Je, Dk. Bashiru Ally 'anajiandaa' kuitosa CCM?

    • Author, Markus Mpangala
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania

Mei 31 mwaka huu mwanazuoni, Dk. Bashiru Ally, atatimiza mwaka mmoja tangu alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania CCM akichukua nafasi ya Kanali Abdulrahman Kinana.

Uteuzi wake katika nafasi hiyo, Mei 31, 2018 ulikuja muda mfupi baada ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa kufuatilia mali za chama hicho. Majukumu yote hayo yalishangaza wengi, na hakika ni wachache tu ambao walikuwa wakijua kuwa mhadhiri huyo alikuwa ni kada wa CCM.

Bashiru alijijengea sifa na heshima miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa kuwa mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa na kijamii, na mara kadhaa alichukua msimamo mkali wa mawazo dhidi ya serikali na CCM yenyewe.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa majukumu yake katika nafa kuu ya utendaji wa chama, Dk. Bashiru ameonyesha namna gani anataka kuendana na kasi ya Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Pombe Magufuli.

Makala haya yanaangazia matamko au kauli ambazo Dk. Bashiru amekuwa akizitoa kwa kipindi chote tangu akabidhiwe madaraka hayo. Aidha, makala haya hayatajibu kila jambo bali yanaangalia mwelekeo wa Katibu mkuu huyo wa chama tawala.

Hivi karibuni Dk. Bashiru amezungumzia hatima yake iwapo atamaliza muda wa kuwa Katibu mkuu wa CCM. Upesi alieleza kuwa atarudi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tafsiri tunayopata kwa mwaka mmoja huu bado Dk. Bashiru Ali haonekani kuwa na mipango ya muda mrefu katika siasa. Kwamba haonekani kuwa anahitaji kuendelea kubaki kwenye siasa za utendaji mkuu na majukwaani. Kwa tafsiri nyingine Katibu huyo anaonesha hana mpango wa kuendelea kukitumikia CCM, kana kwamba amejiandaa kukitosa muda ukifika au kabla haujafika muda wake wa kung'atuka.

Kulalamikia viongozi vijana

Dk Bashiru Ally ameonekana 'kukilalamikia' chama chake kwa kushindwa kufanya kazi ya kuandaa viongozi bora kupitia jumuiya zake, hali inayosababisha kuwa na wanasiasa vijana ambao hawana maadili, hawana unyenyekevu, hawajali hisia za watu wala kuzingatia muktadha na masilahi ya chama hicho.

Akizungumza wakati wa misa ya mazishi ya Mwenyekiti wa kampuni za IPP, Reginald Mengi iliyofanyika katika kanisa la KKKT Usharika wa Moshi mjini, mkoani Kilimanjaro na kuoneshwa moja kwa moja kwa njia ya Televisheni.

Ikikumbukwe Katibu huyo amelalamikia mwenendo wa Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ambaye hadi sasa anamtaja kama mwanasiasa aliyepitia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wakati mfumo wa kuandaa viongozi ukiwa umekufa. Jambo hilo pia alililifanya septemba mwaka 2018 akielezea mwenendo wa kisiasa wa Mbunge huyo na wengine wa kariba yake.

Aidha, amemlalamikia Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye, ambaye amesema anahitaji kusikilizwa, kupikwa na kuongozwa zaidi katika siasa na uongozi ndani ya CCM na taifa kwa ujumla. Kurudiwa kwa matamshi ya Dk. Bashiru dhidi ya wabunge hao na CCM kwa ujumla wake kunaonesha anajaribu kujitenga na siasa za CCM pamoja na mwenendo wake uliokuwapo na unaoendelea sasa.

Dk. Bashiru amekuwa akilalamikia viongozi wasiofundishwa uongozi, hali ambayo inaonesha wazi Katibu huyo ni kama vile anatengeneza mlango wa kutokea CCM. Ni kama vile anawakebehi kwa kushindwa kukijenga chama au kukosa dira ya kuzalisha vongozi mahiri miongoni mwa wanasiasa vijana kutoka jumuiya zake.

Mwanachama mmoja mkongwe wa chama hicho amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa, "Katibu wetu anaonekana kama vile hahusiki na anajitenga na makosa ya viongozi ambao anaamini hawajapitia Chuo cha Diplomasia."

Kumsema 'Mkuu wa Mkoa Kipenzi cha Rais'

Tangu aingie madarakani Rais Dk. John Magufuli ameonekana dhahiri kumpenda Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda na mara kadhaa amemsifu hadharani.

Ikumbukwe mwaka 2017, rais John Magufuli alimtetea hadharani mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Utetezi huo ulikuja ikiwa ni muda mfupi tangu kutokea tukio la kuvamia ofisi za chombo cha habari, hatua ambayo ilimlazimu aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kuunda kamati ya uchunguzi chini ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile.

