Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Mzozo wa Tigray wa Ethiopia: Makubaliano ya amani yaafikiwa

Inakuja baada ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliyowezeshwa na AU na kusuluhishwa na Olusegun Obasanjo.

Moja kwa moja

  1. Na hadi basi tumefika mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja leo hii

  2. Habari za hivi punde, Mzozo wa Tigray wa Ethiopia: Makubaliano ya amani yaafikiwa

    Makubaliano ya amani yamefikiwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Ethiopia huku pande zote mbili zikikubaliana kumaliz uhasama baada ya miaka miwili ya mapigano.

    Umoja wa Afrika (AU) umeiita "mwanzo" mpya, kulingana na shirika la habari la AFP.

    Inakuja baada ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili yaliyowezeshwa na AU na kusuluhishwa na Olusegun Obasanjo.

    Vita hivyo kati ya vikosi vya Ethiopia na waasi wa kaskazini mwa Tigray vilisababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu.

    Takriban thuluthi moja ya watoto wa eneo hilo wanakabiliwa na utapiamlo.

    Ingawa ni mafanikio makubwa, itapokelewa kwa tahadhari fulani. Hii si mara ya kwanza ya kusitisha mapigano katika mzozo huo - ule wa awali ulikiukwa mwezi Agosti, miezi michache tu baada ya pande zote mbili kujitolea.

    Wakati huu, makubaliano yameenda mbali zaidi. Maafisa wa serikali ya Ethiopia na wawakilishi wa chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) wametia saini mpango wa kupokonya silaha na kurejesha huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na misaada.

    "Ethiopia ina kikosi kimoja tu cha ulinzi wa taifa," inasomeka taarifa ya pamoja.

    Waziri Mkuu Abiy Ahmed ameelezea makubaliano hayo kuwa ya "kumbukumbu" na amejitolea kuyatekeleza.

    Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo, ambaye alikuwa mpatanishi wa mpango huo alikubali baada ya wiki moja ya mazungumzo nchini Afrika Kusini, alisema huo ni mwanzo tu wa mchakato wa amani.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema ni "hatua ya kwanza inayokaribishwa, ambayo tunatumai inaweza kuanza kuleta faraja kwa mamilioni ya raia wa Ethiopia ambao wameteseka sana wakati wa vita hivi".

    Tigray imejitenga na ulimwengu wa nje kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita, hospitali zimekuwa zikikosa dawa, huku umeme, simu na huduma za benki zikikatwa, pamoja na mtandao.

    Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa ukatili, ni pamoja na utakaso wa kikabila na unyanyasaji wa kingono.

    Baadhi ya unyanyasaji mbaya zaidi umelaumiwa kwa wanajeshi wa Eritrea wanaopigana pamoja na vikosi vya serikali na baadhi wamebainisha kwa tahadhari kwamba Eritrea haikuwakilishwa katika mazungumzo hayo.

    Vita vilianza karibu miaka miwili iliyopita hadi siku - 4 Novemba 2020 - wakati vikosi vya watiifu kwa chama kilicho madarakani huko Tigray, Tigray People's Liberation Front (TPLF), kiliteka kambi ya kijeshi, na kusababisha jeshi la Ethiopia kuteka eneo hilo, kabla ya baadaye kusukumwa nje ya wengi wake.

    Hii ilifuatia kuvunjika kwa uhusiano kati ya serikali na TPLF, ambayo ilikuwa imetawala Ethiopia nzima kwa miongo miwili hadi Waziri Mkuu Abiy Ahmed alipoingia madarakani mnamo 2018.

  3. Urusi yabadili msimamo na kurejelea makubaliano ya usafirishaji nafaka ya Ukraine

    Siku kadhaa baada ya Urusi kusitisha uungwaji mkono wake wa makubaliano ya usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi, imekubaliana na Uturuki kuanzisha tena ushiriki wake katika makubaliano hayo.

    Siku ya Jumamosi Urusi iliishtumu Ukraine kwa kutumia njia salama ya usafirishaji nafaka kushambulia meli zake mjini Crimea.

