Mzozo wa DRC: Je inawezekana kuyamaliza makundi ya wapiganaji Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo?

    • Author, Dinah Gahamanyi
    • Nafasi, BBC Swahili

Eneo la Mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo limekuwa kitovu cha mapigano ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuwasambaratisha wengine wengi kwa miongo zaidi ya miwili.

Mara hii wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika Mashariki wanakutana tena katika mji wa Mashariki mwa Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo wa Goma, kujaribu kubuni tena kikosi cha kikanda cha kumaliza makundi haya ya wanamgambo Mashariki mwa DRC. Wanatarajia kupanga sheria , vifaa na muda wa mwisho wa operesheni za kikosi hiki, licha ya kwamba kufikia sasa bado haijafahamika ni lini kikosi hicho kitaanza rasmi operesheni zake dhidi ya wanamgambo watakaokiuka maagizo ya kusitisha uasi.

Hata hivyo si mara ya kwanza kwa mkutano wa aina hii kufanyika na hata kuundwa kwa kikosi maalum cha kikanda cha kukabiliana na makundi ya wanamgambo katika Mashariki mwa Congo.

Licha ya juhudi za Umoja wa Mataifa, kupitia ujumbe wake wa walinda amani nchini humo Monusco na Vikosi vya kikanda vya kupambana na makundi vya wanamgambo hao, ghasia za mauaji ya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia zimekuwa zikiendelea kuripotiwa Mashariki mwa DRC.

Je makundi ya wanamgambo yanaweza kukomeshwa Mashariki mwa DRC?

Eneo la Mashariki mwa DRC lina makundi zaidi ya 100 ya wapiganaji wa msitu Wacongo ambao wamekuwa wakisababisha ukosefu wa usalama, kuwauwa raia na kupora mali katika eneo hilo.

Baadhi ya wachambuzi wanasema ni vigumu kwa mashambulio makubwa ya kijeshi kuwamaliza kabisa wapiganaji wa msituni kwani wajumbe wa makundi hayo wamekuwa na mtindo wa kujificham iongoni mwa raia wa kawaida wanapokabiliwa na mashambulio makali.

Hali hii ilijitokeza pale yalipofanyika mashambulizi makubwa yaliyolenga kumaliza uasi wa wanamgambo wa FDLR (wanaoshukiwa kutelekeza mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994) mwishoni mwa mwaka 2019, mashambulio ambayo yaliwauwa baadhi ya wapiganaji wakuu wa kundi hilo akiwemo Sylvestre Mudacumura.

Wakati huo baadhi ya maafisa wakuu wa jeshi la Rwanda walisema FDLR sio tatizo, lakini sasa kundi hilo limeanza kusikika likishutumiwa kufanya mashambulizi na sasa Rwanda inasema linashirikiana na jeshi la serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Unaweza pia kusoma:

Kwa upande mwingine kundi la Banyamulenge la M23 ambao ni Wacongo wenye asili ya Kitutsi , serikali ya DRC imekuwa ikiishtumu Rwanda kuwasaidia. Na kutokana hilo uhushiano kati ya Rwanda na DRC umekuwa mashakani mara kwa mara wanapoibua mashambulizi.

Mwaka jana majeshi ya Uganda yaliingia katika jimbo la Ituri Mashariki mwa DRC kupigana na wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF), ambao Uganda ilidai walihusika na mashambulio yaliyowauwa raia katika mji mkuu Kampala. Licha ya kuendesha operesheni dhidi yao ndani ya Congo, wapiganaji hao bado wanaendelea kuripotiwa kuendesha harakati zao na kuwauwa raia wasio na hatia.

Mnamo siku za hivi karibuni ilisemekana kuwa ''majeshi ya Burundi yaliingia kisiri'' katika jimbo la Kivu Kusini (Mashariki mwa DRC), kupigana na kikundi cha waasi wa Burundi cha RED-Tabara, na inadhaniwa kuwa kikundi hicho kina ngome yake katika milima ya jimbo hilo.

Kwa miaka zaidi 20, Jeshi la Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (FARD), limekuwa mashambulio mengi na ya mara kwa mara yanayolenga kuyatokomeza makundi ya wapiganaji bila mafanikio.

Baadhi ya wadadisi wanasema, kupakana Kijiografia kwa eneo la Mashariki mwa DRC na nchi jirani za Rwanda, Burundi, na Uganda ambazo zimekuwa na historia ya mizozo ya kivita na mauaji, ni hasara kwa eneo hili. Hii ni kutokana na kwamba baadhi ya makundi ya wapiganaji waasi waliozikimbia nchi zao wameweka ngome zao kwenye misitu mikubwa iliyoweza kufikiwa kwa urahisi Mashariki mwa DRC

Suluhu ya kudumu ya makundi haya, kulingana na wachambuzi wa taasisi ya International Crisis Group ni utashi wa serikali ya Kinshasa yenyewe na suluhu hiyo itapatikana kwa njia za amani.

Huenda Tathmini ya International Crisis Group ikawa sahihi kwa upande mmoja, ikizingatiwa mwanzoni mwa wiki hii kundi la wanamgambo wa DRC -Congo Economic Development Cooperative, Codeco, llilitangaza kusitisha uasi baada ya mazungumzo ya amani na serikali, kwa mujibu wa jeshi la nchi hiyo.

Codeco limekuwa ni mojawapo ya makundi hatari zaidi katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo , ambalo mwezi uliopita lilidaiwa kutekeleza mashambulizi ambapo raia wapatao 50 katika eneo la mgodi.

Hii ilifikiwa Jumatatu baada ya mazungumzo ya makabila mbali mbali katika jimbo la Ituri wakati kiongozi wa kabila la Lendu-ambalo linahusishwa na kundi hilo - kutangaza mkataba na serikali wa kumaliza uhasama.

Iwapo makundi mengine ya uasi yatafikia makubaliano na serikali na kuacha mashambulizi kama Codeco, na hivyo kulifanya eneo la Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia lenye utajiri mkubwa wa raslimali asili kuwa na amani, hakuna anayejua hilo kwa sasa.