Mzozo wa DRC na Rwanda : M23, majirani na bahati mbaya ya DRC

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Katika kueleza kuhusu nini hasa ni chanzo cha migogoro isiyokwisha ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mwanadiplomasia mmoja wa Tanzania amefananisha taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mnyama aitwaye twiga. Kwenye lugha ya Kiswahili, kuna msemo maarufu wa wahenga usemao; twiga anaponzwa na urembo wake.

Falsafa ya msemo huo ni kwamba wakati mwingine uzuri wa kitu huleta matatizo zaidi kuliko faida. Katika kufanya uchambuzi kuhusu kwanini serikali za DRC na Rwanda zimerushiana maneno katika siku za karibuni - kiasi cha DRC kuzuia ndege za Shirika la Ndege la Rwanda kuingia nchini humo, ni muhimu kuchambua kwanza matatizo ya kimsingi ya taifa hilo la Rais Felix Tshisekedi.

Kwamba DRC ni moja ya mataifa tajiri kwa rasilimali duniani. Ukitaka dhahabu, mafuta, almasi, miti, coltan, shaba, urani na takribani madini yote ya thamani yapo ndani ya taifa hilo. Unaweza kuigawa DRC kwa kutumia jiografia ya upatikanaji wa madini na mafuta tu - Mashariki dhahabu, Kusini urani na shaba, Magharibi mafuta na Kaskazini almasi. Katikati kuna msitu wa Congo wenye akiba kubwa ya miti ya aina mbalimbali.

Wakati dunia ilipovumbua baiskeli na baadaye magari, matairi yaliyotumiwa na magari yalitokana na mpira uliovunwa kwenye misitu ya Congo. Kwenye Vita ya Pili ya Dunia, bomu la nyuklia lililopigwa kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki lilitengenezwa kwa kutumia urani kutoka DRC. Simu za mikononi tunazotumia zinategemea betri na malighafi nyingine inayopatikana kwa wingi wapi - DRC.

Tatizo la kwanza ni hilo - utajiri. Ndiyo uliofanya wakoloni, baada ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1885, kutangaza taifa kuwa Congo Free State; kuwa ni taifa la watu kujichotea. Mataifa makubwa ya wakati huo kama Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yakaamua taifa hilo lisimilikiwe na mmoja wa "wakubwa" hao na badala yake liachwe liwe "shamba la bibi" la wote - Ubelgiji ikipewa jukumu la kulisimamia. Kimsingi, DRC ni taifa lililotengenezwa mazingira ya kutotawalika ili wanaotaka kulinyonya walinyonye bila kuingiliwa.

Jambo la pili kuhusu DRC ni kuhusu ukubwa wake. Ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba takribani milioni 2.3 - ikimaanisha ni kubwa kuliko muunganiko wa nchi zote wanachama wa EAC; yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini ukiziunganisha kwa pamoja. Kinachofanya ukubwa wake uwe changamoto ni umbile lake kijiografia kwani uwepo wa msitu mkubwa wa Congo unafanya maeneo mengi yasifikike kwa urahisi na Mto Congo ambao ni mpana na usiopitika kirahisi umefanya kazi ya kuiunganisha DRC kuwa ngumu.

DRC na makundi ya waasi

Mgogoro wa sasa, kwa mara nyingine, unahusisha Jeshi la DRC (FARDC) na waasi wa kundi la M23. Kundi la M23 linaundwa na raia wa taifa hilo wenye asili ya kabila la Watutsi. Ni kutokana na kabila lao hilo na kwa sababu ya baadhi ya makamanda wao kujulikana kuwahi kuwa sehemu ya Jeshi la RPA lililoung'oa madarakani utawala wa Rais Juvenal Habyarimana wa Rwanda mwaka 1994, uhusiano kati ya M23 na taifa hilo jirani umekuwa ni jambo la kujirudia mara kwa mara.

Kundi la M23 limeweka kambi yake upande wa Mashariki wa DRC ambao unafahamika kwa utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu. Haikuwa ajabu kwamba wakati kundi la Banyamulenge lilipoanza harakati zilizofanikisha kumng'oa madarakani Rais Mobutu Sesseseko mwaka 1997, kulikuwa na ushirikiano mkubwa kutoka kwa Jeshi la RPF la Rwanda ambayo wakati huo ilidai DRC inahifadhi wauaji waliofanya mauaji ya kimbari yam waka 1994 nchini kwake. Kwa sababu ya historia hiyo ya nyuma, kila wakati M23 inapoibuka, uhushiano kati ya Rwanda na DRC huwa shakani.

Ni bahati mbaya kwa DRC pia kwamba wakati yenyewe ikiwa na eneo kubwa na utajiri mkubwa wa rasilimali - inapakana na nchi kama Rwanda na Burundi zenye ufinyu mkubwa wa ardhi na rasilimali. Ni katika mazingira haya, DRC inaonekana kama sehemu ya nafuu kwa jirani zake hao 'kuhemea'.