    Hata hivyo, Umoja wa Mataifa, Uturuki na Ukraine zimeendelea na mpango huo hata baada ya Urusi kusitisha ushiriki wake.

    Sasa, Wizira ya Ulinzi ya Urusi inasema Kyiv imepeana imetoa hakikisho la maandishi kutotumia njia hiyo kwa hatua za kijeshi.

    Lakini waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alisema ilionyesha kile ambacho jumuiya ya kimataifa inaweza kufikia iwapo itakataa kudanganywa na Urusi.

    Makubaliano hayo yalisimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki mwezi Julai, na kuhitimisha hatua ya Urusi kuzingira bandari za Ukraine kwa miezi mitano hatua ambayo ilizuia usafirishaji wa mamilioni ya tani za nafaka na mafuta ya alizeti na kusababisha bei ya vyakula kupanda.

    Chini ya makubaliano hayo, meli zinaruhusiwa kupita kwenye njia salama kabla ya kukaguliwa na timu maalum ya uratibu nchini Uturuki na kisha kuendelea na safari kupitia Mlango wa Bahari wa Bosphorous.

    Mkataba huo unamalizika tarehe 19 Novemba na wale wanaohusika bado wanapaswa kukubaliana kurefusha.

    Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tani milioni 9.8 za nafaka, mafuta na maharagwe ya soya zimesafirishwa katika shehena zaidi ya 400 kote duniani tangu operesheni hiyo ilipoanza tarehe 3 Agosti.

  4. Hushpuppi alivunja sheria, Instagram yasema baada ya kuizima akaunti yake

    Instagram imeiambia BBC kwamba walizima akaunti ya mshawishi wa Nigeria na tapeli wa kimataifa wa hadhi ya juu, Hushpuppi, kwa sababu alivunja sheria zao kuhusu ulaghai.

    "Hatutaki mtu yeyote atumie programu zetu kulaghai au kupunja fedha za watu, na kuwa na sheria wazi dhidi ya shughuli za ulaghai - ikiwa ni pamoja na utapeli wa pesa," msemaji kutoka Meta, ambayo inamiliki Instagram, ilisema katika taarifa.

    "Tulizima akaunti ya @hushpuppi kwa kuvunja sheria hizi," taarifa hiyo iliendelea kusema .

    Hushpuppi, ambaye jina lake halisi ni Ramon Abbas, alikuwa akituma picha za kifahari kwenye Instagram yake, akionyesha maisha yake ya gharama ya juu kwa wafuasi wake milioni 2.8.

    Lakini maisha hayo ya anasa yalifikia kikomo ghafla baada ya kukamatwa huko Dubai, alikoishi, mnamo Juni 2020.

    Chini ya mwaka mmoja baadaye, alikubali hatia ya utakatishaji fedha katika mahakama ya Marekani na anachukuliwa kuwa mmoja wa walaghai wenye hadhi ya juu zaidi duniani, kulingana na FBI.

    Nyaraka za mahakama ambazo hazijafungwa zilionyesha kuwa katika njama yake ya mwisho, alijaribu kuiba zaidi ya $1.1m ($960m) kutoka kwa mtu ambaye alitaka kujenga shule nchini Qatar.

    Alikuwa na mtandao duniani kote, na baadhi ya mipango yake kuenea kutoka Malta hadi Mexico.

    Hati zilizowasilishwa California zinasema kwamba uhalifu wake uligharimu karibu $24m, na sasa anakabiliwa na kifungo cha miaka 20 jela.

    Licha ya kukiri kosa mwaka jana, Instagram haikuwa imeondoa akaunti yake wakati huo, ikisema walikuwa wameichunguza na kuamua kutoifunga.

    Kuzimwa sasa kwa akaunti yake kuligunduliwa na vyombo vya habari vya Nigeria siku ya Jumapili.

    Sheria za Meta kuhusu ulaghai zinasema zinajaribu "kuzuia shughuli za ulaghai ambazo zinaweza kudhuru watu au biashara".

