Kwanini DRC Mashariki ni eneo hatari?

Watu 19 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mtu mwenye silaha kusahambulia soko la samaki nchini Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Tukio hilo limetokea karibia na mji wa Ituri uliopo kwenye pwani ya ziwa Albert.

"Maiti 19 ziligunduliwa katika kijiji cha Tara, na watu wengine wanane kujeruhiwa," Pilo Mulindo, kiongozi wa jadi wa eneo hilo amenukuliwa na shirika la habari la kimataifa la AFP.

Maiti hizo zimegundulika Jumapili na tukio lilitokea Jumatano ya wiki iliyopita.

Hakuna kundi la waasi ambalo limejitokeza kukiri kuhusika kwenye mauaji hayo. Lakini eneo hilo linafahamika kwa vita ya kikabila baina jamii za Hema na Lundu.

Mapigano ya makabila hayo mawili yameshapelekea vifo vya watu zaidi ya 100 na wengine zaidi ya 300,000 kuvuka ziwa Albert na kutafuta hifadhi kama wakimbizi nchini Uganda.

Amani mashariki ya DRC

Ingawa maeneo karibu yote ya DRC yamekuwa yakikumbwa na changamoto za usalama kama vita ama kushambuliwa na waasi mara kwa mara, eneo la mashariki ya nchi hiyo ndiyo lililoathirika zaidi.

Akiongea na BBC siku chache kabla ya kuondoka madarakani mwishoni mwa maka 2018, rais mataafu wa nchi hiyo, Joseph Kabila amesema katika mambo ambayo angekuwa na muda zaidi kuyashughulikia ni kurudisha amani kwa taifa hilo.

Mashariki mwa DRC kuna makundi ya kijeshi ya waasi na kikabila mengi kupindukia.

Baadhi ya makundi yanaondwa na raia wa nchi hiyo, lakini kuna amakundi mengine makubwa ambayo yanafadhiliwa ama kupambana za serikali za nchi jirani.

Baadhi ya makundi ya waasi yanayotokea nchi jinani ni FDLR ambalo lilitekeleza mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na wapiganaji wake kukimbilia DRC.

Waasi wa ADF wanatokea nchini Uganda.

Makundi hayo ya waasi yanatumia misitu mizito iliyopo kwenye eneo hilo kujificha na kuendesha shughuli zao huku wakitangaza nia ya kushambulia nchi zao walizozikimbia.

Uganda na Rwanda zimeshavamia DRC mara mbili kwa lengo la kusambaratisha makundi hayo na vita hizo kupelekea mamilioni ya watu kufariki.

Eneo hilo la Mashariki ya DRC pia linakabiliwa na ugonjwa hatari wa Ebola ambapo moja ya sababu za kushindikana kushughulikiwa kikamilifu ni uwepo wa makundi ya waasi hao.

Mwezi Machi mwaka huu shirika la habari la kimataifa la Reuters liliripoti kuwa, kundi la waasi la Mai Mai lilishambulia kambi ya matibabu ya Ebola na kuua polisi na kufurusha wagonjwa na wahudumu wote wa afya.

Makundi hayo pia yamekuwa pia yakishutumiwa kwa ubakaji wa wanawake katika maeneo wanayoyashambulia, na kufanya ubakaji kuwa ni moja ya matatizo makubwa yanayolikumba eneo hilo.

Uwepo wa makundi hayo ya waasi yamefanya Umoja wa Mataifa kupeleka kikosi maalumu (MONUSCO) kulinda amani. Hata hivyo, wachambuzi wengi wamekuwa wakilaumu vikosi hivyo kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.