Dk. Bashiru Ally amemsema hadharani mara tatu mkuu wa mkoa kipenzi cha rais Magufuli, Paul Makonda. Mwaka 2019 akiwa kwenye ziara ya kichama mkoani Simiyu na pili akiwa kwenye Misa ya mazishi ya bilionea wa kitanzania, Dk. Reginald Mengi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Septemba 2018 katika mahojiano na gazeti la kila wiki la Raia Mwema, Dk. Bashiru alimuonya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam juu ya tabia yake ya kuwaita wakazi wa Dar es Salaam, wananchi (Mkoa) wangu. Bashiru alisema "Na hii habari ya Dar es Salaam ya Makonda, hakuna Dar es Salaam ya Makonda, ni Dar es Salaam chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda. Kuna wakati namsikia anasema wananchi wangu, nani kamwambia anao wananchi wake? Hakuna wananchi wako. Hakuna kiongozi anamiliki wananchi, ni wananchi wenzangu."

Mara ya tatu ni kwenye Misa ya mazishi ya Reginald Mengi mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Dk. Bashiru alisema, "Kuwa viongozi bora, watiifu, wanyenyekevu na wenye heshima, naomba nitumie fursa hii kumuombea msamaha kijana wangu Makonda mimi namfahamu na hii ni mara yangu ya pili namsema hadharani,"

"Mara yangu ya kwanza nilimsema Simiyu akaja analia ofisini nikasema ubadilike na kwa kweli ameanza kubadilika, bado ni kijana mzuri, shupavu lakini tunahitaji kuwasaidia vijana wetu," amesema Dk. Bashiru Ally.

Matamshi haya yanaonesha wazi Dk. Bashiru Ally si kama viongozi wengine ambao wanaogopa kumsema vibaya Mkuu huyo wa Mkoa wakitambua kuwa ni kiongozi kipenzi cha rais ambaye alikuwa chanzo cha kutimuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye. Wanachama wa CCM wanatambua kuwa ni vigumu kwa sasa kumsema vibaya Paul Makonda kisha wakaendelea kubaki kwenye wadhifa wao. Kwahiyo hatua ya Dk. Bashiru inawashangaza wengi na kuamini kuwa Katibu huyo ni kama vile 'hana cha kupoteza' hivyo yupo tayari 'kukitosa' chama hicho.

Chama na jumuiya 'kukosa nguvu'

Bashiru akiwa mtendaji mkuu wa CCM amepitia vipindi vya kawaida mno, huku chama chenyewe na Jumuiya zake nguvu zikiwa zimefifia mno katika siasa kwa ujumla wake.

CCM hakuna matamko ya kisiasa. Hakuna mihemko ya kisiasa wala pilika zozote ambazo zimezoeleka kuchangamsha siasa za nchi kati ya chama tawala na wapinzani wake. Pilika zote kisiasa 'zimeporwa' na serikali jambo ambalo linadhoofisha taasisi yenyewe ya chama na jumuiya zake.

Hakuna umahiri wa vijana katika anga za kisiasa dhidi ya wapinzani wa CCM, badala yake kila jambo limekuwa likijibiwa na Msemaji wa Serikali badala ya chama chenyewe 'kujibu mapigo'.

Mwandishi wa makala haya amewahi kumwuliza Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kuwa kulikoni chama kimekuwa bubu kwenye masuala ambayo yanahitaji majibu ya kisiasa kama sehemu ya siasa zenyewe? Hakukuwa na majibu halisi, angalau baadaye Katibu huyo alianza mabadiliko kwa 'kujibu mapigo' katika matamko ya kisiasa.

Hasara ya serikali 'kupora' shughuli za kisiasa za chama ni kuvunja nguvu, uimara na utamaduni wa kisiasa ambao ndiyo huibua umahiri wa wanasiasa kutoka ndani ya chama na kuleta ugumu kwenye zoezi zima la uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi mdogo au uchaguzi mkuu. Hayo yote yanatokea wakati Dk. Bashiru Ally ndiye mtendaji mkuu, kana kwamba hayaoni au amekubali kuwa nguvu ya wanasiasa wa serikali ndiyo imekua kubwa kuliko ya wanasiasa wa siasa.

Anafuata nyayo za Kinana ?

Tafsiri nyingine ya matamshi ya Dk. Bashiru Ally yanaonesha kufuata nyayo za mtangulizi wake, Abdulrahman Kinana, ambaye aliingia kwa gia ya kuonekana kama vile mtu ambaye hahusiki na ubovu wa viongozi wa chama na serikali. Kinana alifanya ziara ya kukagua utekelezaji Ilani ya CCM kama ambavyo Dk. Bashiru Ally afanyavyo sasa.

Ziara za Kinana akiwa sambamba na aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye zilianzia katika mikoa ya Tabora, Singida na Manyara ambapo inadaiwa kuwa iliongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho kati ya mwaka 2010-2015.

Nape na Kinana wamekuwa wakitajwa kurudisha matumaini ya wananchi kwa CCM, ambapo waliwataka mawaziri wanaohusika kwenda kutoa majibu ya malalamiko ya wananchi waliotoa tuhuma mbalimbali mbele yake.