    Soma zaidi kumhusu Hushpuppi hapa

  5. Lori la Monusco lateketezwa katika shambulio la DRC

    Lori moja la vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa lilichomwa moto usiku wa Jumanne na wafanyakazi wa Umoja huo kujeruhiwa walipokuwa “wakijiondoa kimkakati” kutoka eneo lililotekwa na waasi wa M23 Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Mwanahabari wa ndani aliambia BBC kwamba “raia wenye hasira” walishambulia msafara wa huo katika eneo la Kanyaruchinya, umbali wa karibu kilomita 10 kaskazini mwa mji wa Goma, kuwajeruhiwa baadhi ya maafisa wa UN.

    Katika taarifa, kikosi hicho cha cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kinachofahamika kama Monusco, kilisema wanajeshi wake walipiga risasi kutawanya umati huo na "kufanikiwa kuondoka kwenye eneo la tukio", na kuongeza kuwa wahandisi wake wawili kutoka Bangladesh walijeruhiwa.

    Jumanne mchana, wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, ambao wanapigana pamoja na jeshi la DR Congo, walisema "wanajiondoa kimkakati na kimbinu" kutoka Rumangabo.

    Waasi wa M23 waliteka kambi ya kijeshi ya Rumangabo, kambi kubwa zaidi karibu na Goma, kufuatia mapigano mwishoni mwa juma na mapema wiki hii.

    Kikosi cha Umoja wa Mataifa, ambacho ni ujumbe wa pili kwa ukubwa wa Umoja wa Mataifa duniani, kimekosolewa kwa kushindwa katika dhamira yake ya kuleta utulivu mashariki mwa DR Congo.

    Maandamano ya kupinga ujumbe huo mwezi Julai katika jimbo la Kivu Kaskazini yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 35, maafisa wanasema.

  6. Korea Kaskazini yarusha makombora mengi zaidi kwa siku moja- Kusini yajibu

    Korea Kaskazini na Korea Kusini zimerushiana makombora kadhaa katika hatua ambayo imeongeza uhasama kati ya nchi hizo mbili.

    Kaskazini ilirusha makombora mengi zaidi kwa siku moja-karibu 23- ikiwemo moja ambayo ilianguka chini ya kilomita 60 kutoka mji wa kusini wa Sokcho.

    Seoul ilijibu kwa kutumia ndege ya kivita kurusha makombora matatu kutoka angani kwenda ardhini katika eneo la mpaka linalozozaniwa.

    Baadaye Pyongyang ilirusha makombora sita zaidi pamoja na msururu wa silaha zingine 100.

    Kaskazini inasema hatua hiyo inatokana na mazoezi makubwa ya kijeshi yanayofanywa kwa sasa na Korea Kusini na Marekani, ambayo inayaita "ya fujo na ya uchochezi".

    Siku ya Jumanne, Pyongyang ilionya kuwa watajutia hatua hiyo "katika historia" ikiwa wataendelea na mazoezi yao ya pamoja ya kijeshi, onyo ambayo inaonekana kama tishio la kutumia silaha za nyuklia.

    Kaskazini imefanyia majaribio idadi kubwa ya makombora mwaka huu huku hali ya wasiwasi ikiongezeka.

    Majibizanoya silaha ya Jumatano yalianza kwa kurusha makombora na Pyongyang katika maji karibu na Korea Kusini, na kusababisha ving'ora vya anga vya Ulleung, kisiwa kinachodhibitiwa na Seoul kulia.

    Kombora moja la balistiki lilivuka Laini ya Kikomo cha Kaskazini (NLL), mpaka wa baharini unaozozaniwa kati ya Korea mbili.

  7. Rapa wa Migos Takeoff aliuawa 'kimakosa'- yadai lebo yake

    Rapa wa Migos Takeoff aliuawa "kimakosa", kampuni yake ya kurekodi imedai katika taarifa.

    Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 28, aliyeteuliwa kuwania tuzo ya Grammy alifariki siku ya Jumanne kwa kupigwa risasi mjini Houston, Texas.

    Ikitoa rambirambi, lebo yake ya rekodi ilisema katika taarifa: "Vurugu zisizo na maana zimekatiza maisha mtu mwingine kutoka kwa ulimwengu huu na tumefadhaika."

