake wamefariki.

"Nilisisitiza nimtoe jeshini lakini aliona bora kufa kuliko kurudi nyuma," anasema Gebresamuel. "Familia yote ilimsihi lakini alikataa."

Hatimaye, mkimbiaji huyo aliuawa akipigana pamoja na vikosi vya Tigrayan. Familia yake bado haijaona kaburi lake alipozikwa.

Kituo cha Maychew

Kocha Mekuria pia alimfundisha Belaynesh Yaya huko Maychew. "Alikuwa kama binti yangu. Alikuwa na nidhamu,” anasema.

"Walikuwa wakifanya mazoezi kwa bidii mchana na usiku. Walikuwa wachapa kazi. Hatukutarajia vita kutokea na hatukufikiri wangejiunga na jeshi."

Uwanja wa Maychew umesaidia kutoa washindi wa medali za Olimpiki kutoka Ethiopia, nyota kama Gudaf Tsegay, ambaye alitwaa shaba katika mbio za mita 5,000 kwenye Michezo ya Tokyo 2020 na ndiye bingwa wa dunia wa mita 10,000.

Kizazi kijacho cha wanariadha wa Tigray wanarejea katika mazoezi katika uwanja wa Maychew, licha ya hali mbaya ya baadhi ya vifaa.

Kuna nyufa kubwa na ndefu katika kuta za kituo cha mafunzo na plasta imebanduka kwenye kuta nyingi.

Ingawa athari ya muda mrefu kwa michezo ya Ethiopia bado haijafahamika, lakini gharama ya kibinadamu ya vita hivyo huko Tigray iko wazi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla