Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu majengo 10 marefu zaidi barani Afrika 2025
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Ni idadi ndogo tu ya miji mikuu ya kifedha na kibiashara iliojivunia mandhari kubwa, kama vile Cairo, Johannesburg, Lagos na Nairobi.
Hata hivyo, kutokea miaka ya 2000, majumba marefu yamejengwa katika miji mingine mingi ya Afrika kulingana na mtandao wa Wikipedia.
Makala haya yanaorodhesha majumba marefu zaidi katika bara la Afrika.
1.Iconic Tower
The Iconic Tower ni jumba refu lenye matumizi mchanganyiko katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala wa Misri.
Likiwa na urefu wa mita 400 (futi 1,300), ndilo jengo refu zaidi barani Afrika.
Jengo hilo lina ghorofa 77, nyingi zikiwa za matumizi ya ofisi.
2. Msikiti Mkuu wa Algiers
Djamaa el Djazaïr unaojulikana kama Msikiti Mkuu wa Algiers ulifunguliwa mwezi Aprili 2019, ukiwa na mnara mrefu zaidi ulimwenguni.
Msikiti huo ni wa tatu kwa ukubwa duniani baada ya Msikiti Mkuu wa Mecca na Al-Masjid an-Nabawi wa Madina huko Saudi Arabia.
Msikiti huo una jumba la maombi (salat) lenye ukubwa wa 22,000 m2 (240,000 sq ft), linaloweza kutumika na takriban waumini 120,000.
3. Mohammed VI Towers
Jumba la Mohammed VI lina ghorofa 55, na urefu wa mita 250 (futi 820) katika jiji la Salé, linalopakana na Rabat, mji mkuu wa Morocco.
Ni jengo refu zaidi nchini Morocco na la tatu kwa urefu barani Afrika.
Ni mradi wa mfanyabiashara wa Morocco Othman Benjelloun na kuongozwa na kampuni ya O'Tower.
4. Leonardo Sandtone
Leonardo ni jengo lenye ghorofa 55 lenye matumizi tofauti huko Sandton, Johannesburg, Afrika Kusini.
Jengo hilo ambalo ni la nne kwa urefu barani Afrika ndilo refu zaidi Afrika Kusini na Jangwa la Sahara.
Lina urefu wa mita 234 ikiwa ni futi 768.
Jengo hilo limejengwa katika Mtaa wa 75 Maude, takriban mita 100 kutoka Soko la Hisa la Johannesburg.
5. Carlton Center
Jumba la Carlton Center ni jumba lenye ghorofa 50 na kituo cha ununuzi kilicho jiji la Johannesburg, Afrika Kusini.
Likiwa na urefu wa mita 223 (futi 732), limekuwa jengo refu zaidi barani Afrika kwa miaka 46 tangu kukamilika kwake mwaka wa 1973.
6. Msikiti wa Hassan II
Msikiti wa Hassan II ni msikiti uliopo Casablanca, Morocco. Ni msikiti wa pili kwa ukubwa barani Afrika na ni wa 14 kwa ukubwa duniani.
Mnara wake ni mnara wa pili kwa urefu duniani ukiwa na mita 210 (futi 689).
Ulikamilishwa mnamo 1993, chini ya mwongozo wa Mfalme Hassan II.
Jumba hilo lina ghorofa 60.
7. Commercial Bank of Ethiopia Headquarters
Makao Makuu ya Benki ya Biashara ya Ethiopia ni jumba refu zaidi mjini Addis Ababa, Ethiopia ambalo lilikamilika tarehe 13 Februari 2022 na kuwa jengo refu zaidi nchini Ethiopia.
linatumika kama makao makuu ya Benki ya Biashara ya Ethiopia yanayomilikiwa na serikali, benki kubwa zaidi nchini humo.
Pia ni jengo refu zaidi katika Afrika Mashariki
8. BRITAM TOWERS
Britam Tower ni jengo la kibiashara jijini Nairobi linalomilikiwa na British-American Investments Company (Britam).
Jengo hilo ambalo ndilo refu zaidi nchini Kenya, lina urefu wa mita 195 (futi 640) kutoka ardhini, likiwa na ghorofa 32 zinazoweza kutumika.
Jengo hili lina umbo la kipekee la prismic, ambalo huanza kama alama ya mraba ya pande nne na kuishia na paa la pande mbili na mlingoti wa mita 60 (197 ft)
9. Nairobi GTC Office Tower
Jumba la Global Trade Center (GTC Office Tower) ndio refu zaidi kati ya majumba ya Global Trade Center jijini Nairobi yanayomilikiwa GTC Industry Ltd.
Jumba hilo lina urefu wa mita 184 (futi 604) na ghorofa 42.
10. Jumba la Ponte City
Jumba la Ponte City ni jengo lililopo katika wilaya ya Berea ya Johannesburg, Afrika Kusini, karibu tu na Hillbrow.
Iilijengwa mwaka 1975 na lina urefu wa mita 173 (futi 567.6).
Limekuwa jumba refu zaidi la makazi barani Afrika kwa miaka 48, hadi lilipopitwa mwaka 2023 na Jengo la D01, katika Mji Mkuu Mpya wa Utawala wa Misri.
Ni Jengo la ghorofa 55.
Imehaririwa na Ambia Hirsi