    Mkuu wa Polisi wa Houston Troy Finner alisema hataki kueneza uvumi kwamba Takeoff ndiye aliyekuwa mlengwa wa shambulio hilo.

    Aliongeza: "Kulingana na kile watu wanasema juu yake, anaheshimika, hana jeuri. "Sitarajii kwamba alihusika na vurugu hizo lakini tunasubiri uchunguzi - hatuna sababu ya kuamini kwamba alihusika katika uhalifu wowote wakati huo, kama vile watu wanavyomuelezea kuwa mtu mpenda amani, mwenye upendo, na mcheshi."

    Aliwasihi walioshuhudia tukio hilo kujitokeza kutoa maelezo. "Tafadhali jitokeze, tupatie taarifa ili tuweze kuifariji familia hii ambayo hivi sasa inaumia," alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne alasiri.

  8. Video inayosambazwa mtandaoni kuhusu kifo cha mtoto wa Davido ni bandia- Polisi Nigeria

    Video ya mtoto aliyezama kwenye kidimbwa cha watoto kuogelea sio ya mtoto wa msanii nyota wa Nigeria Davido, mamlaka imesema.

    Video hiyo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inavuma kwa kasi huku baadhi ya watu wakisema mwathiriwa ni Ifeanyi Adeleke ambaye kifo chake cha Jumatatu katika makazi ya babake huko Lagos kinachunguzwa na polisi kwa sasa.

    Msemaji wa polisi alitaja video hiyo kama "feki".

    "Bado hatujaanza kukagua CCTV iliyopatikana nyumbani kwa Davido. Video yoyote unayoona mtandaoni si kitu halisi. Ni bandia,” msemaji wa polisi mjini Lagos, kitovu cha kibiashara cha Nigeria Benjamin Hundeyin aliambia BBC.

    Kitengo cha habari cha upotoshaji cha BBC kimethibitisha kuwa video inayoonyesha tukio la kuzama la Ifeanyi Adeleke ni picha ya CCTV ya mvulana wa miaka miwili akizama nchini China.

    Tukio lililoonyeshwa kwenye video hiyo lilitokea Uchina mnamo Agosti 23, 2019.

    Kisa cha mtoto mchanga kufa maji ilienea kwenye vyombo vya habari wakati wa tukio.

    Davido na mchumba wake Chioma Rowland, mpishi maarufu na mvuto, bado hawajatoa maoni yoyote kuhusu kifo cha mtoto wao.

    Siku ya Jumanne wafanyikazi wanane wa nyumbani wa mtu mashuhuri walialikwa kuhojiwa, sita kati yao wameachiliwa.

    Hundeyin alithibitisha utambulisho wa mmoja wa mshukiwa ambaye bado anazuiliwa kuwa yaya wa marehemu Ifeanyi.

    "Tunatumai kuwahamishia katika idara ya upelelezi wa jinai ya Serikali leo [Jumatano] kwa mahojiano zaidi," alisema.

  9. Mshindi wa kwanza wa medali ya Olimpiki nchini Kenya afariki akiwa na umri wa miaka 84

    Mwanariadha wa kwanza wa Kenya kushinda medali ya Olimpiki Wilson Kiprugut amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84, shirikisho la Riadha Kenya limetangaza.

    Nguli huyo wa masafa ya kati alifariki katika kaunti ya Kericho nchini Kenya Jumatano jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu.

    Kiprugut alifanya vyema katika ulingo wa kimataifa baada ya kushinda nishani ya shaba katika mbio za mita 800 katika Michezo ya Olimpiki ya 1964 jijini Tokyo.

    Alishinda medali ya fedha katika mbio hizo hizo katika Michezo ya Olimpiki ya 1968 huko Mexico.

    Katika taarifa, Riadha Kenya ilimsifu kama "mtu wa kweli wa kupendwa na mkarimu ambaye aliifanya nchi kujivunia kimataifa".

    Alishinda medali mbili za dhahabu katika mbio za mita 400 na 800 katika Michezo ya kwanza ya Afrika iliyofanyika Kongo-Brazzaville mnamo 1965.

  10. Kenya Power yaelezea kutoweka kwa umeme kote nchini

    Kampuni ya umeme nchini Kenya imetoa taarifa kuelezea kuhusu hitilafu ya umeme inayoshuhudiwa kote nchini.