Lakini ndani ya DRC, kuna makundi zaidi ya 100 vikundi vya waasi vyenye silaha na vinavyojiendesha kwa kutumia rasilimali za taifa hilo. Kama ambayo Mei 29 mwaka 1885 Wabelgiji walivyoamua DRC iwe shamba la bibi - hadi sasa utaratibu ambao unaendelea ndiyo huohuo wa kila mtu kujitwalia utajiri huo.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 wakati takribani mataifa tisa ya Afrika yalipojikuta ndani ya DRC kwenye vita iliyokuja kupachikwa jina la Vita Kuu ya Afrika - ziko taarifa kupitia ripoti za Umoja wa Mataifa (UN) na watafiti mbalimbali walioeleza namna majeshi yaliyokuwa upande wa hayati Rais Laurent Kabila, yalivyojilipa kwa kuvuna madini huku waliotaka kumng'oa rais huyo pia walivyojilipa kwa kutumia madini hayohayo ya DRC.

Labda Lumumba angebadili hali ya DRC?

Ingawa Mobutu alikaa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, Patrice Lumumba, anabaki kuwa kiongozi wa DRC aliyesisimua wengi zaidi wakati wa utawala wake wa muda mfupi. Hata hivyo, aliuawa na askari wa taifa lake katika tukio ambalo sasa kuna ushahidi kwamba nchi za Magharibi zilihusika katika mauaji yake.

Kosa la Lumumba lilikuwa nini? Katika hotuba zake za awali baada ya Uhuru wa DRC mwaka 1960, Lumumba alitangaza hadharani kuwa wakati wa taifa lake kuwa shamba la bibi ulikuwa umemalizika na kwamba Wakongomani sasa wangefaidi utajiri wao. Pengine hilo lilikuwa kosa lililogharimu utawala wake. Kwa wakati huo, na hata sasa, tamaa ya wakoloni na mataifa makubwa yalikuwa kwamba taifa hilo linatakiwa kubaki kuwa shamba la bibi.

Pamoja na mapungufu yake mengine kama kiongozi, Mobutu alidumu madarakani kwa muda mrefu kwa sababu moja kubwa - kuacha taifa lake libaki kuwa shamba la bibi. Ndiyo sababu alikuwa kipenzi cha mataifa ya Magharibi, akipewa misaada na mikopo mikubwa iliyokuwa ikifisadiwa lakini akiongezewa kwa sababu ya kuachia wakubwa watafune utajiri wake.

Wakati mbaya kwa mgogoro?

Kwa vyovyote vile, huu si wakati mzuri - kama kuna wakati ambao ni mzuri kwa vita, kuanzisha mgogoro wowote wa kijeshi kwenye eneo la Maziwa Makuu. Kuna hatari kubwa kuwa mgogoro wa aina yoyote sasa unaweza kuwa na maafa makubwa katika eneo hilo. Hii ni kwa sababu, nchi za Magharibi sasa zimeelekeza macho yake kwenye mgogoro wa Urusi na Ukraine na hali mbaya ya uchumi inayosababishwa na hilo.

Nchini Kenya - ambako Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akijihusisha sana na masuala ya DRC, wanaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti mwaka huu na rais huyo sasa hawezi kufanya uamuzi wowote mkubwa wa kiulinzi na kiusalama na badala yake atamwachia mbadala wake ahangaike na jambo hilo.

Tanzania - ambayo imeshiriki katika jitihada kadhaa kijeshi na kimikakati nchini DRC, sasa ina Rais mpya, Samia Suluhu Hassan, ambaye bado anajaribu kuweka sawa mambo yaliyo mkononi kwake, nchini kwake na si mtu anayeweza kuingia taifa lake katika masuala mengine mazito kwake.

Afrika Kusini ambayo ndiyo taifa kuu miongoni mwa nchi wanachama wa SADC ina matatizo ya kiuchumi na kisiasa na ndani na imeshindwa hata kufanya makubwa kutatua matatizo ya kiusalama ya jirani zake wa Msumbiji. Katika hali ya kawaida, ni vigumu kuona ikiingiza miguu yote kwenye mzozo wa DRC wakati huu.

Nchi nyingine mbili zingeweza kuingia DRC kwa mwavuli wa SADC; Msumbiji na Zimbabwe. Lakini Msumbiji ina matatizo yake ya ndani na bila shaka kwa sababu ya msaada ambao majeshi ya Rwanda yanautoa kwake kwenye kupambana na ugaidi; ni wazi itaangalia kwanza RPF iko upande gani kabla ya kujiingiza huko. Zimbabwe ina matatizo yake yenyewe ya kiuchumi na kisiasa.

Pengine Angola peke yake ndiyo inaweza kufanya chochote sasa ndani ya DRC kwenye kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa sasa. Lakini, Angola peke yake inawezaje kuutafuna mfupa uliowashinda 'fisi'?

Hiyo ndiyo bahati mbaya ya DRC.