    Katika taarifa iliyoandikwa Jumatano, Novemba 2, KPLC ilieleza kwamba inakabiliwa hitilafu ya kiufundi na kuwa inajitahidi kutatua suala hilo.

    Kenya Power ilitoa taarifa hiyo baada ya Wakenya kuangazia suala hilo mitandaoni wakilalamikia kutoweka kwa umeme bila mpango.

  11. Mbu wa Malaria kutoka Asia ahamia Afrika

    Wanasayansi wanasema kwamba aina vamizi ya mbu anayeeneza malaria kutoka Asia imeenea hadi Afrika, ambako ni tishio hasa kwa wakazi wa mijini.

    Barani Afrika, ambapo vifo vingi vya Malaria duniani hutokea, ugonjwa huu huenezwa zaidi na mbu maalumu kwa maeneo ya vijijini.

    Lakini aina ya mbu wa Anopheles stephensi, ambaye ndiye anayehusika na visa vingi vinavyoonekana katika miji ya India na Iran, huzaliana katika vyanzo vya maji mijini - na ni sugu kwa dawa nyingi za wadudu zinazotumika kawaida.

    Mbu huyo tayari amesababisha visa vya ugonjwa huo kuongezeka nchini Djibouti na Ethiopia, na hivyo kutatiza juhudi za kutokomeza ugonjwa huo.

    Watafiti wanasema iwapo atasambaa kwa wingi barani Afrika anaweza kuwaweka karibu watu milioni 130 hatarini.

  12. Uchaguzi wa Israel: Benjamin Netanyahu akaribia kurejea uongozini,kwa mujibu wa kura za maoni

    Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Benjamin Netanyahu yuko mbioni kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, kura za maoni zinasema.

    Makadirio hayo yanaipa kambi yake ya mrengo wa kulia viti vingi vidogo dhidi ya wapinzani wake wa mrengo wa kati wanaoongozwa na Waziri Mkuu wa sasa Yair Lapid.

    Matokeo kama haya yangeashiria kurejea kwa Bw Netanyahu, aliyepinduliwa mwaka jana baada ya miaka 12 mfululizo madarakani.

    "Tunakaribia ushindi mkubwa," aliwaambia wafuasi wa furaha mjini Jerusalem.

    Uchaguzi huo ulionekana na wengi kama kura ya au kupinga kurejea kwa Bw Netanyahu.

    Kura za maoni zinaonyesha kuwa kambi yake itaongoza viti 61 au 62 katika Knesset (bunge) yenye viti 120.

    Huku kukiwa na chini ya asilimia 85 ya kura zilizopigwa Jumanne kuhesabiwa, ilitarajiwa kuchukua hadi viti 65. Hata hivyo, hilo linaweza kubadilika huku kura zilizosalia zikichakatwa.

    Ili kupata wingi wa wabunge, Bw Netanyahu na chama chake cha Likud watategemea uungwaji mkono wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, chenye msimamo mkali wa Kidini wa Kizayuni.

    Viongozi wake wamejipatia sifa mbaya kwa kutumia matamshi dhidi ya Waarabu na kutetea kutimuliwa kwa wanasiasa "wasio waaminifu" au raia.

  13. Bustani ya Wanyama ya Taronga: Simba watano watoroka kwenye bustani ya wanyama ya Sydney

    Simba watano wamezua hali ya dharura kwa muda mfupi katika bustani ya maonyesho ya wanyama ya Australia baada ya kutoroka kutoka eneo hilo.

    Wanyama hao – mama na watoto wanne - walionekana nje ya maonyesho hayo katika Bustani ya Wanyama ya Taronga ya Sydney takriban 6:30 saa za huko Jumatano (22:30 GMT Jumanne).

    Maelezo kuhusu kutoroka kwa simba hao hayajatolewa.

    Lakini mkurugenzi mtendaji wa mbuga ya wanyama Simon Duffy aliliita "tukio kubwa" ambalo litachunguzwa.

    Picha za CCTV zilionyesha kuwa mlinzi aliinua kengele ndani ya dakika 10 baada ya kutoroka, mbuga ya wanyama ilisema.

    Wafanyikazi walijibu haraka kuwahamisha watu wote kwenye eneo hilo hadi maeneo salama, kulingana na Bw Duffy. Simba wanne "walirudi kwa utulivu" kwenye boma lao.

    Maonyesho ya simba yatasalia kufungwa hadi ukaguzi zaidi ili kuhakikisha kuwa ni "salama kwa 100%", Bw Duffy aliongeza.

    Wanyama kutoroka kwenye mbuga za wanyama za Australia ni jambo nadra.

  14. Moto Mlima Kilimanjaro waharibu nyaya mpya za mtandao

    Moto unaoendelea katika baadhi ya maeneo ya miteremko ya mlima Kilimanjaro umeharibu waya wa mtandao ambao ulifungwa miezi mitatu iliyopita na kufikia mita 3720 kutoka usawa wa bahari.

    Kebo zenye urefu wa zaidi ya kilomita 4 kwenye njia ya Marangu zilionekana kuharibika na hakuna muunganisho wa mtandao katika kambi hiyo ya mita 3720.

    Serikali ya Tanzania bado haijatoa hasara iliyosababishwa na moto huo unaoendelea.

    Moto huo ulianza Ijumaa jioni Oktoba 21 na tangu wakati huo umekuwa ukitokea katika maeneo mengi huku mamia ya wazima moto wakiuzima.

    Mvua ambayo imekuwa ikinyesha usiku wa kuamkia jana inasemekana kusaidia kupunguza moto huo katika baadhi ya maeneo.

    Kati ya jana jioni na leo asubuhi baadhi ya maeneo mlimani yalipata mvua.

  15. Marekani yawekea vikwazo kundi la IS nchini Somalia kutokana na ulanguzi wa silaha

    Marekani imeliwekea vikwazo kundi la Islamic State (IS) nchini Somalia na baadhi ya wanachama wake wanaodaiwa kusafirisha silaha kwa magendo Afrika Mashariki.

    IS inaendesha shughuli zake kaskazini-mashariki mwa nchi ambako inalenga vikosi vya usalama na raia katika mashambulizi.

    Licha ya kupata usaidizi wa kikanda na kimataifa, Somalia inaendelea kukabiliwa na ghasia mbaya za wanamgambo. IS Somalia imekuwa ikifanya kazi katika taifa hilo la Pembe ya Afrika tangu 2015.

    Watu waliowekewa vikwazo wanatuhumiwa kutoa msaada kwa kitengo cha kijasusi cha kundi hilo, kusafirisha silaha kwa njia ya magendo kote Afrika Mashariki na kuratibu mashambulizi ya hali ya juu.

    Baadhi walikuwa wanachama wa zamani wa kundi la al-Shabab. Mnamo Oktoba, Marekani iliorodhesha wanachama kadhaa wa al-Shabab pia wanaosemekana kuwa wanasafirisha silaha kati ya Somalia na Yemen ambapo al-Qaeda na Islamic State wamejikita.

    Mashambulizi makali ya makundi ya wanamgambo wa Somalia yamegharimu maisha ya watu wengi na kuzua hofu kubwa.

    Somalia inategemea sana usaidizi wa kimataifa ili kuvuruga silaha haramu na mitandao ya ufadhili ya shughuli za al-Shabab na Islamic State.

  16. Waziri wa Kenya aelekea Saudi Arabia baada ya vifo vya Wakenya wanaofanya kazi huko,

    Waziri wa maswala ya kigeni wa Kenya, Alfred Mutua, Jumanne aliondoka nchini humo kuelekea Saudi Arabia kukutana na mamlaka na watu wanaoishi nje ya Kenya ili kukusanya taarifa zaidi kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa Kenya katika maeneo ya Ghuba.

    Haya yanajiri baada ya taarifa za mwezi uliopita kwamba wanawake 85 Wakenya waliokuwa wakifanya kazi nje ya nchi, wengi wao wakiwa Saudi Arabia walikuwa wamefariki katika muda wa miezi mitatu iliyopita kulingana na Bw Mutua.

    Wanawake wengine 1,000 wa Kenya walikuwa wamerejeshwa makwao, aliongeza.

    Safari za Bw Mutua zinakuja baada ya mkutano uliofanyika Jumatatu na wawakilishi wa mawakala wa uajiri ambao huajiri Wakenya kwa kazi nchini Saudi Arabia na maeneo mengine.

    Mkutano huo, ambao aliutaja kama "mgumu na ufunuo wa kushangaza", ulikuwa na lengo la kutafuta suluhu za kudumu kwa wafanyakazi wa nje ya nchi.

    "Taarifa zilizokusanywa [kutoka kwa maajenti] zinaonyesha hadithi tofauti na ile inayovuma katika vyombo vya habari," Bw Mutua alisema.

    Mnamo 2021 wizara ya mambo ya nje ya Kenya ilisema Wakenya 89, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa nyumbani, walikufa nchini Saudi Arabia katika miaka miwili iliyopita. Vifo hivyo hata hivyo vilihusishwa na mshtuko wa moyo.

  17. Korea Kaskazini yarusha kombora kuvuka mpaka wa bahari wa Korea Kusini kwa mara ya kwanza

    Korea Kaskazini imerusha kombora kuelekea Kusini, ambalo lilivuka mpaka wa bahari wa nchi hizo mbili kwa mara ya kwanza tangu kugawanyika kwa peninsula hiyo. Kombora hilo la masafa mafupi lilitua umbali wa kilomita 60 kutoka mji wa Sokcho Kusini na kufyatua kengele za mashambulizi ya anga kwenye kisiwa cha Ulleungdo.

    Korea Kusini baadaye ilirusha makombora matatu kujibu Kaskazini. Rais wa Seoul Yoon Suk-yeol alikuwa ameuita uzinduzi wa Pyongyang "uvamizi wa wazi wa mpaka".

    Pyongyang ilirusha takriban makombora 10 "mashariki na magharibi" Jumatano asubuhi, jeshi la Korea Kusini lilisema. Baadaye siku ya Jumatano, jeshi la Korea Kusini lilisema limerusha makombora matatu ya angani hadi ardhini kuelekea kaskazini mwa mpaka wake wa baharini, kujibu kurusha Korea Kaskazini.

    Hapo awali ilikuwa imetangaza kuwa jeshi halingeweza "kuvumilia aina hii ya kitendo cha uchochezi cha Korea Kaskazini, na litajibu kwa uthabiti na kwa uthabiti chini ya ushirikiano wa karibu wa Korea Kusini na Marekani," walisema Wakuu wa Pamoja wa Wafanyakazi katika taarifa. Waliongeza kuwa Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol alikuwa ameamuru "jibu la haraka" kwa uchokozi wa hivi karibuni.

    Viongozi wa Korea Kusini na Japan wameitisha mikutano ya usalama wa kitaifa kujibu kurushiana makombora na Korea Kaskazini.

    Nchi zote mbili zilikuwa zimerekodi makombora hayo kabla ya saa 09:00 (00:00 GMT) siku ya Jumatano, likiwemo lile lililokiuka Laini ya Ukomo wa Kaskazini - mpaka wa baharini.

    Kombora hilo lilikuwa limetua katika maji 26km (maili 16) kusini mwa njia ya kuweka mipaka, 57km mashariki mwa jiji la Korea Kusini la Sokcho na 167km kaskazini-magharibi mwa kisiwa cha Ulleungdo.

    Hili lilikuwa "lisilo la kawaida na halikubaliki" kwani lilikuwa limeanguka karibu na "maji ya eneo kusini mwa Mstari wa Kikomo wa Kaskazini kwa mara ya kwanza" tangu peninsula hiyo igawanywe, alisema Kang Shin-chul, mkurugenzi wa shughuli za Wakuu wa Pamoja wa Wafanyakazi.

    Makombora hayo yanakuja siku moja baada ya Pyongyang kuzionya Marekani na Korea Kusini kusitisha mazoezi yake ya pamoja ya kijeshi wiki hii kuzunguka peninsula hiyo.

  18. Sasa watumiaji wa Twitter kulipa ada ya $8 kila mwezi kumiliki bluu tiki- Elon Musk

    Elon Musk amesema Twitter itatoza $8 (£7) kila mwezi kwa watumiaji wa Twitter ambao wanataka tiki ya bluu kwa majina yao ikionyesha akaunti iliyothibitishwa.

    Kama sehemu ya mabadiliko baada ya unyakuzi wa $44bn (£38bn) wa mtandao wa kijamii, Bw Musk alisema ni "muhimu kupambana na walaghai".

    Alama ya tiki ya bluu kando ya jina la mtumiaji - kwa kawaida kwa takwimu za wasifu wa juu - ni bure kwa sasa. Hatua hiyo inaweza kufanya iwe vigumu kutambua vyanzo vya kuaminika, wanasema wakosoaji. Bw Musk, mtu tajiri zaidi duniani, aliongeza kuwa watumiaji wanaolipwa watakuwa na kipaumbele katika majibu na utafutaji, na nusu ya matangazo mengi. "Nguvu kwa watu! Bluu kwa $8/mwezi," bilionea huyo alisema kwenye Twitter, akikosoa mbinu ya zamani ya uthibitishaji wa bluu kama "mfumo wa wakulima".

    Mbinu ya awali ya Twitter ya kuthibitisha watumiaji kwa tiki ya bluu ilijumuisha fomu fupi ya maombi ya mtandaoni, na ilihifadhiwa kwa wale ambao utambulisho wao ulikuwa unalengwa kwa uigaji, kama vile watu mashuhuri, wanasiasa na wanahabari.

    Kampuni hiyo ilianzisha mfumo huo mwaka wa 2009, baada ya kukabiliwa na kesi ikiishutumu kwa kutofanya vya kutosha kuzuia akaunti za walaghai. Lakini Bw Musk anakabiliwa na changamoto kubwa anapofanya kazi ya kurekebisha biashara ya Twitter, ambayo haijachapisha faida kwa miaka mingi. Amesema anataka kupunguza utegemezi wa Twitter kwenye matangazo, hata kama baadhi ya makampuni yamekua na wasiwasi kuhusu matangazo kwenye tovuti chini ya uongozi wake.

  19. Jeshi la Tanzania limetuma mamia ya wanajeshi kusaidia wazima moto Mlima Kilimanjaro,

    Jeshi la Tanzania limetuma mamia ya wanajeshi kusaidia wazima moto ambao wamekuwa wakipambana na moto kwenye kilele cha juu kabisa barani Afrika, Mlima Kilimanjaro, kwa karibu wiki mbili sasa.

    Maafisa wa Jeshi hilo wanasema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) litashirikiana na vyombo vingine na watu wa kujitolea kuhakikisha moto huo unadhibitiwa mapema kabla haujasababisha uharibifu mkubwa wa uoto wa asili katika mlima huo.

    "Maafisa na wanajeshi wa JWTZ tayari wamewasili katika maeneo ya Siha na Mweka mkoani Kilimanjaro tayari kukabiliana na moto," taarifa ya TPDF inasema.

    Timu ya BBC kwenye miteremko ya mlima huo ilishuhudia baadhi ya wanajeshi wakiwasili katika sehemu mbili za kuingilia mlima huo siku ya Jumanne.

    Msururu wa moto wa nyika umekuwa ukizuka katika maeneo tofauti mlimani, baada ya moto wa awali kuanza karibu na kambi kando ya njia maarufu ya kupanda milima tarehe 21 Oktoba.

    Mamia ya watu, wakiwemo wazima moto, wafanyakazi wa hifadhi ya taifa, waongoza watalii na raia, wamekuwa wakipambana kuzima moto huo bila mafanikio.

    Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana lakini serikali inasema shughuli za kibinadamu ndizo zinazoweza kulaumiwa.

    Serikali inasema ukame wa muda mrefu, tabaka za nyenzo za kikaboni zinazooza na upepo mkali ni sehemu ya sababu za moto umekuwa mgumu kudhibiti.

    Miaka miwili iliyopita, moto wa wiki nzima uliharibu maelfu ya hekta za misitu kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro.